BURHANI (MWENYE JEZI NYEUSI) WAKATI AKIWA NA KIKOSI CHA MAJIMAJI YA SONGEA |
Mwili wa Kipa wa Kagera Sugar, David Burhani ambaye alifariki dunia juzi Jumatatu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, unatarajiwa kuzikwa leo huko nyumbani kwao mkoani Iringa.
Jana Jumanne, mamia ya wapenzi wa soka wa jijini Mwanza pamoja na wale wa Kagera wakiongozwa na wachezaji pamoja na viongozi timu ya Kagera Sugar, walijitokeza kwa wingi hospitalini hapo kwa ajili ya kuuaga mwili huo kabla ya kusafirishwa kwa basi kwenda mkoani Iringa.
Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema kuwa kifo cha Burhani ni pigo kubwa kwa timu hiyo lakini pia kwa soka la Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa enzi za uhai wake.
“Leo saa tano (jana) ndiyo tumeuaga mwili wake hapa Bugando tayari kwa kusafirishwa kwenda kwao mkoani Iringa kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika kesho (leo) baada ya kufika kwani utasafirishwa kwa basi.
“Hakika kifo chake ni pigo kubwa kwetu lakini pia katika soka la Tanzania, hivyo tutamkumbuka kwa mema mengi aliyoyafanya enzi za uhai wake, tumuombee kwa Mungu aweze kuipumzisha roho yake mahali pema peponi,” alisema Maxime.
Burhani kabla ya kukumbwa na mauti akiwa na kikosi cha Kagera Sugar, pia aliwahi kuitumika Mbeya City kwa mafanikio makubwa kwani ndiye kipa aliyechangia kwa kiwango kikubwa kuiwezesha kutinga Ligi Kuu Bara kutoka Ligi Daraja la Kwanza, lakini pia aliitumikia Majimaji ya Songea .
0 COMMENTS:
Post a Comment