July 7, 2017

NA SALEH ALLY
MARA nyingi tumekuwa tukijaribu kuangalia nini tunaweza kujifunza kupitia wenzetu nje ya Tanzania wanafanya nini kupata maendeleo ya mchezo wa mpira.

Kujifunza ni hivi; kwamba kuna vitu tunavijua lakini kutokana na mafanikio ambayo wamekuwa wakipata wenzetu hasa Ulaya na kwingineko barani Asia, tunaweza kujifunza zaidi ili kusaidia kupatikana kwa mafanikio.

Hauwezi kusema hatujui nini maana ya uendeshaji wa timu, utafutaji wa wadhamini au kuwa na vyanzo vya mapato ili kuendesha klabu zetu za soka.Hilo ni jambo la kawaida ambalo kimsingi kila mmoja anaweza kujua lakini mipango sahihi ya kufanya jambo hilo inakuwa ni ipi hasa au ipi ni sahihi kufanikisha jambo kwa ufasaha na kupata kile kinachopatikana?

Timu nyingi za Tanzania Bara, katika kipindi hiki ziko ‘busy’ sana na suala la usajili. Kila kikosi zinataka kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao kuhakikisha zinafanya vizuri katika michuano ya aina tatu.

Moja ni Ligi Kuu Bara, pili ni Kombe la Shirikisho na tatu kama imeishafuzu au itafuzu michuano ya kimataifa. Plani hii ni kwa kila timu ingawa mwisho inaweza kuwa ya timu chache.

Wakati usajili unaendelea, timu zikimwaga mamilioni ya fedha katika usajili, ninaamini kuna walakini mkubwa kuhusiana na suala la fedha za uendeshaji wa klabu kuanzia kipindi cha Agosti, mwaka huu hadi Mei, mwakani.Ninaamini klabu nyingi bado hazina mipango madhubuti ya kuwa na fungu au mpango wa kuhakikisha kuna fungu la fedha ambazo zitatosha kuiendesha klabu kwa muda wa miezi yote hiyo bila ya kuyumba.

Hapa ninazungumzia fedha za uendeshaji kwa maana ya kambi ambapo utakuta kuna malazi, chakula na kadhalika. Lakini kuna suala la usafiri ambao utajumuisha kama ni basi au ndege na kadhalika.

Ndani ya uendeshaji kuna mishahara ya wachezaji na maofisa wa klabu. Lakini usisahau suala la posho mfano mazoezini au timu inaposhinda mechi, suala la bonus ni muhimu na lipo duniani kote.

Nguvu nyingi ya viongozi ipo katika usajili, lakini ninaamini wengi hawajajiandaa katika uendeshaji wa klabu katika kipindi hicho au watatumia fedha nyingi wakati wa usajili halafu ikawa shida kubwa kifedha wakati wa uendeshaji katika kipindi cha ligi.

Ukinunua gari, ukawa huna fedha ya mafuta, basi hautakuwa na sababu hata robo ya kujivunia kuwa na gari. Wachezaji bora bila ya kuwa na uhakika wa kuwaendesha, bado hakuna faida na hasa kama hawatakuwa na furaha na maisha yao.

Hakuna haja ya kusubiri au kuamini ile kauli ya “tutajua mbele”.

Kuamini kinachopatikana leo kinatumika na kesho tutapata tena “kwa uwezo wake Mungu”, kitatumika wakati tunasubiri keshokutwa, si sahihi hata kidogo.

Tungependa kufikia mafanikio ya wenzetu hata robo, basi tukubali hakuna mambo ya kubahatisha kufikia mafanikio hayo badala yake ni mipango madhubuti inayohitaji kutumia ubunifu na hesabu za kutosha na haiwezi kuwa ni jambo rahisi tu.

Tunataka kuwa na klabu bora, pia lazima tukubali kuwa tunaofanya mambo kwa uhakika kwa kuachana na mazoea au tabia za kubahatisha kama hiyo kauli ya “tutajua mbele” badala yake kila kitu kiandikwe na kupangwa mapema kabisa.

Mazoea ni jambo lililotubakiza tulipo kwa miaka mingi sana. Huu ni wakati mzuri viongozi wa klabu kualika wataalamu ambao wataweza kuwapangia bajeti sahihi kulingana na hali halisi.

Kuwaalika wataalamu, itasaidia wao kujua mapema kabisa hata uwezo wa kujiendesha kwa miezi sita na sita baadaye itakuwaje ili kwenda kwa uhakika.

SOURCE: CHAMPIONI 


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV