Hatimaye kampuni ya kubashiri matokeo, ya Sportpesa ya nchini Kenya, rasmi imetua jijini Dar kuidhamini klabu kongwe ya Yanga.
Kampuni hiyo itaidhamini Yanga baada ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyokuwa yakifanyika kati ya klabu hiyo na uongozi wa Sportpesa.
Sportpesa, tofauti na Yanga, pia ilikuwa kwenye mazungumzo na vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba ambao nao wanatarajiwa kuingia nao makubaliano.
Kwa mujibu wa mtandao mmoja wa nchini Kenya, kampuni hiyo imetua nchini kwa ajili ya kuzindua matawi yake Tanzania na uzinduzi unatarajiwa kufanyika Mei 9, mwaka huu kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, iliyopo Kivukoni jijini Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa pamoja na kuzindua matawi, pia Sportpesa itapata nafasi ya kukutana na viongozi wa Yanga kwa ajili ya kufanya nao mazungumzo ya mwisho kabla ya kuingia mkataba.
“Kwa heshima na taadhima mnaalikwa katika uzinduzi wa Sportpesa Tanzania Jumanne ya Mei 9, 2017 katika Ukumbi wa Kibo Ballroom kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, Barabara ya Kivukoni,” ilisomeka taarifa kutoka katika mtandao huo.
Sportpesa wanakuja Tanzania kuzindua matawi yao, baada ya kuwa katika uwezekano wa kuidhamini Yanga. Wanaamini kwa kuidhamini Yanga watapata wateja wengi katika soko la Tanzania.
Wakenya hao tayari ni wadhamini wa Hull City inayoshiriki Ligi Kuu ya England, Gor Mahia, AFC Leopards zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya, pamoja na klabu nyingine kadhaa katika soka la Kenya.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa kuzungumzia hilo, alisema: “Yapo mazungumzo yaliyokuwa yanafanyika kati yetu na kampuni ambayo yalienda vizuri, hivyo kwa kifupi tusubirie kidogo hadi mambo yakikamilika tutaweka wazi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment