April 3, 2017



Na Saleh Ally
JESSE Lingard amecheza Manchester United kwa miezi 18 tu, siku chache zilizopita amefanikiwa kununua gari aina ya Bentley Continental GT lenye thamani ya pauni 200,000 (zaidi ya Sh milioni 545.2).


Lingard ni kati ya watu waliokutana na maneno makali ya wakongwe wa Manchester United, Rio Ferdinand na Paul Scholes ambao walionyesha kuchukizwa na Lingard na Paul Pogba ambao kila wakifunga bao walikuwa wakitumia mtindo wa “dabbing” kusherehekea mabao wanayofunga.

Kufurahia si jambo baya, lakini Scholes aliona furaha imekuwa kubwa kupindukia kwa kuwa timu iko katika nafasi ya sita na imeendelea kubaki hapo tangu Septemba 2016. Imekuwa ikichukua nafasi ya 8 au 7 kabla ya kukwama 6!


Scholes alitaka “Celebration with concentration”. Watu wanaoshangilia lakini wanaonyesha bado kuna jambo wanataka na halijakamilika. Mfano unapoona mchezaji anafunga bao, haraka anakimbilia mpira wavuni na kuuwahisha katikati, maana yake anataka kufunga tena katika mchezo huo.



Hapa nyumbani, Simba imekosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo, ninaamini asilimia 99 ya wachezaji waliopo sasa hawajui utamu wa ubingwa hasa kupitia Simba.


Simba imekuwa haina mafanikio kwa kipindi chote hicho, zaidi imekuwa ikiangukia namba tatu au hata nne, jambo ambalo halikuwa limewahi kutokea ukiacha ule mwaka ilipotaka kuteremka daraja.


Wakati kina Scholes na Ferdinand wakiwakataza wachezaji wa timu yao ya zamani kuachana na kushangilia kupindukia wakati timu ikiendelea kufanya vizuri, hapa nyumbani wako wanaoamini wachezaji wao kupiga chenga nyingi ni jambo zuri na linapaswa kupongezwa kwa kuwa wanatoa burudani sana.

Msemaji wa Simba, Haji Manara aliandika mitandaoni akimsifia Ibrahim Ajibu ni mmoja wa waburudishaji bora na wanaoweza kuwa zaidi yake ni Diamond na Ali Kiba pekee ambao ni wanamuziki. Baada ya hapo, anafuatia yeye akiwa mburudishaji bora namba tatu.


Manara anaweza akawa anazungumza kwa utani lakini kauli yake kama kiongozi lazima inachukuliwa kwa uzito wa juu hasa kwa kuwa anamzungumzia mchezaji ambaye tunaamini ni kijana na mtaji wa taifa hapo baadaye kama akiwa makini.



Ajibu anapaswa kuwa mburudishaji au mwanasoka anayepiga hatua? Unaona anasonga na kwa anavyocheza ni anayesonga na baadaye atafanikiwa?


Itakuwa vigumu kwake kununua gari la Sh milioni 500 kama Lingard ndani ya miezi 18. Tujiulize kafanya nini ndani ya misimu mitatu, kweli amepiga hatua kimafanikio? Kajenga, ana kiwanja, ana usafiri?

Kama anayo hayo ni mtu anayeonekana ataondoka Simba? Anataka kucheza nje ya Tanzania, mfano alivyoenda Misri? Kama anataka kwenda amebadilika? Anapenda kuwa mburudishaji tu au anataka kupiga hatua?


Natofautiana na Manara kwenye kitu kimoja, naona kuendelea kumsifia Ajibu mitandaoni ni kuendelea kumbakiza hapa Tanzania akiwa mburudishaji wa Uwanja wa Taifa na viwanja vingine vya Ligi Kuu Bara.




Kama unakumbuka, Mbwana Samata hakuwahi kuwa mburudishaji, alikuwa akicheza mpira wa malengo anayetaka kufanya jambo kwa ajili ya kusaidia timu na si kuburudisha watu kwa kuruka na mpira, kupiga vyenga na mbwembwe za kulitemesha “chips” jukwaa.


Thomas Ulimwengu, ukimuangalia vizuri inaonekana hata kutuliza si kwa uhakika sana. Anachotaka ni ushindi na anayesonga mbele. Leo naye yuko Ulaya tena baada ya kucheza timu ambayo ni mabingwa Afrika, TP Mazembe na akiwa tegemeo.


Tanzania iliwahi kuwa na wanaoweza kuburudisha wakiwa na malengo kama Sunday Manara. Sasa unajiuliza msaada wa Ajibu kwa Simba wakati akiburudisha ni nini kama kwa misimu yote timu yake haijapata makombe naye anaendelea kuburudisha?

Msimu wa 2014-15, Ajibu alifunga mabao nane, 2015-16 akafunga tisa, msimu huu wa 2016-17 amefikisha sita. Je, takwimu hizi zinatosha yeye kusifiwa ni mburudishaji?

Je, msaada wake Simba ni upi? Uchezaji wake bado ni ule wa anapoamua kucheza na siku nyingine akiwa hana “mood” inabidi kumsubiri siku nyingine!

Ushauri wangu kwa viongozi na hata wachezaji wakongwe wa klabu hizi kongwe wasimame imara na kuwakumbusha wachezaji wao kwamba mafanikio ndiyo burudani namba moja.

Mashabiki wa Simba sasa hawataki chenga, kanzu au kukimbia tu bila ya malengo. Wanachotaka ni kombe na ikiwezekana kucheza michuano ya kimataifa ambako kitakuwa kipimo sahihi cha burudani.


Kuanza kumsifia Ajibu anaburudisha leo ni kuzidi kumjaza maneno yatakayomsahaulisha akiamini hakuna tena kama yeye kumbe hajafika popote na asipoangalia ataishia hapo kabla ya kufika popote.

Kuwapa moyo wachezaji ni jambo zuri, lakini vizuri kuchagua maneno sahihi kuliko kwa viongozi kutanguliza ushabiki ambao unaweza ukawafanya kweli wakabaki kuwa waburudishaji badala ya wanasoka wenye malengo.

SOURCE: CHAMPIONI


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic