February 11, 2017



Kocha wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina amesema ili kufikia malengo yao msimu huu, hawana nafasi ya kuidharau timu yoyote, hivyo wanaenda Comoro kwa tahadhari kubwa kuhakikisha wanaibuka na ushindi utakaowaweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele.


Leo alfajiri, Yanga ilitarajiwa kusafiri kwenda Comoro kucheza na Ngaya Club De Mbe katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kupigwa kesho Jumapili.


Lwandamina amesema hawana muda wa kusubiri mchezo wa marudiano waweze kufanya vizuri, bali wanataka kuutumia mchezo huu wa kwanza kwa lengo la kujipa nafasi kubwa ya kusonga mbele.


“Soka la sasa linatakiwa uitumie nafasi yako vizuri pale unapoona inawezekana, hivyo kwa kulitambua hilo tumejiandaa vizuri kuibuka na ushindi ugenini ambao utatoa majibu mazuri kuelekea mchezo wa marudiano.


“Katika soka hakuna ushindi muhimu na usiyo muhimu, hivyo ushindi wowote kwetu ni muhimu iwe nyumbani au ugenini, siwezi kuwazungumzia sana wapinzani wetu, lakini ninachoweza kusema ni kwamba tunaenda kusaka matokeo mazuri na hatuwadharau,” alisema Lwandamina.


MAANDALIZI BOMBA
 “Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunashinda mechi hii, tumefanya maandalizi kulingana na taarifa tulizozipata kuhusiana na aina ya soka ambalo wapinzani wetu hao wacheza.


“Tumeambiwa wanacheza soka la nguvu na wana wachezaji wawili wa kimataifa kutoka Ivory Coast ambao ndiyo wanawategemea zaidi hivyo na sisi tumejipanga kukabiliana na aina hiyo ya soka lao,” alisema Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi.


KOCHA NGAYA APIGA AKOMAA
Kocha wa Ngaya Club, Lucien Sylla Mchangama mwenye leseni C ya ukocha ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf), alisema hana wasiwasi na mchezo huo dhidi ya Yanga licha ya wapinzani wao kuonekana ni timu kubwa.
“Yanga ina uzoefu mkubwa katika michuano hii, hiyo si sababu ya kutufunga kirahisi, tutahakikisha tunashinda nyumbani,” alisema Mchangama.


REKODI YA YANGA COMORO
Yanga ina rekodi nzuri na timu za Comoro, kwani mwaka 2009 ilicheza na Etoile d’or de Mirontsy na kuifunga jumla ya mabao 14-1 (8-1 na 6-0), mwaka 2014 ikaitoa Komorozine kwa mabao 12-2 (7-0 na 5-2). Jumla Yanga ilifunga mabao 26 na kufungwa matatu.


KURUDIANA WIKI IJAYO

Baada ya mechi hiyo ya kesho Jumapili, Yanga itarudiana na Ngaya Club kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Jumamosi ijayo ya Februari 18, mwaka huu. Endapo Yanga itafanikiwa kuiondosha Ngaya, basi itakutana na mshindi kati ya Zanaco ya Zambia au APR ya Rwanda.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic