January 30, 2017
Na Saleh Ally
MECHI ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji Simba dhidi ya wageni Azam FC, imeisha na gumzo kubwa ni kuhusiana na kipa Aishi Manula.

Mechi hiyo, ilikuwa ni ya ushindani huku ikichezwa kwa tahadhari kubwa na mwisho Simba wakalala kwa bao 1-0 lililofungwa na nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco.

Wakati Simba wanalala na Bocco akiendeleza ubabe wake kwa Simba. Gumzo kuu lilikuwa ni kipa Aishi Manula wa Azam FC ambaye alionyesha umahiri mkubwa.

 Manula alionyesha umahiri wa juu ambao unawezwa kutajwa kwa maneno mawili tu “yuko fiti” au kiwango chake kipo juu sana.

Kipa huyo wa Azam FC amekuwa kati ya wachezaji Watanzania ambao viwango vyao vinapanda kila kukicha. Jambo ambalo linaonyesha Manula atakuwa na jambo ambalo wachezaji wengi si makipa tu, wanapaswa kujifunza kutoka kwake.

Nakumbuka mwaka juzi mwishoni, timu ya taifa, Taifa Stars iliweka kambi jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Mechi kadhaa za kirafiki zikaandaliwa na moja ilikuwa ni dhidi ya timu ya vijana ya Afrika Kusini chini ya miaka 23.

Kipindi cha kwanza Manula alikuwa benchi na Stars ikawa nyuma kwa mabao mawili. Alipoingia, yeye akawa gumzo kutokana na umahiri akiwa ameokoa yeye na mshambuliaji mara nne, jambo ambalo lilimfanya Shaun Bartlett kocha wa timu hiyo kuuliza kuhusiana na Manula kuwa anakipiga nchi gani nje ya Tanzania.

Bartlett ambaye aliwahi kung’ara Ligi Kuu England akiwa na Charlton Athletic lazima atakuwa ni mchezaji ambaye sasa ni kocha mwenye uwezo wa kujua mchezaji bora au mwenye kipaji.

Aliulizia kuhusiana na Manula na moja kwa moja aliamini atakuwa anacheza nje ya Tanzania. Kipa huyo alifanya kazi kubwa katika mechi hiyo.

Inawezekana tukawa tumesahau, mara ya mwisho Azam FC inaifunga Simba ilikuwa katika fainali Kombe la Mapinduzi kwa bao 1-0. Manula pia ndiye aliyekuwa kizingiti kikubwa na alionyesha kuwa ni kipa hasa.

Mwisho alimaliza michuano ya Kombe la Mapinduzi bila ya kufungwa hata bao moja. Huku makipa wote wa timu za Zanzibar, Tanzania Bara na URA iliyotoka Uganda wakiwa wametumbukia nyavuni kuokota mipira.

Kwangu sioni hata kigugumizi kusema Manula sasa ndiye kipa bora zaidi  kupita wote kwa wale wenye uraia wa Tanzania lakini hata wale wanaoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kipa huyu sasa anaendelea kushikilia kiwango chake kwa ubora mzuri kwa zaidi ya miezi 30. Kiwango chake kimekuwa kikizidi kusogea mbele na si kuporomoka kama ambavyo mtu yeyote angetarajia iwe.

Tunajua wakati fulani wakati wa usajili kwa ajili ya msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2016/17, Azam FC walileta makipa kutoka nje wakitaka kumpa ushindani kwa maana wanaona michuano iliyo mbele yao ambayo ni ya kimataifa ni migumu sana.

Kipa kutoka Ivory Coast, mwisho ikaonekana Manula ana kiwango zaidi yake. Akapelekwa kipa kutoka Hispania, ikaonekana hauwezi mziki wa Mtanzania huyo anayechipukia kwa kasi.

Hakuna ubishi tena kuwa Manula ni hazina ya baadaye ya taifa letu. Vizuri anavyokwenda angeendelea na kwangu ninamuona ni mfano bora kwa vijana wengi kwa kuwa inaonekana ni kijana mwenye nia ya kufikia ndoto zake.

Hauwezi kufanikiwa kama hauna ndoto ya kufikia. Lakini ili ufanikiwe hasa lazima ujitume bila kuchoka, uwe mtu mwenye kukubali kujifunza na kujiongeza pia mwenye nidhamu ya juu kabisa.

Azam FC kama wanaendelea kumpatia kila kinachotakiwa zikiwemo changamoto. Kwa kuwa sasa hivi ni kati ya makipa bora kabisa Afrika Mashariki na Kati, basi itafikia siku atakuwa kipa bora Afrika. Binafsi nampa moyo wa kuendelea kusonga mbele na kumshauri, asilewe sifa hata chembe.0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV