April 28, 2017Na Saleh Ally
KUNA vigezo vya kuweza kumuita kocha kuwa ni kocha mkubwa. Rafael Benitez Maudes hauwezi kumuacha hata ufanyeje kwa kuwa anaingia katika kila kigezo.


Nitakupa baadhi ya vigezo kama mafanikio ya vikombe, ukubwa wa makombe, ukubwa wa timu alizofundisha au wachezaji maarufu au wakubwa aliowafundisha.


Benitez ambaye alichipukia kisoka katika timu ya Madrid, ingawa hakufanikiwa kufanya vizuri kwa kuishia katika timu za vijana na zile za vyuo vikuu lakini Benitez amekuwa kocha mkubwa na wa mfano.


Amefundisha timu kubwa katika ligi tatu kubwa za Ulaya. Katika La Liga amefundisha Real Valladolid, Osasuna, Tenerife, Valencia na Real Madrid, Italia yaani Serie A amezinoa Inter Milan na Napoli na Premier League amefundisha Liverpool, Chelsea akiwa kocha wa muda na baadaye Newcastle.


Benitez raia wa Hispania ambaye sasa ni kocha wa Newcastle, amepata mafanikio katika kila ligi katika zote tatu, alibeba kombe na hii inamfanya kuwa kocha bora kabisa. 


England ambako kunaonekana kugumu, alibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa akiwa na Liverpool, akabeba Kombe la Europa League, lakini Kombe la Dunia la klabu akiwa na Inter Milan.Benitez ni kocha mkubwa, maana wengi unawajua wakubwa na mfano mzuri Arsene Wenger hawajawahi kubeba Europa Cup, Ligi ya Mabingwa Ulaya au Kombe la Dunia la Klabu, si jambo dogo.


Alinishangaza sana msimu uliopita alipoamua kujiunga na Newcastle ikiwa na hali ngumu, ikiwa njiani kuteremka daraja.


Siwezi kuamini kwamba Benitez alikuwa na “njaa” ndiyo maana aliamua kujiunga na timu ambayo hali yake ilikuwa ngumu na kunusurika kuteremka daraja ilikuwa ni asilimia chache sana.


Baada ya kuteremka daraja, nikiamini Benitez ni kocha mkubwa na isingekuwa rahisi kukubali kubaki Ligi Daraja la Kwanza England, alinishangaza kwa kukubali kuteremka na Newcastle akiahidi atarejea.


Hii ilinikumbusha lile sakata la Italia kwenye Serie A wakati Juventus ilipopokwa pointi na kuvuliwa ubingwa baada ya lile la sakata la upangaji matokeo. Mshambulizi nyota wa Juventus wakati huo, Zlatan Ibrahimovic aligoma kuendelea kuichezea timu hiyo kwa kuwa Serie B ambayo ni daraja la kwanza, “si saizi” yake.


Zlatan ambaye ni muwazi na asiyepindisha maneno, alisema wazi si kiwango cha kucheza daraja la kwanza, lakini Benitez aliamini inawezekana na akarejea chini.


Ligi Daraja la Kwanza England ina timu 24, kila timu inacheza mechi 46 ili kumaliza msimu na Newcastle ilipata upinzani mkubwa kwa Brighton & Hove ambao ndiyo wamekuwa wa kwanza kupanda baada ya kufikisha pointi 92 sasa.

Newcastle ambao waliongoza kwa muda mrefu kabla ya kuteleza mwishoni, nao wamerejea Ligi Kuu England baada ya kufikisha pointi 88. Timu zote mbili zina mechi mbili mkononi na kama Brighton & Hove watateleza, basi Newcastle wanaweza kuwa mabingwa na ukumbuke, kwenye ligi yoyote inayohusisha kupanda, ubingwa ni jambo namba mbili, kupanda ndiyo namba moja.


Mimi nimejifunza hapa kwa Benitez, ndiyo nikaamua kuwaunganisha nanyi tufaidike sote kwamba kuamini uwezo wako na kujikubali ni sehemu ya kuonyesha unajitambua.


Kutegemea matokeo ya ulichokifanya pia inaweza isiwe sahihi kutokana na lililo mbele yako badala yake vema kufanya mambo kwa vitendo.


Benitez anajua yeye ni kocha mkubwa na ukubwa wake ulikwama baada ya kujiunga na Newcastle Machi 11, miezi miwili haikutosha na Mei akawa ameishapata uhakika kuwa ameteremka.

Kwa sasa, unaweza kusema Benitez kweli ni kocha mkubwa kwa kuwa amekubali kwenda chini tena katika ligi inayoaminika ni ngumu zaidi kama wanavyoamini Waingereza ambao husema Championship ni ngumu zaidi ya Premier League.


Amekwenda hadi daraja la kwanza na kuirejesha timu, ameonyesha anaamini zaidi uwezo wake kuliko ukubwa wake na hii itampa soko kubwa na kuingia kwenye kumbukumbu za historia ya Newcastle.

Wakati mwingine kuanza upya si ujinga, kuanza upya kunaweza kuwa kipimo bora zaidi ya mwendelezo wa baadaye. Kuanza upya, kunaweza kusimamia thamani yako na ubora wako kama ambavyo leo unaweza kuuona ubora wa Benitez.Benitez si muoga, anajiamini na anauamini uwezo wake na kweli ameweza. Jipime, umewahi kujiamini kwa kiwango hiki au kutojiamini kumefanya ukwepe mengi ambayo ungeweza kuyafanya kwa ufasaha na mafanikio. Najua, unakumbuka!

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV