April 14, 2017Na Saleh Ally
MECHI ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Jumatatu iliyopita, kwa sasa ndiyo gumzo kuliko nyingine yoyote. Simba ilikuwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ikipambana na Mbao FC.


Mbao FC imepanda daraja msimu huu na sasa inapambana kujiokoa kuepuka kuteremka daraja ikiwa na pointi 27 katika nafasi ya 13 kati ya timu 16 katika ligi hiyo.


Inayoshika mkia ni JKT Ruvu ikiwa na pointi 22. Hii inaonyesha hali si salama kwa Mbao FC na pointi tatu dhidi ya Simba, zilikuwa muhimu sana lakini mwisho ikalala kwa mabao 3-2.


Simba ilikuwa nyuma kwa mabao 2-0 hadi mapumziko, ikaendelea kuwa nyuma hadi dakika ya 82 lakini dakika saba za mwisho ikafanikiwa kupata mabao matatu na kubadilisha matokeo ya mechi kuwa 3-2.

Simba ambayo ilikuwa pia inazihitaji pointi hizo katika mbio zake za kubeba ubingwa ikafanikiwa na Mbao iliyozitaka kujiokoa, ikashindwa.


Baada ya hapo, umeibuka mjadala mkubwa na sasa mzigo umemuangukia kipa Eric Ngwengwe wa Mbao FC ambaye alifanya vema katika mechi hiyo ukiachana na makosa mawili ambayo huenda ndiyo gumzo.


Alipoteza ‘timing’ mara mbili, kushindwa kumuwahi Frederic Blagnon waliporuka juu, hilo likawa bao la kwanza na mpira ulipomgonga miguu na kumkuta Blagnon tena aliyefunga bao la pili.

Simba imetoka Kagera ambako ilikutana na kipigo cha mabao 2-1. Wengi walitegemea kumuona kipa Juma Kaseja “akikosea” ili gumzo liwe aliiachia Simba. Haikuwa hivyo.


Ngwengwe amedaka kwa dakika 82 akilinda lango lake vizuri. Makosa aliyofanya, ukianza lile la kwanza, kipa anapotoka langoni hasa kufuata mpira wa juu, lazima kuwe na beki nyuma yake hasa langoni, hakuwepo!


Kosa la pili, baada ya mpira kumgonga, kama Blagnon angeukosa, basi nafasi ya pili ingekuwa kwa Laudit Mavugo wa Simba kwa kuwa mabeki wa Mbao FC hawakuwa katika nafasi ya kumsaidia kipa huyo. Nao wanaweza kuwa watuhumiwa?


Sasa mjadala ni huo, kuna taarifa Mbao FC wameanza uchunguzi wa jambo hilo na kuna taarifa Ngwengwe amesimamishwa, eti uchunguzi unafanyika. Wanataka kujua kama kuna hongo ilitolewa.


Lakini unajiuliza ilitoka saa ngapi, nani alimuambia Ngwengwe au kumpa, aliipata wapi nafasi hiyo wakati akiwa uwanjani?


Jiulize na uwe mtenda haki, ndani ya kipindi cha dakika 45, Mbao FC inaweza kuifunga Simba mabao mawili. Simba haiwezi kuifunga Mbao FC mabao matatu?


Ukiangalia katika msimamo, Simba ina mabao 44 ya kufunga, yaani ilikuwa na 41 kabla ya mabao hayo matatu. Mbao FC sasa ina 26, kabla ilikuwa na 24. Simba imefunga karibu mara mbili ya mabao ya Mbao FC, kipi cha kushangaza?


Wengi wanaojadili suala hili wanajadili ujinga, hakuna mwenye uthibitisho kuwa kipa huyo kahongwa kama anavyotuhumiwa, tumeelezwa uchunguzi unaendelea, vipi tunamhukumu?

Hili ni kosa la kwanza? Jiulize Peter Manyika alihongwa bao la kwanza la Mbao FC? Vipi wote tumehamia katika mjadala huu unaothibitisha ushabiki zaidi kuliko haki, au ushabiki usioweza kuangalia ukweli zaidi ya kulazimisha kukandamiza.


Simba ilipofungwa na Kagera Sugar, nani alisikika akisema wachezaji wake walihongwa ili kupoteza mechi hiyo?
Yanga ambao ni mabingwa watetezi walifungwa na Simba mabao mawili baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0, tena Yanga ilipata bao ndani ya dakika 10 za mwanzo za mchezo. 

Wakiwa pungufu mtu mmoja, Simba waliifunga Yanga mabao mawili na mwisho wakashinda 2-1, tena nusura wafunge bao la tatu baada ya Mavugo kuwatoka mabeki watatu wa Yanga na shuti lake kumpita kipa lakini likagonga mwamba na kurudi uwanjani!


Jiulize, lililotokea katika mechi dhidi ya Yanga na hilo dhidi ya Mbao FC, ipi tofauti kubwa. Kama Simba ilifunga mabao mawili dhidi ya Yanga tena ikiwa pungufu mtu mmoja, nyuma bao moja! Kipi cha kushangaza kufunga mabao matatu dhidi ya Mbao FC?

Wakati mwingine vizuri kujadili kitu kwa hoja zenye msingi au faida. Si sahihi kugeuza soka sehemu ya kupoteza muda na kuumiza vichwa kwa mambo yasiyo na msingi.

Wale wanaochochea mijadala hii ni kwa matakwa yao na matakwa ya upenzi. Upenzi hauwezi kuzidi nguvu ya ukweli.
Kwa Mbao FC nao wamechangia kuonekana wanapelekwa na mihemko, lakini kipa Ngwengwe naye ni sehemu ya tatizo kutokana na kuanza kuzungumza mambo ya kuona kiza uwanjani wakati akijua makosa yake ni ya kimchezo na yameonekana wazi.

Wakati mwingine ni vizuri kuangalia mambo kwa jicho la kuchimba na hasa kwa wale ambao wanapata nafasi ya kuelezea au kuchambua kupitia vyombo vya habari. Kujitofautisha na ushabiki kama unazungumza kupitia vyombo, linakuwa jambo jema.
Vizuri kuutumia muda tulionao vizuri kuzungumza mambo yenye tija ili kujenga michezo, kuliko mambo ya kijinga kuyalazimisha yaonekane ya maana.


SOURCE: CHAMPIONI 

1 COMMENTS:

  1. MAWAZO MAZURI SANA HAYA, ASANTE NIMEKUELEWA BRO.

    ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV