January 9, 2017Salaam wadau,

Kesho Jumanne usiku pale Amaan Stadium patachezwa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi baina ya klabu kongwe zaidi kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, Simba na Yanga. 

Ni mechi ya tano kwa miamba hiyo ya soka kukutana kwenye uwanja huo wenye historia pana sio Zanzibar tu, bali hata Tanzania kwa ujumla. 

Mara ya kwanza klabu hizi zilikutana mwaka 1975 kwenye fainali ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati, ambapo Yanga ilishinda kwa bao 2-0, mabao yakifungwa na marehemu Gibson Sembuli na baba yangu Al Haji Sunday Ramadhan Manara Computer, ni mechi iliokuwa kali na nilijuzwa ndio asili ya kumeguka kwa Simba na kuundwa klabu ya Nyota Nyekundu. 

Zama hizo babu yangu mzaa mama marehemu Hassan Haji alikuwa mwenyekiti wa Simba, na wanachama wa Simba wakahoji katika mkutano mkuu kwa nn Sunday atufunge kila siku au kwa kuwa ni mkwe wa mwenyekiti? Taarifa ya maneno hayo yaliibua sintofahamu kubwa klabuni, hali iliopelekea wanachama waasisi wa klabu(Waswahili kwenda kuanzisha klabu yao ya Red Star. 

Ikumbukwe game ya Zanzibar ilichezwa muda mfupi baada ya fainali ya ligi ya taifa pale Nyamagana Stadium Mwanza, ambapo Yanga ilifunga Simba kwa mabao 2-1, wafungaji wakiwa Sunday Manara na Gibson Sembuli.  

Moja ya jambo lingine la kukumbukwa kwenye mchezo huu ni kuzaliwa kwa mwandishi wa makala hii siku Yanga ikicheza na Mufurila Wonderes kwenye nusu fainali ya kombe hilo, ambalo Simba ndio timu ya kwanza kulitwaa na bingwa wa kihistoria wa muda wote wa ukanda huu murua.

 Mechi ya pili miamba hii kukutana ilikuwa pia katika fainali ya kombe hili, na Simba kulipa kisasi kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya Penati 6-5, huku mkwaju wa mwisho ukikoswa na beki wa Yanga, David Mwakalebela, Mungu alinijaalia kuishuhudia mechi hii kabambe mno pale Zanzibar.

Nilishuhudia ufundi wa hali ya juu katikati ya uwanja, baina ya Hussen Masha, Michael Paul, Ramadhani Lenny kwa upande wa Simba, na Issa Athuman, Method Mogella, Steven Mussa na Hamis Gaga kwa upande wa Yanga,

Kwangu hii ilikuwa mechi bora kuwahi kuishuhudia baina ya watani hao, ikumbukwe dakika 120 zilishuhudia sare ya 1-1, huku Simba ikitangulia kwa goli la Hussen Masha na Yanga wakisawazisha kwa bao la Said Mwamba 'Kizota'. Nikujuze pia jina la Taifa kubwa ndio lilipobamba wakati wa michuano hii mikubwa zaid kwa ngazi ya klabu kwenye eneo hili la Afrika. 

Mwaka huo wa 1992 tulishuhudia nusu fainali ya kombe la Muungano baina ya timu hizo, ukiwa ni mchezo wa tatu baina yao kuchezwa visiwani Zanzibar, mchezo huu Simba pia ilishinda bao 1-0, bao safi la mwalimu wa lugha ktk shule ya kimataifa nchini na Mrundi wa Kibaha, Daniel Kimti. Hii ndiyo game ya mwisho katika utawala wa Mikidadi Kassanda kama mwenyekiti wa Simba na baada ya hapo Marehemu Amiri Ally Bamchawi akawa Mwenyekiti wa Simba.

Kumbuka Bamchawi alikuwa meneja wa timu wakati wa mgogoro wa 1975, lakini baadae alirudi Simba hadi mauti yalipomkuta. 

Mechi ya nne na ya mwisho kuwakutanisha Simba na Yanga Zanzibar ni Januari 2011, kwenye kombe hili la Mapinduzi na ilikuwa ni mchezo wa fainali ambapo Simba Iliendeleza umwamba wake kwa kuitandika Yanga 2-0, mabao ya Shija Mkina na Mussa Hassan Mgosi, Meneja wa sasa wa kikosi cha Simba.

Nimekupeni historia hii murua vijana wa dotcom ili mpate kujua tulipotoka, mategemeo yetu pia kwa kesho,waamuzi watazingatia sheria 17 za soka. 

Tukutane kesho Amaan Stadium tukimkomala Nyani usoni. 


 Mwana kulitaka, Mwana kulipewa.

MIMI HAJI S. MANARA.

2 COMMENTS:

  1. Ninavojua uwanja wa amaan hauna viti tusije kung'oa nyasi na magoli

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV