Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga Mbrazili, Andrey Coutihno ambaye hivi sasa anachezea Nongbua Pitchaya FC ya Thailand, amesema bado ana ndoto za kurejea Jangwani.
Mbrazili huyo aliondoka Yanga kwenye msimu wa 2014/2015 baada ya kusitishiwa mkataba wake kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Mniger, Issofou Boubacar aliyeichezea timu hiyo kwa miezi sita.
Coutihno kabla ya kutua kuichezea Nongbua Pitchaya alikuwa akicheza soka la kulipwa huko Myanmar barani Asia.
Akizungumza, Coutinho amesema bado ana mapenzi ya klabu yake hiyo ya zamani aliyoichezea kwa mafanikio ya kutwaa taji la ubingwa wa ligi kuu na Ngao ya Jamii, mwaka 2014.
Coutihno alisema angependa kurejea kuichezea Yanga mara baada ya mkataba wake kumalizika lakini siyo hivi sasa huku akiwataja viungo wawili Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mzimbabwe, Thabani Kamusoko ambao anatamani siku moja acheze nao.
"Nashukuru hivi sasa ninaendelea vizuri na nimeondoka Myanmar nilipokuwa nacheza soka na kuhamia nchini Thailand kwenye Klabu ya Nongbua Pitchaya FC.
"Bado nina mipango ya kurejea kuichezea tena kwa mara ya pili Yanga kama wakinihitaji nitarejea hapo baadaye mkataba wangu ukiwa umemalizika.
"Ninafurahi maslahi ya huku Thailand ninayoyapata zaidi ya huko nilipokuwa nacheza awali," alisema Coutihno anayetumia mguu wa kushoto.
0 COMMENTS:
Post a Comment