Ruvu Shooting imeonesha nia ya kuzikomoa timu za Simba na Yanga ambazo zilikuwa zikimfuatilia mshambuliaji wake Abdulrahman Mussa kufuatia kumtafutia dili nchini Misri ambapo anatarajia kwenda kukipiga soka la kulipwa.
Abdulrahaman ndiye mchezaji aliyeibuka mfungaji bora msimu huu akifungana na Simon Msuva wa Yanga ambao wote kwa pamoja walifanikiwa kufunga mabao 14.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema kuwa, kuna timu kutoka nchini Misri imeonesha nia ya kumhitaji mchezaji huyo na iwapo mipango itakaa sawa mchezaji huyo wanaweza kumruhusu kwenda kujaribu bahati yake kwa kucheza soka la kulipwa nchini humo.
“Kuna timu kutoka nchini Misri inamhitaji Abdulrahamn ili kuweza kwenda kucheza soka la kulipwa kwa kuwa tayari walishakiona kiwango chake hivyo hawahitaji kumfanyia majaribio hata kidogo lakini siwezi kuiweka wazi timu hiyo kwa sasa hadi hapo mambo yatakapokamilika.
“Timu za Simba na Yanga zilimfuata mchezaji huyo lakini hakuwa tayari kuzichezea timu hizo kwa kipindi hiki kwani ameweza kuangalia kiwango chake zaidi kutokana na desturi ya timu hizo na pia kulinda maslahi yake binafsi ya hapo baadaye, hivyo alizikatalia kuzichezea msimu ujao.
“Kwa sasa tupo katika mchakato wa kuiangalia ofa hiyo iwapo itakuwa na maslahi hatuna budi kumuachia kwa kuwa tunachokiangalia sisi ni maslahi ya mchezaji kwakuwa kila mchezaji anahitaji mafanikio,” alisema Masau.
SOURCE; CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment