May 21, 2017

ABDULRAHMAN AKIWANIA MPIRA NA SIMON MSUVA, WOTE WAWILI WAMEFUNGA MABAO 14 KATIKA LIGI KUU BARA...



Na Masau Bwire
MSHAMBULIAJI Abdulrahaman Musa  wa Ruvu Shooting ndiye shujaa katika msimu huu wa Ligi ya VPL uliohitimishwa May 20, 2017.

Abdulrahaman katika msimu huu wa Ligi amecheza dakika 2,700 katika michezo yote 30 iliyochezwa na kila timu pasipo kupumzika na kufanikiwa kufunga magoli 14 kati ya hayo, mawili yakiwa ya pinati.

Magoli aliyofunga Abdulrahaman ni dhidi ya Simba (1), mzunguko wa kwanza, Taifa, Yanga (1), mzunguko wa kwanza, Taifa, Ndanda Fc (1, penati), mzunguko wa kwanza, Mabatini, Mbao (1), mzunguko wa kwanza, Mabatini, JKT Ruvu (2), moja kila mchezo, nyumbani na ugenini, Majimaji (3), mzunguko wa pili, Mabatini, Mbeya City (1), mzunguko wa pili, Sokoine, Mbeya, African Lyon (1), mzunguko wa pili, Chamazi Complex, Mwadui (1, penati), mzunguko wa pili, Mwadui Complex, Shinyanga na Stand United (1), mzunguko wa pili, Kambarage Shinyanga.

Abdulrahaman alizaliwa Januari Mosi, mwaka 1995, Hospital ya mkoa wa Mtwara, Ligula akiwa  mtoto wa tano kati ya watoto sita wa mzee Musa Abdulrahaman na mama Somoe Salum.

Mwaka 2001 alianza masomo yake, darasa la kwanza na kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2007.

Mwaka 2008 alianza masomo ya Sekondari katika shule ya Sekondari Mitengo, Mikindani, Mtwara ambapo alihitimu kidato cha nne mwaka 2011.

Mwaka 2012, akichezea timu ya Korosho ya Mtwara iliyokuwa ikishiriki mashindano ya mabingwa wa Mikoa kituo cha Mlandizi alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mpira kiasi cha kumvutia kocha wa Ruvu Shooting, kwa wakati Charles Boniface Mkwasa ambaye aliushawishi uongozi wa timu kumsajili. Baada ya ligi hiyo kumalizika, Abdulrahaman alisajiliwa na timu ya Ruvu Shooting akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na timu ya Korosho kumalizika.



Akiwa na timu ya Ruvu Shooting alionesha uwezo na umahili mkubwa katika kucheza mpira ambapo, mwaka 2013 aliajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kufanya kazi (Askari) Kikosi cha Jeshi 832, Ruvu JKT .
Msimu wa ligi ya VPL, 2014/15 timu ya Ruvu Shooting ilishuka daraja, Abdulrahaman akaenda kuichezea kwa mkopo timu ya JKT Ruvu msimu wa 2015/16.

Akiwa huko, aliendelea kung'ara ambapo msimu wa ligi 2015/16 alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa VPL, mwezi May baada ya kuisaidia timu yake kushinda michezo miwili mfululizo, dhidi ya Ndanda alifunga magoli mawili na Simba uwanja wa Taifa pia akafunga magoli mawili.

Msimu huu wa ligi VPL, Ruvu Shooting ilimrejesha kikosini ambapo aliendelea kutema cheche na kuonesha kiwango kikubwa mno cha kucheza mpira ambapo mwezi April alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa VPL mwezi April na kukabidhiwa kitita cha Tsh 1,000,000 kutoka kwa mdhamini, Kampuni ya simu za mkononi Vodacom.

Abdulrahaman mbali ya uwezo mkubwa wa kucheza mpira, ni mwenye nidhamu ya hali ya juu nje na ndani ya uwanja. Hili linadhihirishwa na kumaliza musimu mzima wa ligi, mechi 30 alizocheza kwa jumla ya dakika 2,700 alikanywa mara moja tu kwa kadi ya njano na mwamuzi Mbaraka Rashid katika mchezo dhidi ya Majimaji uliofanyika Mabatini.

Abdulrahaman ni mchezaji mwenye nguvu, maarifa na akili katika mpira, ni mvumilivu, hachoki wala hakati tamaa awapo uwanja.

Katika mchezo wa mwisho wa VPL, 2016/17 uliofanyika May 20, dhidi ya Stand United, Kambarage, kijana huyo alishangaza wengi kwa mengi katika uchezaji wake wa mpira namna anavyo haha uwanja mzima japo yeye hucheza pembeni (winger) kushpto na kulia.

Dakika ya 60 ya mchezo, Abdulrahaman aliumia vibaya, alipasuka kichwa baada ya kupigwa kichwa na beki wa Stand, akatokwa na damu nyingi katika jeraha hilo la upande wa kushoto wa kichwa chake, juu kidogo ya sikio, jeraha lililoshonwa nyuzi tatu na daktari wa timu Genoveva Kampala.



Haikuwa rahisi kwa hali ya jeraha hilo, namna damu zilivyokuwa zikimtoka, kurudi tena uwanjani na kucheza kwa kasi ile ile na hatimaye kupachika goli lililomfanya awe mfungaji bora. Tulishuhudia mchezaji mmoja mahili aligongana na mchezaji mwenzake uwanja wa Taifa akaumia kidogo kichwani, alizirai! Hapo unaiona tofauti ya dona na viazi dume!

Matibabu ya kulishona jeraha hilo yalimchukuwa Daktari Kampala dakika 17, toka dakika ya 60 ya mchezo hadi dakika 77.

Pamoja na maumivu, Abdulrahaman aliomba nafasi yake isifanyiwe marekebisho akidai atashonwa jeraha, ataingia kucheza hatakama imebaki dakika moja ili atafute goli litakalompa kiatu cha dhahabu! 

Ndoto ya mchezaji huyo Kinda ilitimia kwani, baada ya kuingia dakika ya 77, alicheza kama hajaumia popote, juhudi zake zikazaa matunda kwa kufunga goli safi dakika ya 89.


Abdulrahaman Musa ameoa, ana mke, Swaiba Abdallah Kaisi na mtoto mmoja, Wahda Abdulrahaman.

Mwandishi wa makala haya, ni msemaji wa klabu ya Ruvu Shooting, pia ni mwalimu wa Shule ya Msingi Makumbusho ya jijini Dar es Salaam.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic