February 15, 2017Zikiwa zimebakia siku chache timu ya Simba ipambane na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, benchi la ufundi la timu hiyo limetangaza kumaliza tofauti zake zilizojitokeza hivi karibuni dhidi ya nahodha wake, Jonas Mkude.


Mkude alikuwa akituhumiwa na benchi hilo la ufundi ambalo linaongozwa na Mcameroon, Joseph Omog kwa utovu wa nidhamu kutokana na vitendo vyake mbalimbali ambavyo amekuwa akivifanya klabuni hapo ikiwa ni pamoja na kugomea kucheza baadhi ya mechi.


Hali hiyo inadaiwa kuwaudhi viongozi wa benchi hilo la ufundi lakini pia baadhi ya wachezaji wa timu hiyo na kumtaka kocha wao, Omog ampokonye cheo chake cha unahodha wa klabu hiyo kutokana na kuchoshwa na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu ambavyo amekuwa akivifanya kila wakati klabuni hapo.

Hata hivyo, juzi Jumamosi kocha msaidizi wa timu hiyo, Mganda Jackson Mayanja aliliambia Championi Jumatano kuwa, hivi sasa hawana tena tofauti na mchezaji huyo na mambo yote yapo sawa.


“Mambo yote katika kikosi chetu hivi sasa yapo sawa na hatuna tofauti yoyote ile na mchezaji au kiongozi, suala la Mkude ambalo limekuwa lilizungumziwa hilo limeshapita na sasa tunachoangalia ni kuwa kitu kimoja kwa ajili ya kuhakikisha tunafanya vizuri katika mechi zetu zijazo.


“Hatukumchezesha Mkude katika mechi yetu na Prisons kwa sababu hakuwa fiti lakini katika mechi yetu na Yanga tutamchezesha kwani ni mchezaji muhimu sana kwenye kikosi chetu cha kwanza pia ni kiongozi bora na mchango wake bado unahitajika kwenye kikosi chetu,” alisema Mayanja.Hata hivyo, kuna taarifa kuwa Simba hivi sasa wamekusudia kuwa kitu kimoja na kuzuia migogoro yote ili kufanya vizuri katika mchezo dhidi ya Yanga, Februari 25, mwaka huu ambao unaweza kuamua hatima ya ubingwa.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV