March 10, 2017




Na Saleh Ally
LIGI Kuu Bara inakwenda ukingoni na Simba ndiyo vinara wakiwa na pointi 55. Yanga wanafuatia katika nafasi ya pili wakiwa na pointi 53.

Ukingoni utagundua mambo yanabadilika kabisa ukilinganisha na mwanzoni ambako asilimia 90 ya timu zinakuwa na malengo yanayofanana na si zaidi ya kutwaa ubingwa.

Ligi inapofikia ukingoni, kunakuwa na makundi matatu ambayo lazima yanaundwa hata bila ya timu kupenda, lakini kila moja kutokana na ushiriki wake inakuta imetumbukia katika kundi fulani.

Kundi la kwanza ni timu zinazopambana kuepuka kuteremka daraja. Hizi ni zile zilizo mkiani au kundi la chini kabisa kwenye msimamo.

Kundi la pili ni zile zilizo katikati ya msimamo wa ligi. Hizi baadhi zikizubaa zinatumbukia kwenye kundi la kwanza lakini zinachofanya ni kupambana kuendelea kubaki. Hapa hakuna kushuka au kubeba ubingwa.

Ukienda katika kundi la tatu ni lile ambalo mara nyingi linakuwa na timu chache. Mara nyingi ni mbili, tatu hadi nne. Hizi zinakuwa ni zile vinara na ndiyo zinazokuwa zinawania ubingwa.

Katika Ligi Kuu Bara, ni timu mbili ndiyo zenye nafasi kubwa ya kubeba ubingwa. Vinara Simba na Yanga ambao ni mabingwa watetezi. Kumbuka makundi yote, hakuna upande ambao hautahitaji pointi tatu na kwa kuwa ni ligi, kila upande utakutana na mwingine.

Zinapokutana, kila mtu anacheza kulingana na malengo yake. Kila upande utakuwa unataka pointi tatu lakini kwa ajili ya malengo yake.

Kipindi hiki kimekuwa kikielezwa ndicho ambacho kuna mchezo mchafu wa rushwa kwa timu zinazotaka kujiokoa, pia zile zinazowania kubeba ubingwa.

Taarifa za miaka nenda rudi zimeeleza kuhusiana na namna ambavyo timu zilizo katikati ya msimamo na zisizo na hofu ya kuteremka, zinavyotumika kufanya biashara haramu.

Kuhusiana na rushwa, nimekumbusha mara kadhaa kwamba ni dhambi ya ngono. Vigumu kusema fulani katenda hadi awekewe mtego na kibaya zaidi, lazima kuwe na mmoja aliye tayari kusema kati ya mtoaji na mpokeaji.

Kama hawa wawili, mtoaji na mpokeaji watakuwa na siri moja, inakuwa vigumu sana kuweza kupambana kwa ufasaha na mdudu huyo rushwa.

Wachezaji kadhaa wa zamani, wamekuwa wakielezwa namna mambo yanavyokuwa kinapofikia kipindi kama hicho, maana makundi hayo matatu kila upande unakuwa unafaidika kivyake.

Wachezaji wengi mnajua kama kuna rushwa, sitazungumza na majina yenu. Ninazungumza na nafsi zenu ambazo haziwezi kufanya ukweli ukawa uongo kwa kuwa ni zilizo sahihi.

Ninazungumza na waamuzi pia. Mnajua kwamba mmekuwa mkitumika na katika karibu kila mechi kumekuwa na madudu.

Kuna rafiki yangu mmoja ambaye ni mwamuzi mstaafu aliwahi kuniambia namna kila timu inavyotoa fedha ikiwa ni sehemu ya hongo na hukabidhiwa kwa watu wa karibu na wao hufanya kazi.

Kila mtu kazini kwake na waamuzi wanajua wafanye nini. Naomba msiseme nawadhalilisha, lakini nataka kuwakumbusha baadhi yenu walio wachafu kwamba ni vizuri wakaepuka tamaa ya fedha na kuacha mpira wenyewe uamue.

Kwa wachezaji pia kumbukeni nyie baadhi mnaofaidika kwa kupata fedha. Basi kumbukeni hamko “fair” kwa kuwa mnawaangusha wenzenu kwa faida zenu binafsi na si timu. Onyesheni mabadiliko na mjue mnatakiwa kutenda haki zaidi kuliko kufanya mazoezi au maandalizi pamoja halafu mwisho nyie mnageuka na kufanya mambo yasiyo sahihi.

Kama kweli mnataka kulimaliza tatizo hilo ili apatikane bingwa halali ambaye atakuwa na nguvu sahihi kupambana kimataifa, basi wadau kataeni rushwa ili kuepuka kufanya mambo ya kuungaunga.

Bingwa akipatikana kwa matokeo ya soka, timu nyingine zikashika nafasi fulani kwa mpira wa halali, basi utakuwa ni ushindani halali unaotokana na ligi halali na bora na itaongeza mafanikio na ubora wa mchezo wa soka nchini kwetu. Chonde.
SOURCE: CHAMPIONI



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic