July 12, 2017




Na Saleh Ally
UNAWEZA ukawa unajiuliza, una sababu gani ya kwenda Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuishuhudia Everton FC ikiwavaa mabingwa wa SportPesa Super Cup, Gor Mahia.
Mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa ina mambo mengi ya kujifunza kwa kuwa Everton ni timu kubwa nchini England na maarufu barani Ulaya.

Lakini uamuzi wa Wayne Rooney kurejea Everton umefanya kuwe na mengi zaidi ambayo yanamlazimu au kumshawishi mpenda soka yeyote kuitumia nafasi hiyo ya kumuona.
 Binafsi ninaamini Rooney ni kati ya Waingereza wanaojua mpira sana kwa maana ya akili ya haraka, uamuzi, ufundi, kipaji na kadhalika na mengi aliyoyafanya haipingiki.

Rooney ni mmoja wa wachezaji gwiji kabisa wa England katika kizazi hiki kwa kuwa amefanya mengi katika Premier League ambayo ndiyo ligi maarufu zaidi duniani.

Anashuka nchini na akiwa mchezaji pekee aliyewahi kubeba makombe matano ya Ligi Kuu England na huenda akawa ndiye wa kwanza kucheza katika uwanja huo akiwa na idadi hiyo kubwa ya makombe England.

Unaweza ukawa pembeni ya mambo mengi ya nje ya uwanja lakini ukaangalia ufundi wake kuwa ni mmoja wa wachezaji bora kabisa kuwahi kuitumikia Manchester United lakini pia aliyewahi kucheza Ligi Kuu England.

Rooney amefunga mabao zaidi ya 300 lakini kama hiyo haitoshi ana mabao zaidi ya 10 ambayo ni gumzo na yanaendelea kuchuana katika mzunguko wa mabao bora yaliyowahi kufungwa katika ligi hiyo ngumu na maarufu zaidi duniani.

Wabongo wa kwanza:
Wakati ukimuangalia jifunze unamuangalia mchezaji wa aina gani huku mashabiki wa Tanzania watakaohudhuria katika Uwanja wa Taifa hiyo kesho wakiwa na bahati ya kuwa mashabiki wa kwanza duniani kote kumuona Rooney akiichezea Everton kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga nayo akirejea kutokea Manchester United.



Mashabiki wa Tanzania pia watakuwa wa kwanza kumuona Rooney akiwa katika jezi ya Everton baada ya miaka 13 ya kuonekana katika jezi ya Mashetani Wekundu wa Old Trafford.

Jezi mpya:
Wakati wanamshuhudia Rooney akiichezea Everton kwa mara ya kwanza, shabiki yeyote atakayekwenda Taifa atakuwa wa kwanza kuishuhudia Everton ikiwa imetinga jezi zake mpya za ugenini kwa ajili ya msimu wa 2017-18.
Everton imezitangaza jezi hizo jana lakini kwa mara ya kwanza zinavaliwa katika mechi ya kesho na itakaporejea Ligi Kuu England, kwa mara ya kwanza itazivaa katika mechi dhidi ya Manchester City Agosti 21, mwaka huu.

Rooney biashara:
Rooney atakuwa uwanjani lakini nikukumbushe alivyowahi kuwa biashara kwelikweli na bado thamani yake ipo juu.
Julai 2011, Rooney alishika namba moja ya vifaa vinavyomhusu kuwa na mauzo ya juu sana.

Katika msimu wa 2009-10, Manchester United iliuza kati ya jezi milioni 1.2 hadi milioni 1.5 za Rooney duniani kote na kumfanya kuwa mchezaji aliyeuza zaidi jezi zenye jina lake.


Kigogo mtandaoni:
Oktoba 2014, alikuwa mwanamichezo wa kwanza kufikisha watu milioni moja wanaomfuatilia.

Hata hivyo, amekuwa akiendelea kushuka kwa kuwa kuna wengine wanapata watu wengi kama Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na wengine kadhaa lakini ameendelea kuwa mmoja wa wanamichezo wanaofuatiliwa zaidi mtandaoni au wanaokubalika zaidi mtandaoni.

Alishitakiwa na Moyes:
Mwaka 2008, kocha aliyemkuza ni David Moyes lakini kocha huyohuyo ndiye aliyewahi kumfungulia Rooney mashitaka mahakamani akimtuhumu kumuandika kwamba alivujisha uhamisho wake kwenda Manchester United.

Rooney aliandika hayo katika kitabu kilichokuwa kinaelezea maisha yake. Jambo hilo lilimkera Moyes akafungua kesi ya madai ambayo ilianza kusikilizwa lakini baadaye walimaliza mambo yao nje ya mahakama na inaelezwa kocha huyo alilipwa kitita cha pauni 500,000.

Mechi ya 68:
Katika mechi ya kesho, Rooney atakuwa anaichezea Everton mechi ya 68 katika maisha yake na akifunga bao litakuwa ni la 16.

Kabla ya kuondoka Everton mwaka 2004 na kujiunga na Manchester United chini ya Alex Ferguson, Rooney tayari aliichezea Everton mechi 67 na kufunga mabao 15.


Timu mbili:
Alianza kucheza Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza mwaka 2002 akiwa na Everton na baada ya hapo alihamia Manchester United.

Baada ya hapo amerejea tena Everton, hivyo kumfanya katika miaka 15, Rooney amecheza mechi zaidi ya 400 lakini akiwa na timu mbili pekee.

Everton milele:
Rooney amekuwa shabiki wa Everton milele na mara zote amekuwa akitumia kauli ya “If you are Blue, you are Blue forever”. Ikiwa ni msisitizo wa kuonyesha kama ukiwa shabiki wa Everton, basi wewe ni milele na kamwe hauwezi kubadilika.

Mara nyingi, Rooney amekuwa akimtumia mwanaye Kai kuonyesha yeye ni Everton milele. Kwani Kai amekuwa akivaa jezi za Everton licha ya baba yake kuendelea kuichezea Manchester United.

Kakataa mamilioni:
Rooney ameonyesha mapenzi yanavyoweza kuzidi mamilioni ya fedha baada ya kukataa mabilioni ya dola ambayo angepata kama angekubali kwenda Marekani au China.

Lakini mapenzi yake kwa Everton, ameamua kubaki England ingawa imeelezwa angependa watoto wake kuendelea kuishi nchini England na bahati nzuri wanarejea jijini Liverpool ambako amezaliwa.

Mnazi zaidi:
Wakati wakisoma katika shule ya Msingi ya Our Lady and Swithin akiwa na ndugu zake wawili, John na Graham, Rooney ndiye alikuwa mnazi zaidi wa Everton.

Inaelezwa, hakutaka kusikia mtu akiizungumzia vibaya Everton na alikuwa tayari kuzichapa ili kulinda jina la timu hiyo ambayo sasa amerejea na kuanza kuitumikia tena.

Haipendi Liverpool:
Rooney na familia yake yote, hawaipendi Liverpool kama mpinzani mkubwa na ndiyo timu wamekuwa wakiiombea ifanye vibaya kuliko nyingine zote.
Rooney amekuwa na furaha kubwa kuifunga Liverpool na ilionekana kila alipoifunga akiwa Man United, aliiona ni kama ameifunga kwa mujibu wa Everton!

Hat trick kwanza:
Akiwa anacheza mechi yake ya kwanza leo kwa mara nyingine baada ya kurejea Everton, je, anaweza kufanya maajabu ya kufunga hat trick kama alivyofanya baada ya kujiunga na Man United?

Septemba 28, 2004 alipojiunga na Manchester United akitokea Everton, Rooney alipangwa katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Fenerbahce ya Uturuki na mwisho United wakashinda kwa mabao 6-2, Rooney akiwa amepiga hat trick na kutoa asisti moja.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic