Timu zinazoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara(VPL), zinatarajiwa kukabidhiwa vifaa mbalimbali wiki hii na mdhamini mkuu wa ligi hiyo Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC, vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500/= .
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania PLC, Matina Nkurlu, alisema kuwa wameamua kutoa vifaa mapema ili waweze kuzipa muda wa kutosha timu zitakazoshiriki VPL inayotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu, ikiwa ni baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 23.
Alisema kwa mara nyingine katika kuhakikisha ligi ya soka nchini inaenda vizuri, kampuni yao inakabidhi vifaa mbalimbali vya ligi ili kuwezesha ushiriki wa timu katika msimu huu utakaoanza mwezi ujao bila kipingamizi.
Alivitaja vifaa vitakavyokabidhiwa kuwa ni jezi za mechi na mazoezi, viatu vya mechi na mazoezi, soksi, vilinda ugoko, glovu, ‘bibs’, pampu’, kitambaa cha nahodha, jezi na viatu vya waamuzi, sare za waokota mipira, mabegi ya kusafiria na vinginevyo vinavyozihusu timu, waamuzi na mchezo kwa ujumla.
“Tunajisikia furaha kwani vifaa vipo tayari na tutavikabidhi rasmi wiki hii tukiwa tunatekeleza matakwa ya mkataba wa udhamini, ni imani yetu kwamba timu zitakazoshiriki ligi zimejiandaa vya kutosha kwa msimu mpya wa ligi wa 2017/2018,” alisema Nkurlu.
Aliongeza: “Vodacom Tanzania inaendelea kudhamini ligi kuu kwasababu soka ni mchezo unaopendwa sana hapa Tanzania na duniani kote kwa ujumla, ukiwa na washabiki wengi, hivyo tunapenda kuona wananchi ambao baadhi yao ni wateja wetu, wanapata burudani ya mchezo waupendao, ukizingatia michezo ni ajira kubwa duniani, ikiendelezwa inaweza kubadilisha maisha ya watu wengi na taifa kunufaika kwa mapato makubwa ya kodi kutoka katika sekta hiyo.”
Aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi ya Tanzania na kuongeza maslahi kwa wachezaji wanaoshiriki ligi hiyo ambayo itashirikisha timu 16, zikiwamo tatu zilizopanda msimu huu.
“Tukiunganisha nguvu timu zetu zinaweza kuwa na wachezaji wa kimataifa na kufuata nyayo za Mtanzania Mbwana Samatta anayeipeperusha Bendera ya Tanzania huko Ulaya katika klabu ya Genk ya Ubelgiji. Ni muhimu kwa wadau mbalimbali kuanza kuwekeza katika timu za vijana chipukizi kwa kuwa vipaji vinaanzia ngazi ya chini,” alisema Nkurlu.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ambapo msimu huu inatarajiwa kutetea ubingwa wake, huku ikitarajiwa kupata changamoto ya aina yake kutoka kwa timu nyingine 15, wakiwamo watani wao wa jadi, Simba.
Mbali ya wakongwe hao wa soka nchini, timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo msimu huu ni Azam FC, Singida United, Kagera Sugar, Mbeya City, Njombe Mji, Mtibwa Sugar, Ndanda FC, Mbao FC, Tanzania Prisons, Majimaji, Mwadui, Ruvu Shooting, Lipuli na Stand United.
0 COMMENTS:
Post a Comment