Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, ametamka kuwa kufungwa na watani wao Simba siyo sababu ya wao kukata tamaa ya kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na badala yake ameingia vitani kupambania taji lao.
Timu hizo, zilivaana wikiendi hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Yanga ilifungwa mabao 2-1.
Pluijm amesema wao kitu kikubwa walichokipoteza ni kushindwa kushinda mechi ya ‘derby’ pekee lakini siyo ubingwa.
Pluijm alisema timu yao bado ina nafasi ya kushinda kwenye mechi zijazo za ligi kuu na hilo linawezekana, kwani tayari amekutana na wachezaji wao kwa ajili ya kuwatengeneza kisaikolojia pekee.
Aliongeza kuwa, hivi sasa ameingia vitani kwa kushirikiana na benchi la ufundi la timu hiyo kuhakikisha wanautetea ubingwa wao kwa kushinda mechi zote nane walizozibakiza.
“Kiukweli kabisa nimekosa furaha moyoni mwangu ni baada ya kufungwa mechi ya derby na wapinzani wetu Simba na nimeshindwa kuelewa kilichotokea uwanjani wakati mechi inaendelea.
“Lakini nimeirudisha furaha yangu kwa kuungana pamoja kwa kuanzia wachezaji na benchi la ufundi kwenye mechi hizi zilizobaki kuhakikisha tunashinda na tunaubakisha ubingwa wetu Yanga, licha ya Simba kuongoza,” alisema Pluijm.
0 COMMENTS:
Post a Comment