May 20, 2017Beki wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy amemtupia kijembe Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Simba, Haji Manara akimwambia kama angeendelea kubaki huko kombe angebeba wapi?

Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya Yanga kuifunga Toto African bao 1-0 mapema wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.

Awali, Manara alionekana akimpiga vijembe Kessy kuhusiana na maamuzi yake ya kutoka Simba na kwenda Yanga akimwambia amelifuata benchi baada ya mechi za mwanzoni kutopata nafasi kikosi cha kwanza.

Kessy amesema aliondoka Simba na kwenda Yanga kusaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo kwa ajili ya kubeba mataji ya ligi kuu na siyo kitu kingine.

Kessy alisema, anaamini kama angeendelea kubaki kuichezea Simba, basi ndoto zake za kubeba makombe zingepotea kutokana na timu hiyo kuukosa ubingwa wa ligi kwa mwaka wa tano mfululizo.

Aliongeza anajisikia furaha kuona Yanga ikiendelea kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili mfululizo tangu ametua kuichezea timu hiyo.

“Kama unakumbuka wakati nakaa benchi na kukosa nafasi ya kucheza Yanga, (Manara) alikuwa anazungumza sana kuhusiana na mimi, lakini nilikaa kimya kwa malengo ambayo hivi sasa yamekamilika.

“Nashukuru timu yangu inachukua ubingwa wa ligi kuu mimi nikiwepo uwanjani nikiipambania, pia nimeitwa timu ya taifa.


“Nafikiri hizi ni salamu tosha kwa Manara, sasa aendelee kuchonga tena kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, kikubwa afahamu kuwa mimi nimefuata makombe Yanga,” alisema Kessy.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV