December 12, 2016


Na Saleh Ally
KOCHA mpya wa Yanga, George Lwandamina ameanza vizuri sana kazi yake akiwa na kikosi chake hicho baada ya kuwa amepokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKU ya Zanzibar.

Mechi hiyo iliyoisha kwa Yanga kupoteza, imezua mijadala mingi sana mitandaoni na hasa kwa mashabiki wa Simba ambao Yanga ni watani wao, wametumia muda mwingi kuporomosha maneno mengi wakiwaeleza namna walivyofeli.

Kawaida kwa mashabiki wa soka na hasa unapozungumzia wa Yanga na Simba, mara nyingi hawaangalii suala la mechi ya kirafiki au la. Wanachojali wao ni kuona timu yao inashinda tu.

Hivyo kwa sasa, mashabiki wa Yanga, hakuna ubishi kwamba watakuwa hawana furaha kwa kuwa timu yao imefungwa na JKU kutoka Zanzibar ambayo walitarajia kuichakaza ikiwezekana kwa uchache angalau mabao matatu.

Wakati mwingine wanaweza kuwa sahihi, lakini kwa Lwandamina anaweza kuwa amepata faida kubwa kwa kuwa amepata nafasi kubwa ya kuwasoma wachezaji wakati wa mechi na si mazoezi tena.

Lwandamina alikipanga kikosi hicho namba hii; Ally Mustafa, Hassan Kessy, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Nadir Haroub, Said Juma, Juma Mahadhi, Matheo Antony, Obrey Chirwa, Malimi Busungu na Geofrey Mwashuiya.

Waliokuwa benchi ambao wengi wao waliingia katika kipindi cha pili ni Deogratius Munishi, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Andrew Vicent, Simon Msuva, Vincent Bossou, Thaban Kamusoko, Justin Zulu, Donald Ngoma Amissi Tambwe, Deus Kaseke na Kelvin Yondani.

Baada ya mechi, Lwandamina alisema alichotaka cha kwanza katika mechi hiyo hayakuwa matokeo. Badala yake ni kukisoma kikosi chake ili ajue nini cha kufanya wakati akiingiza mifumo yake.

Kwa mashabiki nimesema wana haki ya kuona hivyo kwa kuwa mtazamo wao si wa kiufundi kama ambavyo itakuwa kwa kocha. Nimesema kiasi fulani nawaunga mkono kwa kuwa jiulize, vipi mchezaji wa akiba wa Yanga ashindwe kufanya vizuri hata katika mechi dhidi ya JKU.

Kawaida, mchezaji anayekaa benchi anatakiwa kuwa bora ikiwezekana zaidi. Anatakiwa awe msaada na hatari zaidi kwa kuwa yeye huingia kutoa msaada mambo yanapoharibika.

Unaweza kunielewa hivi, mtu anayepigana halafu anatumia mkono wa kulia. Muda mwingi hutanguliza mkono wa kushoto. Anafanya hivyo kwa kuwa anaujua wa kulia ndiyo bora zaidi, utakwenda kumaliza kazi.

Lakini pia unajaribu kuangalia suala la wachezaji walioanza. Wengi wao walionekana kuwa na hofu, wasiokuwa na maamuzi sahihi na kama wale ambao hawajiamini. Hili si jambo zuri kwao.

Unapokuwa kwenye kikosi, mara nyingi wachezaji wanaokuwa benchi husema wanaweza lakini hawaaminiwi. Lwandamina ameonyesha kuna jambo analijua kuhusiana na saikolojia ya wachezaji, akaamua kuanza na wale wanaokaa benchi.

Wameshindwa kuitumia nafasi hiyo na wakaa benchi wamethibitisha kwamba wale wenzao waliokuwa wakianza wakati wa Kocha Hans van Der Pluijm, wanastahili kabisa kuendelea kuanza.

Kama imefikia hivyo, wamepewa nafasi na wameshindwa kuonyesha lolote kama msaada, basi huu ni muda mwingine wanapaswa kujipanga na kuutumia badala ya kugeuka na kuwa ‘wajuaji’.

Katika timu kuna majungu sana, mara kadhaa tumesikia wachezaji wakilalama kukosa nafasi kwa kisingizio kocha hawapendi au kadhalika. Wakipewa nafasi, hushindwa kuonyesha kwamba wanastahili kupangwa au kuanza.

Nafasi aliyowapa Lwandamina wachezaji wa Yanga, ilikuwa kubwa. Najua wako ambao wamefanikiwa kuitumia na wengine wameshindwa, ikiwa na maana hii. Sasa wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kuipata tena na isitokee ambao wataanza kulalama kwamba wanaonewa wakati wameonyesha ni watu wa ‘kumbwela’.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic