February 9, 2017




Mshambuliaji wa zamani wa timu ya Liverpool, Joho Barnes anatarajiwa kutua nchini Machizi mwaka huu kwa ajili ya kuendesha kliniki ya soka kwa vijana wa timu ya taifa ya vijana walio chini ya miaka 17, 'Serengeti Boys'


Sambamba na hilo, Barnes pia atahudhuria awamu ya pili ya mashindano maalum ya kombe la Standard Chartered ambayo yatashirikisha timu tatu kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.



Mtendaji mkuu wa benki ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani alisema ujio wa Barnes unalenga kuimarisha vipaji vya soka kwa vijana wa Kitanzania.


"Tutahakikisha John Barnes anatumia ujuzi kadri atakavyoweza ili aweze kuvinufaisha vipaji vya hapa. Na sisi kama wadhamini wa timu ya Liverpool, na iwapo kama ataridhishwa na kuvutiwa na vipaji vya baadhi ya wachezaji, tutaangalia namna ya kuhakikisha vipaji hivyo vinapata nafasi ya kujiunga na timu za vijana ya Liverpool," alisema Rughani.


Kuhusu mashindano hayo ya kombe la Standard Chartered, Rughani alisema kuwa awamu ya kwanza itashirikisha timu 32 ambazo zitacheza kwa mtindo wa mtoano ili kupata timu itakayoiwakilisha Tanzania.


Mshindi wa mashindano awamu ya pili, wachezaji wake watapata fursa ya kwenda kufanya ziara kwenye timu ya Liverpool ambapo gharama zote zitakuwa chini ya benki hiyo.


Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi aliipongeza benki hiyo kwa kuunga mkono harakati za kukuza michezo nchini.


"Mchezo kama mpira wa miguu, unasaidia kutengeneza fursa kwa vijana na pia inaweza kuimarisha uchumi wa nchi. Nawaahidi kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika juhudi zenu," alisema Malinzi.


Naye katibu mkuu wa shirikisho la soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa aliishukuru Standard Chartered huku akiiomba sapoti zaidi ya kukuza soka la Tanzania.


"Kwa sasa timu yetu ya vijana imefanya vizuri na kufanikiwa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana wenye miaka chini ya 17, zitakazofanyika Gabon. Tunaamini mtasaidia kuiunga mkono ili iweze kufanya vizuri zaidi na kufika kwenye fainali za dunia," alisema Mwesigwa.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic