December 30, 2016



Na Saleh Ally
GUMZO kubwa kwa sasa ni uamuzi wa uongozi wa Azam FC kuamua kuwatimua makocha wake wote ikianza na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.

Zeben ametimuliwa kazi baada ya kuiongoza Azam FC katika mechi 17 za Ligi Kuu Bara, ikiwa imeshinda saba, sare sita na kupoteza nne.

Katika mechi 17 washambuliaji wa Azam FC walifunga mabao 22 na difensi ikaruhusu mabao 15. Jambo ambalo mwisho viongozi unaona wameamua kuachana na Zeben na wenzake.

Kwanza si rahisi kuulaumu uongozi wa Azam FC kwa kuwa umeonyesha uvumilivu tofauti na awali walivyozoeleka.

 Kawaida mtu anayetaka mafanikio, mara nyingi hana uvumilivu wa kupita kiasi, anataka mambo yaende haraka.
Azam FC kufungwa mabao 15 katika mechi 17, maana yake bado haikuwa katika kiwango kizuri cha ulinzi na huenda uongozi ulijitahidi kuongeza wachezaji. 

Kuna hali fulani ya kushangaza, namna makocha hao walivyokuwa wakifanya mazoezi yao kwa juhudi kubwa kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.

Mazoezi yalikuwa yanaonekana kuwaingia vizuri wachezaji na walichangamka kweli. Waliyafanya kwa ufasaha na ungewaona Azam FC wakikutana na yoyote, angekuwa hatarini. Hawakufanya hivyo na ukweli, soka ni majibu kwa maana ya matokeo na si ubora au uzuri tu wa mazoezini.

Azam FC wameanza mazungumzo na Kali Ongala ambaye alikuwa Majimaji. Taarifa nilizonazo za uhakika, tayari Majimaji imeshamruhusu Kali kwenda Azam FC, hivyo huyo atakuwa kocha wao kipindi wanatafuta nguvu ya kocha mwingine kutoka nje wakiamini atakuwa msaada katika michuano ya kimataifa.

Siwezi kuwakataza Azam FC, lakini ninaweza kuwashauri kwamba wanaweza kuendelea kubadili makocha lakini huenda tatizo wakashindwa kulipata ambalo limo ndani na wamekuwa wakiliacha kila kukicha.

Kwanza lazima wajiulize, wachezaji wote waliosajiliwa, makocha kweli waliwataka. Au kuna watu walikuwa wakifaidika na inawezekana waliwalazimisha makocha au kuwashawishi ili wao wafaidike.

Azam FC lazima iangalie, kwamba hivi je, makocha wote ambao walitakiwa na makocha hao walipatikana? Kama walishindikana tatizo lilikuwa nini.

Kuna suala la wachezaji wengi wakongwe ambao mimi ninaamini wanaweza kuwa msaada au tatizo kulingana na wenyewe wanavyoamua.

Wachezaji wakongwe wa Azam FC, wamekaa kwa muda mrefu katika klabu hiyo na wengine walipanda nayo. Kama wakiamua upande mwingine, yaani si wa mwalimu, basi ni rahisi sana mwalimu huyo kufukuzwa kazi.

Ndani ya Azam FC, suala la maslahi haliwezi kukosekana. Suala la wale wanaotaka kufaidika badala kuifaidisha klabu hawawezi kukosekana na asili inaonyesha hivi, wanaojali maslahi yao binafsi ni wajanja kupeleka majungu kwa mabosi ili wengine waonekane wabaya na wao kuendelea kufaidika huku wakijificha na kivuli hicho cha fitna na majungu.

Uongozi wa Azam FC unastahili kusifiwa kwa uwekezaji, lakini lazima uhakikishe kuwa na watu sahihi ambao wanafanya kazi kwenye kile walichokianzisha. Lazima tukubali kuna tatizo kubwa la rasilimali watu, wengi sisi ni wavivu na majungu ni mtaji. 

Kuwaamini wahusika au wafanyakazi wako ni vema, lakini usimamizi wa karibu ni jambo bora zaidi ili kufikia kile kinachotakiwa. Kuwaamini wao kupindukia ni sahihi kwa kuwa kuna tatizo.

Wachezaji wakongwe wakiamua kuwa na mapenzi ya kuendeleza wengine, wakaamini kadiri siku zinavyosonga wanatakiwa kuwapa wengine nafasi ili Azam FC iendelee watakuwa msaada mkubwa sana kwa klabu.

Lakini wakiwa ni watu wasiokubali kutoa nafasi, wasioamini kuwa wanakwisha kutokana na muda. Basi mwisho wanageuka kuwa tatizo kubwa na huenda wakawa sehemu ya kuzuia maendeleo huku klabu ikihaha kuwatimua makocha kila kukicha.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic