Na Saleh Ally
WAKATI katika soka la England gumzo kubwa ni mechi ya wikiendi pale Arsenal itakapoivaa Liverpool, hapa nyumbani kuna tofauti kubwa.
Gumzo kubwa katika soka ni wachezaji wawili wa kimataifa wa Yanga, Donald Ngoma raia wa Zimbabwe na beki, Vincent Bossou kutoka Togo wakiwa katika mzozo na uongozi klabu hiyo.
Bossou amekuwa akiandika mitandaoni kwamba anadai mshahara wa miezi minne na kumekuwa na taarifa kuwa amesusa kucheza.
Tayari uongozi umelifafanua hilo kwamba anadai mshahara wa miezi miwili na alichelewa kulipwa baada ya kwenda Afcon.
Mechi ya juzi dhidi ya Ruvu Shooting alirejea uwanjani na kucheza. Swali langu likabaki hivi je, kama akishalipwa, zile siku ambazo hakuitumikia Yanga atakatwa? Je, ataweza kuilipa Yanga ambayo ilimhitaji na hakuwepo kwa makusudi?
Lakini nikashangazwa zaidi kumuona Bossou akibishana na mashabiki mtandaoni huku akiwatukana. Nikajiuliza ni sahihi kumuita mchezaji wa kimataifa kwa kukusudia atakuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa hapa nyumbani?
Jibu langu na ninachoamini, Bossou hawezi kuwa kipimo bora cha mfano bora. Pia si mchezaji wa kiwango cha juu sana na unaweza kusema asipokuwepo, basi Yanga itasumbuka sana. Hivyo anapaswa kujipima, kubadilika na kuachana na nyodo zisizoendana hata na kiwango chake.
Kwa upande wa Ngoma, hakika amenishangaza sana hadi nilifikia kuhoji kwamba Yanga hii, inaweza kuchezewa na mtu kama Ngoma ambaye hofu ya wazi ilionekana. Niliwahi kuwaambia wafanyakazi wenzangu ofisini kuwa Ngoma hakuwa mgonjwa kama alivyokuwa akisema.
Mimi ni binadamu, kuwa na hofu na jambo hakuna anayeweza kunizuia. Ilionekana wazi kuna jambo analoshinikiza, labda hasira za kuzuiwa kuondoka au kutaka kuongezewa mkataba wenye maslahi zaidi kama ilivyoelezwa.
Kuna vyombo vya habari viliripoti amegoma, Gazeti la Championi Jumatano iliyopita likaripoti amekabidhiwa mwanamke ambaye anampa mazoezi kuhakikisha anarejea uwanjani. Akaingia mitandaoni na kutushambulia, nikawashauri wenzangu kuachana na mwendawazimu ili kuepuka kuonekana tunafanana naye kwa kuwa hakuna tulichokuwa tumekosea, maana picha za mnato na video zipo, mwanamke huyo akisimamia mazoezi yake.
Siku chache zimepita, amemshambulia daktari aitwaye Haroun Haroun kwamba alitumia fedha za Yanga, hakumtibu na alimtapeli. Lakini pia akawashambulia viongozi wa Yanga kuwa hawana weledi.
Huo ni uhuru wa Ngoma, kweli anaweza kuzungumza lolote. Yeye ni mwandishi anajua utaratibu wa uandishi? Kweli Ngoma anaweza kuwa ndiye mtu maarufu zaidi kuhojiwa na gazeti hadi aone ni anayejulikana sana, hivyo ni kama mtu anayeonewa sana. Ni upuuzi mtupu.
Kuonyesha dharau zaidi akaandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa hamuogopi yeyote zaidi ya Yusuf Manji anayemlipa mshahara, upuuzi.
Anajua uandishi, anajua udaktari, anajua uongozi bora. Vipi hawi mtu makini wa kazi yake na badala ya kumaliza mambo kama mwanaume, anaonyesha tabia za kipuuzi kwa kususa mambo?
Daktari Haroun naye amefafanua mambo, ameeleza namna ambavyo Ngoma alikuwa na nafasi ya kucheza lakini hakufanya hivyo huku akisisitiza kwamba aliacha kucheza makusudi na alimkasirikia daktari huyo baada ya kuwaeleza viongozi kwamba alikuwa tayari kucheza.
Ngoma anataka kuiibia Yanga, anataka alipwe mshahara huku hachezi! Nini kilimleta Tanzania? Nani anataka kuona anavyotembea au sura yake? Arudi kwao na kuacha nafasi hiyo kwa Watanzania au wachezaji wa kulipwa wenye nafasi ya kuleta changamoto.
Kweli ni mchezaji mzuri lakini watu wanapaswa kuvumilia dharau na majivuno kwa kigezo hicho pekee?
Ananikumbusha ule msemo wa “Mjinga mpe kilemba, utamwona mwendowe”.
Anayepata cheo au umaarufu, hujisahau na kuanza kuonyesha dharau kwa wenzake au wanaomuongoza.
Najiuliza anashindwa vipi kujipima kuwa Yanga ndiyo iliyomtangaza zaidi kwa kuwa sasa hana nafasi hata kwenye timu ya taifa. Ubora wake anaupima katika kipi, eti “Ngoma msumbufu”. Amewahi kuongoza kwa mabao ya kufunga? Kama anaringa hivyo, Amissi Tambwe aseme vipi? Kafanya makubwa zaidi yake na nidhamu yake iko juu. Vipi Thabani Kamusoko haisumbui au hana nyodo kama yeye?
Matukio lukuki kama kupigana kambini, kubeza wenzake amehusishwa nayo. Uongozi wa Yanga unaonekana kutokuwa na meno, viongozi waoga, kuhofia “kuwaudhi” mashabiki eti kwa kuwa Ngoma ni kipenzi chao. Hii si sawa hata kidogo.
Lazima uongozi ujue, kuendelea kumtukuza Ngoma ni kuwavunja wengi mioyo yao na mwisho madhara yake yatakuwa makubwa na wataanza kumtafuta mchawi wakiwa wamechelewa.
Hauwezi kuwa na waajiriwa, wengine wafuate utaratibu na mwingine awe juu ya utaratibu. Jiulize, kama Zlatan Ibrahimovic anafuata utaratibu Manchester United, Lionel Messi anafuata kule Barcelona na Cristiano Ronaldo anaheshimu pale Madrid. Huyu Ngoma ni nani awe juu ya heshima na utaratibu wa Yanga tena akionekana badala ya kucheza soka ni bora kwenda kwenye mitandao na kupambana na maneno kama mwanamuziki wa taarabu.
Yanga kama uongozi wanaweza wakakubali kwa uoga wa kuzongwa na mashabiki. Mimi kama mdau wa soka, napinga upuuzi huu na kuweka msisitizo, nidhamu haina mmoja.
Kuna ule msemo wa Kiswahili, “Njaa ya leo ni shibe ya kesho.” Watanzania tuamke, tusidharauliwe hadi itie kinyaa. Ngoma afanye kazi yake akifuata utaratibu, kama hawezi, anaweza kusafiri na dharau zake nje ya Tanzania na kuziendeleza huko ili atupe nafasi tuwape somo jema vijana wetu wanaochipukia kwa kuwa alikuja akaikuta Yanga.
Sina cha kuongeza. Ngoma amepoteza sifa muhimu kabisa na ya kwanza kwa mchezaji yeyote yule duniani, NIDHAMU.
ReplyDeleteHuu ni ujinga na tabia ya kusujidia wachezaji inaboa hivi Busungu akipewa nafasi anashindwa kuwa zaidi ya ngoma au Martin tujiamini nakumbuka sana Tarimba alimkata Lunyamila na Kizota wakati watu wakiwataka maana walishajiona ni zaidi ya timu. Wamuuze Simba au Azam maana wote wanamtaka.
ReplyDeleteHuu ni ujinga na tabia ya kusujidia wachezaji inaboa hivi Busungu akipewa nafasi anashindwa kuwa zaidi ya ngoma au Martin tujiamini nakumbuka sana Tarimba alimkata Lunyamila na Kizota wakati watu wakiwataka maana walishajiona ni zaidi ya timu. Wamuuze Simba au Azam maana wote wanamtaka.
ReplyDeleteWewe mwandishi ni kimeo tu unajitahidi kupamba habari zako ili uwe na soko ila huna point za kisoka.
ReplyDeleteWewe Gilbert point zako za kisoka ni zipi! mbona husemi unaishia tu kumlaumu mwandishi?
DeleteTuambie nawazo yako ni yapi? Kama huna cha kusema ni afadhali usiandike usitutoe kwenye somo.