Unaweza kusema ni kiroho safi Mtibwa Sugar imesema kipigo cha mabao 5-0 walichopata kutoka kwa Mbao FC juzi Alhamisi kwenye Ligi Kuu Bara ni haki yao na wala hakuna wa kumtupia lawama.
Ikicheza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mtibwa ilikubali kipigo hicho kutoka kwa Mbao ambayo imepanda msimu huu kucheza ligi kuu. Hicho ni kipigo cha pili kwa Mtibwa kutoka timu za Kanda ya Ziwa kwani mwanzoni mwa wiki hii, walifungwa mabao 2-0 na Kagera Sugar.
Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru, ameliambia Championi Jumamosi kuwa: “Ama kweli kipigo tulichokipata kutoka kwa Mbao ni halali yetu, hatuwezi kumlaumu mtu yeyote wa nje, waamuzi wamefanya kazi yao ipasavyo, wanahitaji pongezi.
“Tumekumbana na dhoruba kali sana, Mbao walistahili ushindi kwa sababu hatujacheza kwa kiwango chetu kile cha kawaida, lakini kipigo hicho kimetufanya tujipange kikamilifu kwa ajili ya mchezo wetu ujao dhidi ya African Lyon, tunawaahidi mashabiki wa Mtibwa hatutarudia makosa.”
Baada ya kipigo hicho, Mtibwa imebaki katika nafasi ya tano na pointi zake 31 katika mechi 21 ilizocheza ikiwa imefunga mabao 23 na kufungwa 26.
0 COMMENTS:
Post a Comment