February 11, 2017

Sasa maneno yamekuwa mengi mitaani sababu eti kasi yake ya ufungaji imepungua, sasa kiungo wa Simba, Shiza Kichuya amesema atahakikisha anaongeza nguvu ya kupambana ili arejee katika ubora wake wa ufungaji.


Wiki iliyopita Simon Msuva wa Yanga alifunga bao moja katika ushindi wa Yanga wa mabao 4-0 dhidi ya Stand United na kufikisha mabao 10 na kumtoa kileleni Kichuya katika orodha ya ufungaji.


Awali Kichuya, Msuva na Amissi Tambwe wote walikuwa na mabao tisa, lakini Msuva ameongeza moja na kuwaacha wenzake katika nafasi ya pili.


Kichuya amesema kuwa: “Maneno yamekuwa mengi, ni hali tu inatokea na kujikuta hupati nafasi za kufunga ila nitaendelea kupambana ili nifunge.


“Nimepitwa bao moja tu hivyo sioni tabu ya kurejea kileleni katika ufungaji, nina uwezo wa kupambana na hata kama nikishindwa kuwa mfungaji bora natamani tuzo hiyo aichukue Msuva.


“Nataka tuzo ya ufungaji bora ibaki Tanzania na kutovuka mipaka ya nchi, hadi sasa haijajulikana nani atakuwa mfungaji bora ila naendelea kufarijika kuona Mtanzania anaongoza kwa ufungaji.“Ikitokea nikakosa ufungaji bora nitatamani kuona Msuva au Mtanzania yeyote anapata nafasi hiyo,” alisema Kichuya.

Kauli ya Kichuya kutotaka raia wa kigeni kutwaa ufungaji bora inamgusa Tambwe wa Yanga ambaye ni raia wa Burundi mwenye mabao tisa katika ligi.

1 COMMENTS:

  1. Nimeipenda sana kauli ya kizalendo ya Kichuya .......Big Up

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV