July 24, 2017



Na Saleh Ally
WAKATI Kocha Zdravko Logarusic alipokuwa Simba aliweka wazi kwamba timu waliyokuwa nayo haikuwa ya kuchukua ubingwa abadan. 

Akawataka viongozi kusajili wachezaji ambao wamepevuka, au wazoefu badala ya kujaza vijana wanaochipukia kwa wingi.

Uongozi wa Simba haukukubaliana naye, mwisho ukaamua kumfungashia virago kwa madai ya uzembe. Akaondoka akiwa anasisitiza Simba haitabeba ubingwa.

Miaka mitatu na ushee baadaye, Simba imebeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho baada ya asilimia kubwa ya vijana waliokuwa kikosi cha Logarusic kuonekana wamepevuka kiasi chake.

Lakini sasa Simba imefanya usajili ikiangalia wazoefu zaidi ili iweze kushiriki michuano ya kimataifa kwa ufasaha. Haya ndiyo yale mawazo ya Logarusic yaliyoonekana hayafai wakati ule.
Kocha Arsene Wenger naye mara ya mwisho alibeba ubingwa wa England msimu wa 2003-04. Baada ya hapo wachezaji wengi walianza kuondoka na yeye akashikilia sera ya vijana ambayo imemtesa kwa zaidi ya miaka 10. Mwisho naye ameamua kurejea kwenye ukweli. Tokea msimu wa juzi amekuwa akisajili wachezaji wenye uzoefu au wale wa bei ya juu wanaoweza kusaidia au kuleta mabadiliko. Mwisho, ukweli ulimzidi nguvu licha ya misimamo yake na kuwa na kundi linalomtetea.
Tukirudi katika timu yetu ya taifa, TFF iliamua kutoa nafasi kwa wazalendo, Charles Boniface Mkwasa ambaye alifanya kazi katika presha kubwa. Nasema hivyo kwa kuwa hakulipwa maslahi yake kama mishahara, aliishia kulalamika tu na mwisho kazi ilimshinda kwani hakuna kubwa alilofanya.

Baada ya hapo, TFF ilimteua Salum Mayanga ambaye wengi walianza kumuunga mkono kwa kigezo cha uzalendo, mimi nilipinga kwa kuwa sikuona tofauti ya Mayanga na Mkwasa.

Wakati Tanzania ilipoanza kufanya vizuri katika michuano ya Cosafa ambayo iliishia kushika nafasi ya tatu, watu wengi wakaibuka na kuanza kuwazodoa waliosema Mayanga bado hastahili nafasi hiyo.

Kama unakumbuka, niliandika makala kumpongeza lakini nikasisitiza bado Mayanga kavishwa viatu visivyomtosha na Tanzania haina shida na kushinda Cosafa badala yake inataka michuano ya Chan na Afcon au Kombe la Dunia, hivyo tunataka mtu wa kutufikisha huko.
Nilitoa ushauri wa kwamba kama ni michuano hiyo mingine mikubwa, basi Mayanja anahitaji usaidizi wa juu. Anahitaji kocha mwenye uwezo wa juu ambaye amewahi kuzifundisha timu nyingine za taifa kama Nigeria, Cameroon, Misri na kadhalika kwa lengo la kutumia uzoefu wake kufuzu na Mayanga atabaki kuwa msaidizi ili ajifunze zaidi.

Nilisema siamini Mayanga atatupeleka Chan au Afcon au Kombe la Dunia na kuendelea kumtumia kipindi hiki ni kukubali kupoteza na kusubiri tena na tena bila ya mafanikio.

Waliokuwa wakitetea bila ya kuwa na hoja badala yake wakapeleka maneno makali wako wapi sasa. Huu ndiyo wakati wenu wa kuanza kujifunza, badala ya kuwa na maneno ya mihemko mjifunze kwa hoja na muache ushabiki kwa wa kushangilia bao wakati watu wanajadili hoja za msingi.

Tanzania imetolewa na Rwanda kuwania kufuzu Chan, kwangu naona ni uzembe mwingine mkubwa na kocha anapaswa kuwajibika.

Namjua Mayanga ni mtu mzuri, asiye na matatizo na watu lakini nataka kusema ukweli ili kulisaidia taifa langu. Sitaki kuchotwa na upepo wa wengi eti kisa wamesema wengi basi sina ujanja.

Achaneni na mambo hayo, kuweni imara kunapohitajika ukweli. Tukubaliane, Mayanja anahitaji msaada na ujifunze, kama amewashindwa Rwanda katika Chan, atawaweza vipi Uganda, Cape Verde ambao tunawajua uwezo wetu. Maana kumbuka hata hao Lesotho tulioamini ni wazoefu, nao tulianza nao nyumbani, unakumbuka kilichotokea!



2 COMMENTS:

  1. Saleh Watanzania hawatupendi kitu kinachoitwa ukweli, tunapenda kusifiana hata kwenye ubovu. Bado kama haitoshi tunataka mafanikio bila kuyajenga tukihitaji yaote kama uyoga. Sikupata kuwa na matumaini na timu yetu ya Taifa hata siku moja kwa sababu ni timu inayojengwa kwa mihemko na hamasa na si weledi wala misingi. Wakati wa Marcio Maximo niliyasema hayo na hata sasa nitayasema. Tukiangalia kuanzia wachezaji wetu wanaoteuliwa kwenda timu ya taifa na walio katika klabu zetu takriban zote ukiondoa timu zenye akademi zao wengi hawana utamaduni wa kujua kanuni na misingi ya uchezaji mpira bali kucheza ilmradi.
    Siku tukifahamu kuwa mpira unachezwa kwa malengo, weledi, ufundi na maarifa ndipo tutajua HAMASA na MIHEMKO havina nafasi katika fani.
    Kuwa na kocha mzalendo si tatizo sana lakini je misingi ipo? Joel Bendera alipata sifa (akiwa kocha msaidizi 1980 ikumbukwe baadae alipewa tena timu hiyo na akufanya lolote la maana) lakini watu wamesahau kwamba kizazi cha kina Leonald Tenga, Peter Tino/Godian Mapango RIP, Ahmed Amasha walikuwa na msingi bora toka klabu zao na uchezaji wao wa awali Kama ambavyo Jeff Hudson na makocha wengine wa kigeni na hawa kina Mayanga wasivyoweza kutuvusha na hawatatuvusha. Na jingine ni kwamba inakuwaje kocha anaehitaji mafanikio atumie mchezaji mgonjwa ilhali wazima na wenye uzoefu wapo au kuna rushwa zinaendelea katika soka letu? Nimewasilisha.

    ReplyDelete
  2. He is not a national team coach he is club level coach

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic