October 20, 2017



Raundi ya sita ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeondoka na Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja hii ikiwa ni siku chache baada ya Simba kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Wakati Mayanja anaondoka, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara raundi ya 7, inatarajia kuendelea kesho Jumamosi baada ya mchezo wa Mwadui FC dhidi ya Kagera Sugar iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.

Timu hizo zinakutana katika Raundi ya Saba katika duru hili la kwanza la VPL ambalo mbali ya Kampuni ya Simu ya Vodacom - wadhamini wakuu, wadhamini wengine ni Kituo cha Televisheni cha Azam (Azam Tv) na Benki ya KCB ambayo huduma zake za kibenki zinazidi kushamiri nchini.

Wadhamini hao wanachagiza ligi hiyo ambayo itaendelea Jumamosi Oktoba 21 kwa michezo sita  itakayofanyika kwenye viwanja tofauti huku mechi nyingi zikipata fursa ya kuonyeshwa kwenye chaneli mbalimbali za Azam Tv kupitia king’amuzi cha Azam.

Michezo ya Jumamosi itakutanisha timu za Mbao na Azam kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, wakati Lipuli itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa ilihali Ruvu Shooting watakuwa wageni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumamosi hiyo hiyo Simba yenye mabadiliko kidogo kwenye benchi la Ufundi, itawaalika Njombe Mji kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku Ndanda ikicheza na Singida United kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Wakati Jumamosi hiyohiyo tena, Mtibwa Sugar wakicheza na Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Manungu mkoani Morogoro, Jumapili kutakuwa na mchezo mmoja tu - ambao ni kati ya Stand United na mabingwa watetezi, Young Africans ya Dar es Salaam - mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic