August 18, 2017


Na Saleh Ally
NIMEKUWA na kawaida ya kufuatilia wachezaji wa kigeni hasa ninaposikia wanataka kusajiliwa na timu za Tanzania.

Mara nyingi nafanya hivyo kwa mambo matatu muhimu. Kwa kuwa ninaamini mimi ni Mtanzania na ninapaswa kukizungumzia kwa kukiweka sawa, kukisifia au kukikosoa kile naona kinakuwa si maslahi ya nchi yangu.

Jambo la kwanza ambalo hunifanya nifuatilie ni kuona kama mchezaji anayekuja kucheza nchini kweli atakuwa na faida na mpira wa hapa nyumbani.

Mfano, huyo mchezaji akija, wachezaji wa hapa nyumbani watakuwa na nafasi ya kujifunza kupitia yeye. Yaani anaweza kuwa changamoto ya kuwafanya wao waamke na kumuona mfano au mshindani.

Pili ni suala la huduma atakayopewa na hudumu atakayotoa kwa timu yake. Mfano apewe nyumba nzuri au usafiri huku wachezaji wa Kitanzania wakiwa hawapati hivyo na mchango wake ukawa chini kuliko Watanzania. Sitanyamaza.

Tatu na mwisho, malipo yake hasa mshahara na usajili. Fedha atakazolipwa anastahili, kwani kama hastahili basi bora wapate Watanzania ambao ni Watanzania wenzangu hasa kwa wale watakaokuwa na kiwango bora kuliko mgeni huyo.

Mara nyingi nimeshauri mgeni akiwa na kiwango hata sawa na Watanzania wengine, basi hastahili kuja kucheza hapa kwa kuwa anapaswa kuwa mchezaji mwenye kiwango cha juu zaidi ili kutimiza mengi yakiwemo hayo niliyoyataja. Timu itakayomsajili itaangalia zaidi suala la faida kama mchezaji uwanjani. Mimi kama Mtanzania, naangalia mengi zaidi kwa kuwa timu hiyo ni mali ya Watanzania. Kumbuka hakuna timu inayoshiriki ligi yoyote ya Tanzania na si mali ya Watanzania.

Wakati naangalia hayo yote, nimemfuatilia kwa karibu sana mchezaji Nicolas Gyan raia wa Ghana ambaye amesajiliwa na Simba.

Gyan aliyekuwa akikipiga katika timu ya Ebusua Dwarfs ya Ghana na kufunga mabao 11 katika Ligi Kuu Ghana msimu uliopita. Tayari ameichezea Simba mechi ya kirafiki dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.

Wakati namuangalia katika mechi dhidi ya Rayon Sports, nilitaka kupata uhakika wa kile ambacho nilikiona kwenye video zake wakati Simba ikitangaza kuwa ina nia ya kumsajili. Mechi hiyo ya Dar es Salaam, haikuwa ya muda mrefu sana kwake kwa kuwa aliingia.

Lakini naamini watu wachache sana walimfuatilia kwa kuwa akili ilikuwa kwa wale wachezaji maarufu kama Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, John Bocco, Aishi Manula na kadhalika.

Huyu Mghana si maarufu Tanzania wala Afrika Mashariki. Watu hawawezi kuwa na ‘mzuka’ naye. Lakini mimi nikajikita kumfuatilia kutaka kuona kile alichokuja nacho. Nikajiridhisha.

Nimejiridhisha kuwa huyu Gyan ni mtu anayejua mpira kweli na umri wake hajafikisha hata miaka 25. Maana yake Simba ina faida kubwa na kwangu naona kama ataendelea kama alivyokuja na kuongeza zaidi, ninaamini kabisa atakuwa tegemeo la Simba na huenda akawa maarufu zaidi ya Okwi.

Niliona mambo kadhaa kwake wakati akicheza dakika chache dhidi ya Rayon Sports, ukipata nafasi unaweza kuiangalia tena mechi hiyo runingani.

Hata kidogo, Gyan hakucheza kuwafurahisha mashabiki. Badala yake, zaidi alifanya kinachotakiwa kufanywa na mchezaji mwenye malengo na anayejali zaidi kuona timu inafanikiwa kile inachokitaka.

Katika kila mpira aliogusa, alifanya kilichotakiwa. Mfano; mpira uliotakiwa kutolewa haraka, alifanya hivyo. Pasi fupi au ndefu alifanya hivyo na ana uwezo mkubwa sana wa kubadilisha mchezo kama ambavyo hufanya Niyonzima lakini yeye ana kasi zaidi.

Uwezo mkubwa wa kutafuta nafasi anapokuwa hana mpira. Hili ni jambo linawashinda wachezaji wengi wa Kitanzania na wanaotokea Afrika Mashariki na huenda ni athari ya kutopitia katika akademi wakati wanajifunza.

Lakini kujiamini kwa Gyan ni kwa juu sana. Mchezaji ambaye anapokuwa na mpira hahitaji kuinama kuuangalia mpira na hana hofu hata beki anapomsogelea.
Kikubwa zaidi ni ‘touch’, namna anavyoupokea mpira, kuukokota na kuutoa. Inakuonyesha ni mchezaji wa aina tofauti kabisa na wengi tulionao.

Huenda Kocha Joseph Omog atakuwa na kazi kubwa ya kupanga kikosi chake. Lakini ningepewa nafasi ya kumshauri, basi ningemuambia kuangalia zaidi uwezo ndiyo atoe nafasi na si majina kwa ajili ya kuwafurahisha mabosi na mashabiki.

Bado nina imani kubwa, Gyan anaweza kuwa funzo kwa wachezaji wetu hata kama nilimuona akicheza dakika chache. Tuache ligi ianze, tuone lakini maneno yangu, ninaamini hayataanguka.



1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic