January 28, 2017
Na Saleh Ally
MVUTO wa Ligi Kuu England unazidi kupaa hasa kutokana na namna ambavyo vigogo kama Manchester United, Arsenal na Liverpool wanavyoonekana si wenye chao au hawana uhakika.

Msimu uliopita, Leicester City ilichukua ubingwa kwa kuwashangaza wengi. Msimu huu inaonekana haina kitu na hata nne bora haitawezekana, hii inazidi kuonyesha hii ni ligi ambayo haina mwenyewe kama ilivyo Hispania, lazima uwazungumzie “wenye ligi” Real Madrid na FC Barcelona.

Kwa ilipofikia sasa ligi hiyo maarufu kama Premier League inazidi kuongeza utamu kwa kuwa Chelsea wanaongoza wakiwa na pointi 55, wanafuatia Arsenal wakiwa na 47 halafu Tottenham wakiwa na 46 na Liverpool wanakamilisha Top Four wakiwa na 43.

Angalia namba tano ambao ni Man City wana pointi 43 na jirani zao Man United wako nafasi ya sita walipokwama “topeni” wakiwa na pointi 41.

Hakuna anayepumua kwa raha, angalau Chelsea ambaye pengo lake la pointi nane linampa nafasi ya kuwa na ahueni lakini bado hana uhakika.

Angalia mechi zake tano zijazo, ndani ya mwezi mmoja, watakuwa wamecheza mechi hizo tano lakini utagundua katika mechi tano, mbili watakutana na vigogo.

Tena vigogo hao wanakutana nao katika mechi mbili za mwanzo wakianza Jumanne watakapowavaa Liverpool halafu Jumamosi ijayo Arsenal.

Baada ya hapo watakuwa na mechi nyingine dhidi ya Burnley, Swansea City na West Ham. Hapa pia hakuna timu ya kuidharau lakini kama watazicheza vizuri karata zaidi dhidi ya vigogo hao wawili watakuwa wameangusha ndege wawili kwa jiwe moja.Maana Chelsea ikichukua pointi sita kutoka Liverpool na Arsenal zilizo Top Four, watakuwa wameweza kuongeza ukubwa wa pengo na kujaza upande wao asilimia zaidi za kubeba ubingwa.


Lakini itawaongezea hali ya kujiamini kuhakikisha wanawaangusha Burnley, Swansea na West Ham ambao kamwe huwezi kutabiri hata kidogo.


Mechi hizo tano, pia zinaweza kuwa faida kubwa kwa Arsenal au Liverpool na hata Tottenham hasa kama watazicheza vizuri.


Tottenham si ya kuidharau hata kidogo kwa kuwa ukiangalia katika suala la safu ngumu ya ulinzi. Ni yenyewe na Chelsea ndiyo zinaongoza kuwa ngumu kufungika.


Katika mechi 22, Chelsea imefungwa mabao 15, Spurs imefungwa 16 na Man United ambayo sasa imecheza mechi zaidi ya sita bila ya kufungwa inaonekana imekaa vizuri maana imefungwa 21 tu.Man United imekwama namba sita, lakini uchezaji vizuri wa karata za mechi tano zijazo, unaweza kusababisha kubadilisha mambo kabisa na mwisho ikawashangaza wengi.

Hakika kwa mwendo ulivyo, ligi hiyo ni ngumu na kila kocha yuko katika wakati mgumu kwa kuwa hakuna kilicho na uhakika.

Kama Chelsea itashinda mechi mbili za mwanzo kati ya hizo tano, ni faida kubwa maradufu. Ikishindwa itatengeneza hofu.

Arsenal na Spurs zinaweza kuwa pia ni tishio kwa mwendo wa Arsenal wakati Liverpool inalazimika kujituliza maana mwendo wake umeanza kuyumba hasa hapa mwishoni.


Man City, wao wanaonekana kama wamepotea njia sahihi. Huenda wakajirudisha kwenye mstari kupitia mechi hizo tano, lakini kama watapotea. Basi watakuwa wamepoteza kwelikweli na ndiyo itakuwa ni kubahatisha kama siku moja “Mungu akipenda”, wanaweza kurejea tena Top Four.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV