August 25, 2017



NA SALEH ALLY
UKIANGALIA mashabiki waliojitokeza katika mechi ya Ngao ya Jamii, wale wa Simba walikuwa ni wengi zaidi ya wale wa Yanga ambao pamoja na kujitokeza wachache, walionekana ni wanyonge.

Mashabiki wa Yanga, walionekana ni kama ambao hawakuwa wakijiamini sana hasa kabla ya mchezo. Walikuwa watulivu na ambao walionyesha hawakuwa wakiamini walichokifuata pale Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam hiyo juzi, kingewapa furaha.

Upande wa pili, yaani wenzao wa Simba walionekana kujiamini, walikuwa na uhakika wa furaha na walijua kwa hali ilivyo, Yanga hawatatoka na muda mwingi waliimba nyimbo za kuwadhihaki watani wao kwamba kama wangefungwa mabao machache basi saba ilikuwa ni saizi yao.

Mwisho mechi iliisha kwa Simba kushinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 za bila bao katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii! Hapo sasa ndipo tunarudi kukumbushana kuhusiana na mpira, kuwa si kitu cha kila mmoja wetu anavyoamini au kufikiria, ndivyo inakuwa.

Niliwahi kuandika makala na kuwaeleza mashabiki wa Simba kwamba wanapaswa kukumbuka uongozi wao umejitahidi kusajili timu nzuri na wachezaji wengi ni wale wanaowajua, lakini wajue wao si malaika.

Niliwaeleza kwamba wachezaji waliosajiliwa si wanaotokea Madrid, Manchester United, Barcelona, Bayern Munich, PSG na kadhalika. Tena nikawakumbusha kwamba hata wachezaji wa timu ambazo nimezitaja wamekuwa wakikosea na wamekuwa wakicheza mechi na kufungwa.

Mara nyingi, mashabiki huanzisha mambo na mwisho huangusha mzigo kwa vyombo vya habari kwamba vimewaponza kuamini tofauti. Hata mimi ninachokiandika kuwakumbusha ni kwenye vyombo hivyohivyo vya habari kwamba mpira huamuliwa uwanjani baada ya dakika 90 na si maneno ya kila anayeamini.

Nilikuwa nikishangazwa na shabiki anayeonyesha kweli kwamba anajiamini timu yake itashinda saba na kama ni chache basi zitakuwa ni tano. Ukimuuliza atasema Simba imemsajili Emmanuel Okwi, John Bocco, Aishi Manula na kadhalika. Utaona ni wachezaji ambao wamecheza mara nyingi na Yanga na wanaijua, inawajua.

Kuna wale waliotaka kuwaaminisha Yanga imesajili vibaya sana. Usajili wao si mzuri na kikosi ni kibovu kabisa, lakini ukiangalia waliochukua ubingwa mfululizo wakiwa na Yanga, hata sasa waliomo ni asilimia 80 au zaidi. Sasa vipi ghafla wageuke na kuwa wabovu? Au vipi siku chache waonekane hawawezi kabisa na watafungwa saba?

Simba kweli imesajili vizuri lakini wamesajili idadi kubwa ya wachezaji ambao sasa ndiyo wanaanza kutengeneza timu ili kupata kikosi wanachokitaka. Lazima wahitaji muda kutokana na namna wanavyoshirikiana kila kukicha ili kujenga kikosi sahihi kwa ajili ya kuwapigania.

Mechi ya Ngao ya Jamii imeisha kwa sare ya bila bao kwa dakika 90. Mashabiki sasa wanalalamika, kwamba Kocha Joseph Omog hajui kupanga kikosi kwa kuwa wana kikosi kipana sana. Sasa walitaka Simba ichezeshe wachezaji 14 kwa kuwa wana kikosi kipana!

Leo mashabiki wanaamini wanajua zaidi kupanga kikosi kuliko kocha mwenyewe? Nafikiri ni kutengeneza mazingira ya kutaka kuonyesha wanajua sana jambo ambalo si sahihi pia. Simba imesajili timu nzuri, inaweza kushinda, sare au kufungwa pia.

Kuanza kujenga hisia kwamba Simba haifungiki wakati haijacheza mechi ukaiona au haijacheza mechi na kutengeneza takwimu sahihi ni kosa kubwa.

Mashabiki wa Simba lazima wajue timu yao ni ya mpira. Kweli inaweza kuwa bora lakini itaonyesha ubora huo uwanjani na matokeo yapatikane uwanjani. Kusema gazeti lilisema kasajiliwa mchezaji mzuri, kweli anaweza kuwa mzuri lakini haina maana kila akicheza lazima afunge.


Wakati mwingine, mchezo hasa wa soka, unaendeshwa na asili yake ambayo ni hakuna anayeweza kufanya vizuri bila kujituma, lakini hakuna mwenye ubora wa milele hata kama ni bora sana. Hivyo niwasisitize, kwenda uwanjani na matokeo mfukoni ni kutengeneza maumivu ya baadaye.

SOURCE: CHAMPIONI

4 COMMENTS:

  1. Ali Saleh happ unaonyesha udhaifu wako kiuandishi. Hamna shabiki yeyote anayetegemea miujiza. Hizo ni fikra zako. Matokeo ya mechi ni kushinda kufungwa na sare. Piga debe kwa hao unaowajenga. Timu ya Simba imefanya usajili kwa mahitaji yao. Hamna yeyote aliyesema tumesajili malaika.Malaika hawachezi mpira huo mfano wako ni dhaifu kwa calibre ya mwandishi kama wewe.Simba imeshinda kwa penalti ingefungwa ungebeba bango.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Acha kukurupuka na kukosoa bila research sijaona Ali Saleh anakokurupuka. Na naamini wewe ni mmoja wa waliokuwa wanaamini hivyo lkn unahasira kwanini Simba hawakushinda. Jifunze kutokana na wengine sio kukurupuka. Salehjembe keep it up endelea kusema ukweli wachache kama hawa wasiojielewa wasikurudishe nyuma

      Delete
  2. Unaishi sayari ipi?Ngao kachukua nani?Aliyeshinda nani?Penalti tano zinaamua hata kombe la dunia. Huwezi kuwalaumu wapenzi kwa kuiamini timu yao.Mashabiki wa Yanga walikuwa wanyonge kwa sababu hawaiamini timu yao.Confidence ni muhimu sana kwenye football. Aliyekosolewa ni Ally Saleh.Punda wa nyuma kachapwa wewe punda wa mbele yowe la nini?

    ReplyDelete
  3. Simba alishinda hata kama ni kwa penalties.Yanga angekuwa bora angeifunga Simba ndani ya dk.90.Msitumainishe Yanga ina timu nzuri sana wakati tukirudia takwimu za nyuma ktk mechi nne zilizopita Yanga haimjafunga Simba. Mashabiki wa Yanga walikuwa wanyonge ni kwa sababu ya Niyonzima kuvaa jezi nyekundu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic