May 8, 2017


THAMANI ya Ligi Kuu ya Kenya maarufu kama Kenya Premier League imekuwa ikipanda kwa kasi kubwa na kuanza kurejesha heshima ya soka la Kenya.

Kabla, soka la Kenya lilionekana limepoteza mvuto kabisa na kwa zaidi ya misimu nane limekuwa likisuasua na kuandamwa na migogoro ya kila aina.

Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), chini ya mkongwe Sam Nyamweya lilionekana kupoteza mwelekeo na mambo yakazidi kuwa magumu.

Ilifikia wakati kukawa na ligi mbili ndani ya nchi moja. Ligi moja ilisimamiwa na FKF na nyingine bodi ya ligi.

Mwisho wa msimu, kukawa na bingwa wawili, washindi wa pili wawili halikadhalika watatu na wengineo. Hii ilikuwa ni sehemu ya kuonyesha kwamba soka la Kenya limekosa mwelekeo kabisa.


Miaka minne iliyopita wakati Nyamweya anakaribia kuondoka, timu ya taifa ya Kenya “Harambee Stars” chini ya Kocha Adel Amrouche, ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji lililofanyika nchini humo.

Wengi walishangazwa na sifa nyingi zikaenda kwa kocha Amrouche raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria. Kwamba ana uwezo wa kufanya katika mazingira magumu kama alivyokuwa akiifundisha Burundi.

Uchaguzi uliofuata, Nyamweya aliangushwa na Nick Mwendwa, akiwa ni rais kijana kushika nafasi hiyo. Wengi waliingiwa hofu angeweza vipi kuendesha mambo naye alikubaliana na hali haikuwa nzuri.


Mwaka wa kwanza, hali ilionekana kuzidi kuwa ngumu na ule usemi kwamba angekwama ukazidi kuchukua nafasi.
Lakini wakati ikionekana na Mwendwa alikuwa ameshindwa, ghafla mambo yalibadilika na kuanza kwenda kwa kasi kubwa.

Wengi wakaonekana kushangazwa kwa kuwa Kenya ilikuwa kati ya timu zilizokuwa chini ya kiwango cha 130 katika viwango vya soka vya Fifa. Hawakuwa tena na tofauti na Tanzania ambao angalau walikuwa na nafuu.

Utaona ule mlolongo wa wachezaji wengi wa Kenya na hata Uganda kukimbilia Tanzania ulizidi kuongezeka kwa kuwa hata zile timu kama Sofapaka zilizokuwa zikilipa vizuri zilidorora na wakongwe Gor Mahia na AFC Leopards walikuwa wameyumba na kuonekana hawana nafasi kwani kila walipoinuka walianza kuyumba tena.

Mwendwa akaonekana ni shujaa, lakini ukweli ni udhamini mnono ambao walianza kuufanya kampuni ya masuala ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa.

SportPesa walidhamini timu zote kongwe mbili za Gor Mahia na AFC Leopard na kawaida wao ndiyo chachu ya ushindani. Pia wakadhamini timu nyingine na Nakuru All Stars.


Kama hiyo haitoshi, kampuni hiyo ikaingiza udhamini mnono katika Ligi Kuu Kenya na kufanya kuwe na ushindani zaidi kwa kuwa fedha hizo zinaingia kwenye mifuko ya timu zote 18 zinazoshiriki ligi hiyo.

Ukiangalia thamani ya ligi ya Kenya imepanda, ushindani umerudi na hamasa hata ya mashabiki kwenda viwanjani imerudi kwa kasi kubwa na sasa ni kati ya ligi zilizo juu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Taarifa zimekuwa zikieleza SportPesa tayari wako nchini na wamenuia kuzidhamini Yanga na Simba ambazo ni timu zenye mashabiki zaidi katika ukanda huu.

Inawezekana siku moja wakaingia kwenye ligi lakini kampuni hiyo kama itatumika vizuri basi inaweza kurejesha hamasa tena.

Huenda tuaona kawaida lakini mfano mzuri, Simba kwa msimu mzima wa 2016-17 imecheza kwa hasara kama tulivyowahi kuandika makala.

Kwamba hawana mdhamini na vifua vyao ni mali, lakini hakukuwa na aliyeona thamani yao baada ya kujiondoa kwa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Shukrani kwa TBL kwa kuwa waliweza kujali angalau kwa misimu kadhaa. Lakini kama SportPesa basi ndiyo wakati mwingine wa kurejesha heshima ya soka nchini.

Hakuna unapoweza kukwepa fedha katika maendeleo ya soka. Vizuri pia kufanya kazi na watu waliojifunza kupitia hatua mbalimbali.

Mfano SportPesa wanadhamini timu ya Ligi Kuu England (EPL), Hull City. Unapozungumzia udhamini wanajua nini cha kufanya kusaidia zaidi.

Kawaida wadhamini walioendelea hupenda mafanikio kwa wale wanaowadhamini. Hii ni nafasi kwa Yanga na Simba kubadili mambo na hasa kama wataingia udhamini, basi fedha watakazozipata ziwe kwa ajili ya maendeleo na si mifuko ya wahusika.
SportPesa ni sehemu wa wadhamini wa klabu maarufu ya Arsenal ya England. Hivyo wanajua kitu kinachoweza kuwasaidia Yanga na Simba lakini soka la Tanzania.

Kikubwa ambacho SportPesa wamekuwa wakikifanya ni kurudisha kiasi cha fedha kwa jamii kama udhamini. Wameweza kuzirudisha Gor Mahia na AFC Leopards katika ramani ya soka zikiwa na nguvu.


Simba na Yanga hazikuwa zimekufa lakini mwendo wao ulikuwa unaashiria “kifo”. Sasa ndiyo wakati mwafaka wa kutumia vizuri udhamini huo unaelezwa kuwa utakuwa mkubwa zaidi kuliko waliowahi kupata hapo awali.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV