March 18, 2017Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI Mtanzania, Mbwana Samatta ameweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza michuano ya Europa League hatua ya robo fainali.

Hatua hiyo, utaiona hata timu kama Manchester United, zilikuwa zikipambana kuhakikisha zinafikia hapo zikitumia juhudi kuu kutoka kwa wachezaji nyota kama Zlatan Ibrahimovic, Juan Mata na nyota wake wengine wakiongozwa na kocha maarufu, Jose Mourinho.

Kama haitoshi, timu kongwe za Ulaya kama Ajax ya Uholanzi na Anderlecht ya Ubelgiji zimepata nafasi hiyo ya kuingia katika robo fainali. Nyingine ni Lyon ya Ufaransa, Besiktas ya Uturuki, Schalke 04 ya Ujerumani, Celta Vigo ya Hispania na KRC Genk ya Ubelgiji ambayo anaitumikia Samatta.

Safari hii kwa Tanzania ndiyo kipindi upangaji wa ratiba za robo fainali ya Europa League imefuatiliwa kuliko wakati mwingine wowote.

Wengi walikuwa na hamu au hofu kama Genk ingepangwa na Manchester United, mambo yatakuwaje? Samatta atatua pale Old Trafford na kumvuruga Mourinho?

Wapo waliofurahia kuona Samatta na Genk wameikwepa Genk na wako waliotamani wangepangwa nayo tu.

Mwisho, Genk imeangukia kwa Celta Vigo, timu ambayo wameona kuwa ni nafuu kuliko ingepangwa na Manchester United. Unaweza kusema ni dakika 180 sawa na pochi kwa Samatta, akizichangamkia na kufanya vizuri basi ni bonge la tangazo na nafasi nzuri kwake “kutusua” zaidi.

Celta Vigo si timu ya mchezo, si rahisi kama wengi wanavyoona na huenda ni mtihani mgumu kwa Genk na Samatta mwenyewe ingawa wamewahi kukutana na timu ya Hispania katika michuano hiyo.

Celta Vigo si timu yenye mwenendo ulionyooka na huenda hili likawa shida kuu kwa Samatta na Genk. Kwamba hawaaminiki na mwendo wao haueleweki kwa kuwa wanaweza kuwa vizuri mfululizo au wakaboronga mfululizo.

Kikubwa au kibaya kwa Celta Vigo kwenda Genk, timu hiyo ya Hispania haina kawaida ya kuwa na hofu na kila mechi ngumu ndiyo inakuwa bora zaidi.

Inaweza kuwa faida kwa Genk kama Celta Vigo wataona mechi dhidi ya Genk si ngumu kwao. Lakini kama wakiamini wanacheza na timu ngumu kama Real Madrid au Barcelona, ubora wao hupanda maradufu na kama wakiona Genk ni hatari kwao, hata wao Genk wawe makini sana kwa kuwa safu ya ushambulizi ya Celta Vigo iko vizuri katika upachikaji mabao.

Ukiangalia katika msimamo wa La Liga, Celta Vigo iko katika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 35. Ina mabao 39 ya kufunga ikiwa inawazidi Alaves walio katika nafasi ya 10 wenye 28, pia wanawazidi Athletic Bilbao katika nafasi ya 7 wenye mabao 34.

Rekodi zao za nyuma hasa katika La Liga inaonyesha ni timu isiyo na mwendo ulionyooka lakini wakiwa vizuri na ukakosea, basi unaona mvua ya mabao.

Oktoba 2, mwaka jana waliitwanga Barcelona 4-3 katika La Liga lakini wakakwama kwa kuchapwa mabao 2-1 na Real Madrid, hii ilikuwa Agosti 27, mwaka jana, mwanzoni kabisa mwa La Liga msimu wa 2016-17.

Deportivo La Coruna ambao juzi wameifunga Barcelona, wao waliitwanga mabao 4-0. Pia waliitwanga Sevilla kwa mabao 3-0 hali kadhalika Malaga wakaitundika mabao 3-1.

Utagundua, Celta Vigo ni timu inayokomaa sana na timu kubwa au mechi inazoziona ngumu. Kuna mechi zinazoonyesha udhaifu mkubwa wa safu yake ya ulinzi.

Kuna mechi ambayo Celta Vigo imeonyesha ni “utelezi” katika safu ya ulinzi hasa siku wakikosea. Mfano mechi dhidi ya Atletico Madrid walichapwa mabao 4-0, Villarreal wakawachapa 5-0, Sevilla wakawanyoosha 3-0.

Genk inaingia ikiwa na ‘confidence’ ya kuwachapa Gent kwa mabao 5-2 katika mechi moja. Wanaanzia ugenini kwa mara nyingine.

Samatta na wenzake wa Genk wanaweza kusonga mbele kama wataenda na mfumo walioanza nao katika hatua ya 16 Bora ya Europa League ambayo walianza na ushindi ugenini.

Ushindi wa mabao mengi, maana walishinda 5-2 dhidi ya Gent huku Samatta akipachika mawili. Mechi ya pili ikawa 1-1 na kutengeneza jumla ya 6-3.

Hivyo kama watashinda ugenini dhidi ya Celta Vigo, wakajiimarisha vizuri nyumbani basi wanaweza kuwa na nafasi kwa kuwa Celta Vigo ni timu isiyokata tamaa na mapambano.

Samatta ni nafasi nzuri kwake, kama atafanikiwa kucheza vizuri katika mechi hizo mbili ambazo ni dakika 180, pamoja na kusaidia kuivusha Genk, litakuwa ni soko maradufu kwake.

Tayari ameanza kuwa gumzo, bado ana nafasi ya kuwa gumzo zaidi na dakika 180 zitakuwa ni lulu na bonge la pochi kwake ambalo anapaswa kuondoka nalo ili kutengeneza nafasi nzuri ya maisha mbele.

Nafasi ya Genk haiko wazi, nafasi ya Samatta kung’ara si rahisi lakini Genk inaweza kufanya jambo na Samatta ana uwezo wa kufanikisha anachotaka na kikubwa ni maandalizi na kuelekeza hisia kwenye kutaka kutimiza malengo.

NANI ANACHEZA NA NANI? 
Anderlecht Vs Man United
Celta Vigo Vs Genk
Ajax Vs Schalke 04

Lyon Vs Besiktas

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV