July 10, 2017



Na Saleh Ally
MPIRA ndio mchezo unaopendwa zaidi Tanzania lakini tumekuwa hatuna bahati nao kwa kuwa maandalizi yetu kwa asilimia 95 yanakuwa si mafunzo bora na zaidi ni vipaji.

Si vibaya kusema Alhamisi hii, Watanzania watapata bahati kuiona Everton ikiwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa SportPesa Super Cup.

Wakati wanakwenda kucheza mechi hiyo tena kwa kiingilio cha chini cha Sh 3,000, huenda wengi wangeweka mjadala wa kuwa kama si Arsenal au Man United basi wasingeenda uwanjani.

Msimu uliopita wa Premier League, Everton ilimaliza katika nafasi ya 7, nyuma ya Manchester United iliyokuwa nafasi ya 6. Hii ni sehemu ya kukuonyesha ni timu kubwa na itakuwa na mengi ya kujifunza.

Everton imefanya usajili mkubwa kuwanasa wachezaji mbalimbali kama Davy Klaassen kutoka Ajax, Sandro Ramirez kutoka Malaga na beki kisiki wa Sunderland, Michael Keane lakini pia zaidi ya wachezaji wanne.



Imepania kujiimarisha na kuhakikisha inawapiku wapinzani wake wakuu Liverpool lakini kufanya zaidi na kupata nafasi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Soka ni furaha lakini kwa mdau wa soka ukifika uwanjani na kuishuhudia mechi hiyo kwa umakini mkubwa, lazima utajifunza jambo au mambo na ikawa faida. Mfano angalia wachezaji hawa watatu kabla ya wengine wengine walio katika kikosi hicho.

Wachezaji wapya

Keane:
Keane ambaye ana ‘clean sheet’ 10, yaani mechi bila ya kufungwa huku akiwa ameokoa mara 260 na hana hata kosa moja lililosababisha timu yake kufungwa bao.

Uwezo wa Keane kulala na kuokoa ni 86% lakini utaona ‘fitness’ yake iko juu kwa kuwa amecheza mechi 35 kati za Ligi Kuu England. Huyu ni mchezaji ambaye beki yeyote wa kati angependa kujifunza jambo kwake.

Kwa wachezaji kama wa hapa nyumbani, lingekuwa jambo zuri kwenda kujifunza na kumuona uchezaji wake kuwa ni mtu wa aina gani na beki wa kati anaweza kucheza vipi na kuwa bora.

Kinachovutia zaidi kuna tofauti kubwa unapomuona Keane akicheza kwenye moja ya viwanja vya England na wewe ukawa unamshuhudia. Sasa atakuwa anacheza kwenye Uwanja wa Taifa, eneo ambalo ni nyumbani na mabeki wetu wa hapa nyumbani wamekuwa wanalitumia.

Sandro Ramirez:
Kisoka amekulia FC Barcelona hadi kufikia kuaminika kuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania. Hili si jambo dogo kwa mchezaji yeyote. Bado hajapata namba ya uhakika lakini ni mchezaji anayetaka kufanya vema na kuchukua nafasi ya juu zaidi.

Msimu uliopita, alionyesha cheche zake akiwa na Malaga. Alicheza dakika 2,316 akiwa ameanza na kuingia jumla ya mechi 28 na kufanikiwa kufunga mabao 14, pia katoa pasi tatu zilizozaa mabao, uwezo wake wa pasi zinazofika ni 79%.

Sandro anataka kufunga zaidi, anataka kufanya zaidi na sasa ametua England ambako angependa kuonyesha uwezo wake zaidi na anajua kuna ushindani mkubwa zaidi.

Huyu atatoa somo pia kwa washambulizi katika mambo mengi. Mfano, ‘position’ sahihi ambayo inatakiwa kwa mshambulizi au wakati gani anatakiwa kupiga shuti na anatumiaje miguu yake. Mfano anapokuwa katika rundo la mabeki au katika nafasi iliyo wazi.

Jifunze pia kuangalia wachezaji wanapokuwa wanasubiri faulo, wachezaji hasa wenye maumbo makubwa kama Sandro wanakaa katika nafasi ipi.

Klaassen:
Klaassen kwa muonekano ni kama mtu mzima hivi lakini uhalisia ana miaka 24 na alitoa mchango mkubwa kuifikisha Ajax fainali ya Europa League.

Kacheza mechi 33 msimu uliopita akiwa na jumla ya dakika 2851 na kafunga mabao 14 ikiwa na maana ni mshambuliaji mwingine aina ya Ramirez na kwa kuwa umri unamruhusu, ana nafasi ya kufanya vizuri zaidi.

Utaona tayari ana uzoefu na michuano ya kimataifa lakini ana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri zaidi kwa kuwa Everton ni klabu inayotaka kubadili njia.

Jiulize, bahati gani kumuona mshambulizi ambaye msimu uliopita tu amecheza fainali ya michuano ya Europa League. Maana yake kwa wale wanaopendelea nafasi ya ushambulizi watakuwa na nafasi ya kujifunza.

Mshambuliaji huyo anaweza hata kuwafunza makocha wa timu kadhaa ambao watakuwa uwanjani na kujiuliza nini wafanye au wawape ni washambulizi wao.


Ingewezekana ingekuwa ni kitu maalum, basi timu zingeandaa utaratibu wa kwenda uwanjani pamoja na kukaa. Zikaangalia mechi pamoja na baadaye kujifunza jambo fulani. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic