July 24, 2017



Na Saleh Ally
KIKOSI cha Singida United kimesajili jumla ya wachezaji 16 wapya kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Singida United ndiyo imepanda daraja msimu huu ikitokea Ligi Daraja la Kwanza na bahati nzuri moja kwa moja wamepata wadhamini kadhaa.

Kampuni ya Kubashiri ya SportPesa imekuwa ya kwanza kujitokeza kuidhamini Singida United kwa kutoa kitita cha Sh milioni 250 kwa mwaka huku wengine kama Puma nao wakiingia kutoa sapoti ya udhamini.

Wakati Singida United ikiwa imeanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, tayari imeshaanza kuwa gumzo kutokana na kusajili wachezaji wengi wapya lakini pia ule uamuzi wa kumchukua Kocha Hans van Der Pluijm.

Kama utataja kocha bora ndani ya misimu minne katika Ligi Kuu Bara, Pluijm raia wa Uholanzi ndiye kocha bora kabisa zaidi ya wengine kwa kuwa amebeba ubingwa na Yanga zaidi ya mara moja katika muda huo na kikosi chake kilionyesha uwezo mkubwa.

Usajili wa wachezaji 16, unathibitisha ile kauli yangu ya awali, kwamba Simba waliosajili wachezaji 12 wapya, hawakukosea kwa kuwa unahesabu wangapi waliotoka lakini pia unaangalia mbele ni michuano gani inafuata.



Simba waliangalia Ligi Kuu Bara, waliangalia Kombe la Shirikisho pia michuano ya kimataifa. Ndivyo ilivyo kwa Singida United ambao wanaangalia Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho lakini wakifikiria kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Kwa hali ilivyo sasa, baada ya kukamilika kwa usajili wa wachezaji 25, Singida United imetangaza kufunga usajili lakini presha kubwa sasa inaangukia kwa Kocha Pluijm.

Kama nilivyoeleza kwanza, hakuna anayeweza kukataa kwamba Pluijm ni kocha bora lakini presha kwake inaweza kuwa kubwa saizi ya kati au kubwa sana kulingana na mazingira.

Kwa sasa anafanya kazi ya kuunganisha kikosi chake chenye wachezaji 16 wapya kati ya hao saba wakiwa kutoka nje ya Tanzania na tisa pekee ndiyo wale waliopanda na timu.

Utaona wachezaji 16 wanakwenda kuzoea mazingira mapya wakiwa saba na tisa wamekutana hapo na tisa wengine ambao wamewakuta.

Muunganiko huu wa makundi matatu haiwezi kuwa kazi rahisi kwa Pluijm ingawa kuna mambo mawili lazima utayaona katika kikosi hicho.



Mapema:
Kutokana na namna wachezaji wanavyoweza kuendana haraka na mfumo wa kocha na wenyewe kuzoeana, inaweza kumsaidia Pluijm kutokuwa na presha kubwa na hii itamsaidia kupata utulivu na kufanya mambo yake kwa mpangilio mzuri na uhakika zaidi.

Wachezaji kuunasa mapema mfumo wa kocha na wenyewe kuelewana vizuri mapema ni mambo yanayoweza kutokea kutokana na aina ya wachezaji uliowapata.


Kuchelewa:
Bado inawezekana wachezaji wakachelewa kuunasa mfumo wa kocha halafu wakashindwa kuungana haraka kama kikosi.

Hii kwanza huisababisha timu kupoteza mechi au kupata sare mfululizo. Hali kama hii inapotokea mara nyingi husababisha presha kubwa miongoni mwa wachezaji, makocha na uongozi.

Kwa kawaida, uongozi mfano wa Singida United unakuwa haujui sana masuala ya ufundi. Badala yake unachoangalia umetoa nini na ungependa kupata mafanikio.

Lakini kiufundi, kuna mambo hayajali mmetoa kiasi gani, na kama ni jambo la kusubiri muda ni lazima mvute subira.

Kama Singida United itapoteza mechi mbili ndani ya tatu, lazima presha itaamka ndani ya kikosi hicho.

Kocha atakuwa ni mtu wa kwanza kuwa na hofu na huenda mipango yake haitaenda kama anavyotaka kwa kuwa wakati mwingine ni vizuri sana unapowapa mipango wawe wametulia ili uweze kuiingiza vizuri na wao waifanyie kazi.

Kama watakuwa katika presha kubwa, basi hawataweza kuelewa haraka na inawezekana wakachangia kuendelea kwa presha hiyo kwa muda mrefu zaidi.



Nini kifanyike?
Kwa wanaoiongoza Singida United, bila ya kujali wametoa nini lazima wajue timu yao imesajili wachezaji 16 wapya na hii ni rekodi katika Ligi Kuu Bara.

Kusajili wachezaji 16 ni kikosi kizima. Kama kikosi chote kimesajiliwa msimu huu maana yake inatakiwa kuwa na maandalizi ya kutosha na ikiwezekana suala la muda.

Kama ikitokea mambo yameanza vibaya basi ni vizuri kuunganisha nguvu, kupeana moyo na kushauriana kipi hasa cha kufanya ili kuweka mambo sawa.

Kwa wachezaji na kocha, hali kadhalika wajue wana jukumu la kuungana na kuwa kitu kimoja kinachofanya vizuri. Hivyo, suala la upendo ili kujenga umoja ni lazima na ikiwezekana wenyewe, wageni kutoka nje ya Tanzania na wageni wa hapa nyumbani lazima wakubaliane na ushindani unaojenga timu moja badala ya kuibomoa.

Kama wachezaji watajigawa makundi na kujenga nafasi kwa majungu, basi watajibomoa na mwisho mamilioni yaliyomwagwa Singida United, hayatakuwa na faida hata kidogo.

 WACHEZAJI 7 KUTOKA NJE:
 1. Elisha Muroiwa (Zimbabwe)
2. Twafadzwa Kutinyu (Zimbabwe)
3. Simbarashe Nhivi (Zimbabwe)
4. Wisdom Mtasa (Zimbabwe)
5. Shafik Batambuze (Uganda)
6. Dany Usengimana (Rwanda)
7. Michel Rusheshangoga (Rwanda)

WACHEZAJI WAPYA WA NDANI:
1. Atupele Green (JKT Ruvu)
2. Miraji Adam (Africa Lyon)
3. Kenny Ally (Mbeya City)
4. Roland Msonjo (Mshikamano FC)
5. Pastory Athans (Simba)
6. Deus Kaseke (Yanga)
7. Ally Mustapha ‘Barthez’ (Yanga)
8. Salum Chuku (Toto Africa)
9. Kigi Makasi (Ndanda FC).

FIN.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic