February 15, 2017



Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya ni kama taratibu anaanza kulizoea benchi, baada ya kukalishwa katika mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara.
Awali, Kichuya alikuwa akianza kwenye kikosi cha kwanza cha Mcameroon, Joseph Omog huku akiwa mchezaji tegemeo.

Kichuya, mechi yake ya kwanza kuanza kukaa benchi ni dhidi ya Majimaji iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea ambayo ilimalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 3-0 kabla ya juzi kuifunga Tanzania Prisons 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kichuya aliianza ligi vyema huku katika raundi ya kwanza akiwa kinara wa mabao baada ya kufunga mabao tisa lakini amegota hapohapo, hajafunga katika mechi yoyote ya mzunguko wa pili na mara ya mwisho kuweka mpira kimiani ilikuwa ni Novemba 2, 2016 dhidi ya Stand United ambapo Simba ilishinda bao 1-0 mjini Shinyanga.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Jumatano limezipata, mfumo mpya anaoutumia kocha wa timu hiyo, ndiyo umemuondoa Kichuya kwenye kikosi cha kwanza.

Mtoa taarifa huyo alisema, kocha hivi sasa anataka soka la kushambulia kuliko kulinda goli huku akiwatumia mastraika watatu katika kushambulia ambao ni Laudit Mavugo, Ibrahim Ajibu na Juma Liuzio.

"Uwezekano wa Kichuya kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza hivi sasa ni ngumu, hiyo ni baada ya kocha kuonekana akitumia mfumo wa kushambulia zaidi kuliko kujilinda kama alivyokuwa anafanya mwanzoni.

"Hivi sasa anatumia mfumo wa kushambulia lango la wapinzani muda wote kwa kuwatumia washambuliaji watatu tofauti na awali alikuwa akitumia mfumo wa kujilinda huku akitumia mshambuliaji mmoja na viungo wengi wakabaji, hivyo kocha kampunguza kiungo mmoja ambaye ni Kichuya," alisema mtoa taarifa huyo.

Alipoulizwa Omog kuzungumzia hilo, alisema: “Kikosi chetu kina wigo mpana wa wachezaji, hivyo tunamtumia mchezaji kulingana na aina ya mechi tunayoicheza.


"Niseme kuwa, Kichuya bado ni mchezaji mzuri anayetakiwa kuwepo kwenye kikosi cha kwanza, lakini mfumo na aina ya mechi husika tunayoicheza ndiyo inasababisha aanzie nje, lakini nikuhakikishie mechi zinazofuata ataanza kikosi cha kwanza."

SOURCE: CHAMPIONI

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic