February 10, 2017





Na Saleh Ally
MSIMU uliopita, Leicester City ilikamilisha mechi zake 38 ikiwa na pointi 81, hivyo kutwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi 10 dhidi ya Arsenal iliyobaki na 71.


Arsenal ilipewa nafasi kubwa ya kubeba ubingwa kwa kuwa vigogo wengine kama Chelsea waliokuwa mabingwa watetezi, Manchester United, Manchester City hawakuwa na mwendo mzuri.


Lakini mwisho, Leicester wakautumia vizuri udhaifu wa “kuugua mwishoni” wa Arsenal na kubeba ubingwa kwa tofauti hiyo kubwa kabisa.


Msimu huu baada ya mechi 24 Leicester iko katika nafasi ya 16 na tayari hofu kwa mashabiki wake imetanda kwamba wanaweza kuteremka daraja.


Kumbuka asilimia 90, soka ni mahesabu, ukiangalia takwimu zinaibana Leicester kwa asilimia nyingi zaidi kwa kuwa ukiachana na msimamo kuwa katika nafasi ya 16 katika timu 20, misimamo mingine pia iko hoi.



Msimamo wa nyumbani, Chelsea imekusanya pointi 33 kwa maana imeshinda mechi nyingi nyumbani. Tottenham inafuatia kwa kuwa na pointi 32, Man City pointi 28 na Leicester iko katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 18.


Msimamo wa ugenini, Leicester inashika nafasi ya pili kwa kuboronga kwa kuwa ina pointi tatu tu za ugenini na Burnley inashika mkia kwa kuwa na moja tu ya ugenini.


Kwa maana ya ubutu wa ushambulizi, iko katika nafasi ya 16 na ulinzi iko katika nafasi ya 14. Hauwezi kuamini kama hawa ni mabingwa wa msimu uliopita!


Msimu uliopita ilishinda mechi 23 na kubeba ubingwa. Msimu huu hadi sasa imeshinda mechi tano tu na kati ya hizo zote ni nyumbani. Sare tatu ni ugenini kama ilivyo nyumbani. Imepoteza nyumbani mara nne na kufungwa ugenini mara 9. Dalili za kuteremka zimeiganda na wahusika lazima wabadili gia angani, la sivyo, mchuma utaanguka pwaaaa.




Wakati Leicester inapambana kutoingia kwenye aibu ya kuteremka daraja, timu tatu za Sunderland, Crystal Palace na Hull City zimeishaingia kwenye mstari mwekundu.


Lakini wengine Swansea City nao wako katika nafasi ya 17, moja tu kabla ya kuingia kwenye shimo hilo la hatari kurejea daraja la kwanza.


Kitu kibaya zaidi ni kwamba hakuna tofauti kubwa kati ya walio mkiani na wanaotaka kukwepa kuingia shimoni.


Mfano, Sunderland katika nafasi ya 20 na Palace katika nafasi ya 19 kila moja ina pointi 19. Hull City ina pointi 20 katika nafasi ya 18 lakini zinazofuatia Leicester, Bornemouth na Middlesbrough kila moja ina pointi 21.


Mfano, Middlesbrough katika nafasi ya 15 ikipoteza mechi ijayo, Sunderland akashinda, basi anachukua nafasi yake. Hivyo kazi ya mkiani, si ya mchezo.


Hadi sasa si rahisi kusema timu fulani imeteremka daraja lakini inawezekana kabisa ukazitaja timu sita au saba kuwa ziko kwenye hatari.


Kwa Leiceter City wasiposhinda mechi mbili zijazo, kuna uhakika wa wao kuwa mkiani bila ya ubishi. Hivyo si kazi kwa kuwa wao wanaweza kuwa tofauti na wengine kutokana na ukubwa wa presha.



                        TAKWIMU
                        W       D        L     Jumla
Nyumbani          5        3        4       12 
  Ugenini            0       3        9       12 
  JUMLA             5       6       13      24



                                    Nyumbani   Ugenini      Jumla 
Mabao/kufunga                  16                  8          24
Mabao/kufungwa               16                  25         41



Mechi walizocheza                    24
Wamesawazisha mabao               6
Wamenza kufunga mabao            5
Wapinzani wameanza kufunga    19



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic