July 21, 2017




Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Singida United kwa msimu ujao wa ligi akitokea kwa mabingwa wa Ligi, Yanga, hatimaye golikipa mkongwe nchini Ally Mustapha maarufu kama Barthez amewasili jijini Mwanza kujiunga na wachezaji wenzake kwenye kambi inayoendelea jijini humo kwenye viwanja vya Nyamagana na Chuo cha Ualimu cha Butimba.

Barthez aliwasili majira ya saa tatu na nusu asubuhi kwenye uwanja wa Nyamagana  ambapo alipokelewa na katibu mkuu wa Singida United Ndugu Abdulrahman Sima kabla ya kukutana na kocha Hans van der Pluijm na wachezaji wa Singida United walipomaliza mazoezi.

Neno lake la kwanza
“Nina furaha kujiunga na Singida United kwasababu ni timu inayoonekana kuwa itakuja kuleta upinzani kwa Tanzania. Nina matarajio ya kufanya vizuri nikiwa na Singida United kwasababu nakutana na mwalimu ambaye nilikuwa naye Yanga kwahiyo najua tutafanya vizuri”, yalikuwa ni maneno ya Barthez baada ya kuwasili uwanjani hapo.


Barthez amesema kuwa amejiunga na timu hiyo ili kubadilisha mazingira lakini pia akawa na neno kwa mashabiki wa klabu hiyo.

“Nimeamua kutoka Yanga kuja huku ili niweze kubadilisha mazingira na nina Imani nitafanya vizuri kwasababu kuna wachezaji tayari  nawajua.

“Ninapenda kuwaambia mashabiki wa Singida United kuwa waiunge mkono timu yao kwasababu timu inatakiwa kuwa na viongozi , wachezaji na mashabiki pia ambao ni wachezaji wa 12 hivyo watuunge mkono na tukiwa pamoja tutafanya vizuri”, alisema Barthez.

Ujumbe kwa SportPesa
Hata hivyo Barthez alikuwa na neno kwa wadhamini wa klabu hiyo, kampuni ya SportPesa ambao wana mkataba wa mwaka mmoja na klabu hiyo.

“Napenda kuwashukuru SportPesa kwa kile wanachokifanya na tunaheshimu mchango wao kwenye soka letu lakini napena kuwaambia kuwa wazidi kuboresha mambo mengi kwasababu ndio kwanza wameingia nchini kwahiyo kuna mambo mengi ambayo anahitaji kuyaboresha yeye kama mdhamini na nafikiri uwepo wake utafanya mambo yatakaa vizuri tu”, alisema Barthez



Ukongwe
Barthez alisisitiza kuwa watashirikiana vyema na mkongwe mwenzake Nizar Khalfan katika kuhakikisha kuwa Singida United inapaa, lakini hata hivyo hakusita kuzungumzia matarajio yake siku Singida United itakapokutana na Yanga kwenye mechi ya Ligi Kuu.

“Sisi kama wakongwe inabidi tuwasaidia wale ambao ni vijana kwahiyo tunatakiwa kuiongoza timu ili na hawa wengine wafuate na hicho ndicho kinatakiwa.

“Mechi kati ya Yanga na Singida United itakuwa ni ngumu kwasababu Yanga ni timu kubwa na Singida United ni timu ambayo inachipukia hivyo haitakuwa mechi rahisi kwa Yanga eti kwasababu Singida United imepanda daraja. Mechi itakuwa ngumu sana kwasababu Singida United wamesajili vizuri na wana mwalimu mzuri”, alimalizia Barthez.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic