September 21, 2017






Kuna rekodi moja ya Bundesliga inayoziunganisha Borussia zote yaani Monchengladbach na Dortmund.

Wakiwa wanajiandaa kukutana katika dimba la Signal Iduna Park katika mechi kali ya wiki hii Siku ya Jumamosi, kitu cha uhakika ni kwamba rekodi hiyo haitavunjwa.

Kwenye mechi ya mwisho wa msimu wa 1977/8, Monchengladbach waliingia uwanjani wakiwa na idadi sawa ya point na Cologne, lakini wakiwa nyuma kwa tofauti ya magoli 10 nyuma ya wapinzani wao ambao walikuwa wanatazamia kushinda kirahisi mchezo wao dhidi ya St Pauli.

Kwenye mchezo uliolalia upande mmoja zaidi katika historia ya Bundesliga, Monchengladbach walifunga mabao sita katika kila dakika 45 za mchezo bila majibu hivyo kupelekea matokeo ya 12-0 baada ya kipenga cha mwisho kulia. Ikiwa ni rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa ndani ya Bundesliga.

Tangu kipindi hicho Monchengladbach hawajakaribia hata kidogo kushinda ubingwa wao wa sita huku wapinzani wao wakishinda Ubingwa huo mara tano na kuwa ndio hasimu mkubwa wa Bayern Munich.

Japokuwa idadi ya zaidi ya watu 80,000 hawatarajii kuona rekodi ya mabao 12 ikivunjwa, wanaweza kutazamia mchezo ambao bado utakuwa na mabao mengi ukizingatia timu hizi zina uwezo mzuri wa kushambulia na soka la kuvutia. Michezo 5 ya nyuma waliyokutana umeshuhudia angalau idadi ya magoli manne kwenye kila mchezo.

Mfungaji bora wa msimu uliopita Pierre Emerick Aubameyang ameendelea kutikisa nyavu bila wasi, huku Monchengladbach wakiwa na vijana machachari Lars Stindl na Thorgan Hazard, ambao wanachezea timu za taifa, Ujerumani na Ubelgiji.

Mchezo huu pia utakuwa ni kwanza kwa kiungo Mahmoud Dahoud kukutana na timu yake ya zamani tangu alipojiunga na Dortmund majira ya joto. Nafasi yake katika kikosi cha Monchengladbach imejazwa na kinda kutoka Uswizi Denis Zakaria ambaye amepata sifa kedekede kutoka kwa kocha wake.

“Ni burudani unapomtazama Denis namna alivyozoea. Hakika ameshatulia ndani ya Bundesliga”, Kocha wa Monchengladbach Dieter Hecking alisema, “Lakini sasa anahitaji kuendelea kucheza vizuri bila kuonyeshwa kadi”, aliongeza.

Watazamaji kote nchini wataweza kutazama mchezo huu MUBASHARA kupitia Chaneli ya World Football Saa 1:30 Usiku Jumamosi hii.

Hii ni moja kati ya mechi zinazofanya Bundesliga iwe na mvuto wa kipekee na pia nafasi kwa waafrika kumtazama muafrika mwenzetu Aubameyang ambaye ni kinara ndani ya timu ya Dortmund. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic