April 20, 2017Na Saleh Ally
Mtanzania Mbwana Samatta ni kama wewe na mimi kwa vitu vingi sana. Ninaamini unakubaliana nami.

Samatta ni binadamu, anakula, anakunywa, anachoka, analala na ikiwezekana anaweza kuugua.

Unajua Samatta anaweza kuchukua, kufurahi, kuumia. Pia Samatta ni Mtanzania na hapishani nasi kwa mambo mengi sana.

Kisoka au kikazi anaweza kuwa na tofauti kubwa sana na wengi kwa kuwa Watanzania wengi ni watu tusio na tabia za kupambana, tunapenda kuridhika mapema na huenda kupumzika ni jambo namba moja.

Wengi wetu, midomoni ni hodari lakini ukizungumzia utekelezaji au vitendo, ni wachovu kabisa ambao tunaamini porojo zinaweza kusababisha upatikanaji wa mafanikio.

Samatta anaamini mafanikio yanaweza kupatikana sehemu yoyote ile ndiyo maana alikubali kutoka Mbagala Market iliyobadilishwa kuwa African Lyon na kuichezea Simba inayovaa rangi nyekundu.

Simba ndiyo iliyomtangaza Samatta kimataifa na kusajiliwa na TP Mazembe, timu inayovaa jeuzi zenye rangi nyeupe na michirizi ya rangi nyeusi.

Mtanzania huyo amefanya vizuri sana akiwa na Mazembe, akafanikiwa kuchukua makombe makubwa Afrika ikiwa ni pamoja na kutushangaza kuwa kumbe inawezekana katika kila tuliloona ni gumu.

Mtanzania kutegemewa na timu kubwa kama TP Mazembe! Wako wapi Wakongo wenyewe? Wako wapi Wanigeria, Wacameroon au Waghana? Kweli Samatta ndiye kinara wao?

Samatta amecheza hadi Kombe la Dunia ngazi ya klabu. Tena amecheza mara nyingi au sawa na wachezaji kama Wayne Rooney. Hili si jambo dogo.

Sasa Samatta ni kijana anayetamba katika kikosi cha KRC Genk kinachoshiriki michuano ya Europa League na timu kama Manchester United inayofundishwa na Kocha Jose Mourinho.

Samatta huyu aliamini kutoka Mbagala Market hadi Simba, angeweza kupambana na kufanya vizuri.

Akaamini kuwa anaweza kutoka Simba na kufanya kweli kwa kuushinda ushindani wa TP Mazembe, kweli akaweza.

Baada ya hapo, akaondoka kwenda Ulaya ambako wengi waliamini huenda amekosea. Kweli anaonekana kuweza na anapambana kweli kutaka kufanya vema zaidi.

Huyu Samatta ni Mtanzania kweli? Kama wote tunasema YES NI MTANZANIA. Vipi wengi wetu ni wazembe, tuna visingizio, tuna maneno mengi, hatupendi kujituma na tunaamini majungu na porojo?

Tunataka kufanikiwa machoni bila matendo? Mnaocheza mpira hamtamani mafanikio ya Samatta nanyi mpambane kwa vitendo na si maneno?

Msio wachezaji mpira, hamuoni juhudi na maarifa za Samatta zinaweza kuwa changamoto katika maisha yenu ya kawaida na mkafanikiwa.

Huku kijana wa Mbagala ana somo kubwa. Kama unajiona duni, unaweza kujipima kwake. Lazima tukubali, anapambana na kazi yake si rahisi na tusiendelee kumsifia pekee badala yake tujifunze kupitia kwake.

Mafanikio yake yanaweza kuwa chachu ya mabadiliko na baadaye mafanikio kwa wengi. Tupunguze longolongo tu, tubadilike na kupambana.


Mimi napenda rangi za Samatta, nyekundu, nyeupe na bluu, zote ameng’ara nazo kwa kuwa tu si mtu wa longolongo.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV