May 17, 2017


Na Saleh Ally
NIMEKUWA nikimfuatilia kwa karibu sana mshambuliaji wa Yanga ambaye amejiunga na mabingwa hao wa Tanzania Bara akitokea Mgambo Shooting ya Tanga.

Huyu ni Malimi Busungu. Kama unakumbuka wakati wa usajili kabla ya kuanza kwa msimu uliopita, Busungu alikuwa gumzo akigombewa na klabu mbalimbali na wakongwe, Yanga na Simba walikuwa wameingia katika vita hiyo.

Ilionekana Busungu angeenda Simba, lakini mwishoni alijiunga Yanga ambayo ilimsajili kwa kumpa fedha pamoja na gari aina ya Toyota IST. Gumzo lake likawa limechukua sehemu ya yale yaliyotamba wakati wa usajili.

Kama ilivyo ada, usajili unapopita, kinachofuata huwa ni kazi. Kipindi cha klabu kuona wapi imekosea na wapi imepatia kutokana na usajili ilioufanya. Ingawa Busungu hakupata nafasi ya kutosha, lakini baadaye alianza kuonyesha anainuka na mwisho akafunga katika moja ya mechi ambazo Yanga iliwafunga wapinzani wake Simba.

Busungu alifunga bao la pili akiwa anatokea benchi ambalo lilikuwa ni jambo zuri kabisa kwa kuwa ndiyo furaha namba moja kwa mashabiki wa Yanga; kuifunga Simba.

 Naamini unakumbuka, baada ya hapo ikawa ni “Busungu, Busungu.” Hakuna tena kama Busungu na furaha ya Wanayanga na uaminifu kwake ukazidi kupanda.

Mategemeo ya wengi ni Busungu kufanya vizuri zaidi. Lakini ajabu baada ya hapo akaanza kurudi nyuma na mwishowe ndiye Busungu tuliyenaye.

Busungu ambaye naona kuwa “ameshindikana” kwa kuwa hakuna anayeonekana ameweza kumrudisha katika njia sahihi au salama.

Kwanza alilalamika Kocha Hans Van der Pluijm hakuwa akimpa nafasi bila ya sababu za msingi. Alipompa aliona haukuwa muda wa kutosha. Lakini katika hali ya kawaida mshambulizi kama yeye, ilikuwa ni lazima afanye kazi ya ziada kuwapangua watu kama akina Amissi Tambwe, Donald Ngoma na wenzake ambao tayari walikuwa na nafasi zao kutokana na ubora wao wa kazi ndani ya Yanga.

Hakuna ubishi hata wakati Busungu akiwa Mgambo, bado Ngoma na Tambwe walikuwa bora kuliko yeye kama utafanya ujumuisho wa ligi nzima.

Sasa anapokwenda Yanga, vipi atapata nafasi ya kucheza kirahisi utafikiri embe dodo lililodondoka lenyewe kutoka juu ya mwembe? Lazima afanye kazi ya kulenga mwenyewe na kama anaweza, basi apande juu ya mti kwenda kulitungua.Lakini utaona Busungu anaingia Yanga hakuwa akijitambua vizuri. Hakuwa amejiandaa kwa ushindani ambao ataukuta Yanga na badala yake akaanza kuona huenda anawazidi aliowakuta kutokana na bao alilofunga dhidi ya Yanga.

Lawama akamuangushia Pluijm ambaye mwisho walikorofishana na akaamua kumuweka kando katika kikosi chake akidai alikuwa akionyesha tabia za “ajabu”.

Pluijm alimtuhumu Busungu hakuwa na subira ambaye yuko tayari kuendelea kupambana. Baada ya hapo Yanga ikapata kocha mpya, George Lwandamina ambaye aliamua kumpa nafasi na kumuingiza katika kikosi.

 Alimpa nafasi katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, baadaye akamtoa na hilo likawa kosa, akasusa. Baadaye Lwandamina angependa kuendelea na wengine wanaofanya vizuri.

Kumekuwa na taarifa kwamba Busungu ana matatizo na mmoja wa makocha. Jambo ambalo linaweza kumtokea binadamu yeyote. Lakini hili lililotokea hivi karibuni la picha za Busungu kusambaa akiwa amelewa chakari, si jambo jema.

 Busungu amekuwa hapokei simu na meneja wake pia amesema amekuwa akihangaika kumpata na atakutana naye. Hili ni jambo ambalo Busungu anapaswa kukubali kuwa yeye ana matatizo ili apate chumba cha kujirekebisha.

Anaweza akawa anaamini anaonewa lakini ukweli matatizo mengi yanaweza kuwa yanaanzia kwake. Inaonyesha hivi, kama hatakubali kwamba ana shida, basi hatapata nafasi ya kujirekebisha.Kama angekuwa hana shida yeye, basi angefanikiwa. Hakuna kocha ana mchezaji anaamini ni msaada halafu aache kumtumia. Tumeona Yanga ikiwa imeandamwa na majeraha, Tambwe, Ngoma na Chirwa alikuwa amegoma. Vipi hakupewa nafasi yeye?

 Picha zile zinaonyesha ni kama mtu ambaye ana matatizo ya kisaikolojia. Na mambo mawili yanatakiwa kufanyika. Moja watu walio karibu naye kumuweka chini na kuzungumza naye na pili yeye kukubali kwamba kuna tatizo.

Kama Busungu ataendelea kuona anaonewa, hapendwi au hana bahati. Basi mambo yataendelea kubaki hivyohivyo hadi mwisho na ndiyo utakuwa mwisho wake.

Mara nyingi wasio tayari kuangalia kinachowaangusha, husema wanamuachia Mungu. Lakini ninaamini Mungu ametufundisha kukubali na kurekebisha makosa. Au kukubali kukosolewa ili kurekebisha ulipokosea. Kabla ya kumuachia Mungu, vizuri Busungu akajikabidhi hili suala linalomkabili ili aweze kulirekebisha kwa kuwa uwezo wa kufanya vizuri kama mchezaji anao lakini akiwa na haya yaliyomzunguka, nafasi ya kuendelea na kung’ara, hana.

SOURCE: CHAMPIONI0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV