MWAKA 1998, ulikuwa na mafanikio makubwa sana kwake. Katika msimu wake wa kwanza akiwa na Arsenal, anafanikiwa kubeba mataji mawili kwa mpigo, Ligi Kuu England (Premier) na Kombe la FA, anamaliza msimu na kujiunga na Ufaransa katika Kombe la Dunia ambako pia anabeba Kombe la Dunia 1998. Maisha yanakuwa matamu, yenye raha mustarehe kwa kiungo fundi Emmanuel Laurent Petit.
Katika maisha yake yote, hakuna mwaka ambao umekuwa na mafanikio makubwa kwake kisoka, kama 1998. Huu ulikuwa ni mwaka wake, dunia ilimzungumza, mashabiki walimuimba, alipata mafanikio makubwa na hadi anastaafu soka, hayakuwahi kujirudia.
Petit, aliyezaliwa Septemba 22, 1970, kabla hajatua Arsenal, alitokea kutwaa taji la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) akiwa nahodha wa Monaco mwaka 1997. Monaco hiyo iliyotwaa ubingwa ambayo Petit alitokea, ilikuwa na vichwa kama Fabien Barthez, Gilles Grimandi (ambaye alijiunga Arsenal mwaka mmoja na Petit), Victor Ikpeba, huku ikiwa na makinda ambao walikuja kuiteka dunia akina Thierry Henry na David Trezeguet.
Anapotua Arsenal, Wenger ambaye alikuwa kocha wake wa zamani Monaco, anambadilisha kutoka kwenye kiungo wa kati hadi kuwa kiungo mkabaji akicheza kwa kuelewana vizuri na Mfaransa mwenzake, Patrick Vieira na kuifanya Arsenal isishikike msimu huo wa 1997-98 walipopata mafanikio hayo.
Aliikuta Arsenal ikiwa ina watu kama kina Ray Parlour, Marc Overmars, mastraika Dennis Bergkamp, Ian Wright na Nicolas Anelka ambao Wenger alikuwa anawachezesha kwa kupokezana.
Petit, 46, aliichezea Arsenal kwa misimu mitatu ambapo alicheza jumla ya mechi 118 na kufunga mabao 11, likiwemo bonge la bao la shuti nje ya 18 dhidi ya Derby County ambalo lilikuwa bao la ushindi, msimu wa 1997-98.
Katika timu ya taifa ya Ufaransa, nako Petit ameacha alama, akicheza katika michuano miwili ya Kombe la Dunia na miwili ya Ulaya (Euro). Wengi wanakumbuka bao lake la tatu alilofunga katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Brazil kwenye fainali ya Kombe la Dunia 1998, pia alikuwemo katika kikosi kilichoshinda Euro 2000. Kwa jumla, aliichezea mechi 63 na kufunga mabao sita. Aliichezea kwa miaka 13, kuanzia 1990 hadi 2003.
Mwaka 2000, Barcelona ilimtamani Petit na ikafanikiwa kumshawishi, ikamsajili yeye na mwenzake Marc Overmars lakini klabuni hapo alijikuta akichezeshwa kama beki, baadaye akapata majeraha na kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza. Katika kitabu chake alichokichapisha mwaka 2008, kiungo huyo alitenga sura nzima kwa ajili ya kuzungumzia maisha yake Barca ambapo alieleza kuwa kocha Lorenzo Serra Ferrer aliua kiwango chake kwani hakujua hata Petit anacheza nafasi gani wakati alipojiunga. Aliondoka hapo kwa aibu akiwa amefunga bao moja tu.
Alitua Chelsea mwaka 2001 ambako alikutana na msimu mgumu, akacheza katika fainali ya Kombe la FA ambapo walifungwa na timu yake ya zamani, Arsenal ambayo ilibeba makombe mawili tena, likiwemo la Premier.
Kwa ujumla hakuwa na mwenendo mzuri Chelsea kutokana na majeraha, hasa baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti. Baada ya kutoswa na timu hiyo mwishoni mwa msimu wa 2003-04, Petit aligomea nafasi ya kusajiliwa Bolton Wanderers, na akatangaza kutundika daruga Januari 20, 2005 kutokana na kushindwa kupona kikamilifu goti. Alistaafu akiwa na umri wa miaka 35.
KLABU ALIZOCHEZEA
Mwaka klabu mechi mabao
1988–1997 Monaco 292 5
1997–2000 Arsenal 116 11
2000–2001 Barcelona 38 1
2001–2004 Chelsea 76 3
Jumla 522 20
MATAJI
Monaco
Ligue 1 (1): 1996–97
Coupe de France (1): 1990-91
Arsenal
Premier League (1): 1997–98
FA Cup (1): 1997–98
Ngao ya Jamii (2): 1998, 1999
Ufaransa
Kombe la Dunia (1): 1998
Euro (1): 2000
Tuzo Binafsi
Mchezaji Bora wa Mwezi Premier (1): Aprili 1998
Kuingia kwenye Timu Bora ya Mwaka Premier (1): 1998-99
MAISHA BINAFSI
Petit alimuoa muigizaji Mfaransa, Agathe de La Fontaine mwaka 2000, lakini baada ya miaka miwili akampa talaka wakiwa na mtoto mmoja, Zoe. Sasa anatoka kimapenzi na mrembo Maria Servello, ambaye wana mtoto mmoja, Violet, aliyepatikana mwaka 2007.
Kaka yake Petit, Olivier, alikuwa mwanasoka, lakini wakati akiichezea Arques mwaka 1988, alianguka ghafla uwanjani lakini alipokimbizwa hospitalini ikabainika kuwa ameshafariki dunia baada ya damu kuganda kwenye ubongo. Katika kitabu chake, Petit aliandika kuwa, tukio hilo lilimshtua kiasi kwamba kidogo aachane na soka.
Julai 1998, Petit alishinda bahati nasibu ya pauni 17,000 (kwa sasa karibu 50m) lakini zote akazitoa kwa masikini. Namba yake ya jezi kwenye klabu zote ilikuwa 17.
ANACHOKIFANYA KWA SASA
Petit hivi sasa ni mchambuzi wa soka katika vituo vya televisheni. Mara nyingi amekuwa akionekana katika kituo cha televisheni cha French TV.
0 COMMENTS:
Post a Comment