October 11, 2017



Na Saleh Ally
WAKATI tayari nchi 17 kati ya 32 zinazotakiwa kufuzu Kombe la Dunia zimeshajulikana, gumzo wala si kina nani watapata nafasi hiyo kukamilisha idadi hiyo ya 32.

Gumzo la sasa ni kufuzu kwa timu ya taifa ya Iceland kucheza Kombe la Dunia, michuano mikubwa zaidi ya soka ambayo safari hii itafanyika mwakani nchini Urusi.

Iceland imekuwa gumzo baada ya kufuzu Kombe la Dunia kutokana na ushindi wao wa mabao 2-0 dhidi ya Kosovo na sasa wanaendelea kuishangaza dunia.

Ushindi huo unawapeleka Urusi na mara moja wanaamka na kuandika rekodi ya kuwa nchi yenye wakazi takriban 350,000 tu kufuzu michuano hiyo.

Mara ya mwisho, nchi iliyokuwa na wakazi wachache zaidi kuwahi kufanikiwa kucheza Kombe la Dunia ilikuwa ni Trinidad & Tobago yenye wakati wapatao takriban milioni 1.3.

Kwa mnaojua Trinidad & Tobago, ni nchi iliyokuwa ikiongozwa na nyota wa Manchester United, Dwight Yorke katika Kombe la Dunia mwaka 2006.

Sasa ni Iceland, nchi yenye wakazi wapatao 350,000, angalau wanaweza kuwa takriban sawa na wakazi wa kitongoji maarufu cha Sinza jijini Dar es Salaam. Tena ninaamini, wakazi wa Sinza ni wengi zaidi ya idadi hiyo.

Unaweza kujiuliza kwamba vipi leo watu wanashangaa taifa lenye watu wapatao 350,000 kuonekana ni gumzo. Unaweza ukawa na hoja au sababu ya kuwa watu wanaoingia uwanjani ni 11 tu!



Lakini taifa kubwa unalijua, wingi wa watu una maana kubwa na inaumiza kusikia taifa lenye watu wapatao milioni 52, limekuwa na ndoto ya kucheza Kombe la Dunia kwa zaidi ya miaka 50 na hakujawahi kuwa na mafanikio hata kidogo.

Unaweza kujiuliza kuwa nchi yenye watu wengi zaidi wenye vipaji imeshindwa kuwa na mipango madhubuti ya kufikia katika sehemu ambayo inaweza kuweka rekodi ya kuifanya ijuvunie.

Nchi yako wewe ni Tanzania, ndiyo nchi yangu mimi. Haimilikiwi na mtu yeyote zaidi ya mimi na wewe lakini tuliowakabidhi dhamana ya kuuendesha mpira wetu wameendelea kuwa wababaishaji, wasio na upendo na wanaotaka kudumisha ubora wa matumbo yao na nafsi zao.

Ukisikia Iceland inakwenda Kombe la Dunia, ni jambo ambalo linaumiza kwa kila Mtanzania mpenda soka ambaye amekuwa na ndoto ya kuona nchi yake inapata mafanikio.



 Hata kama idadi ya wakazi siyo jambo kubwa, lakini najiuliza idadi ya wakazi angalau kama kitongoji cha Sinza, Dar es Salaam au Nyakato, Mwanza au Mwanjelwa, Mbeya au Bachu, Tabora wanaweza kucheza Kombe la Dunia na Tanzania yenye watu takriban milioni 52, ndoto ilishakufa!

Nani kati yetu anaweza kunyoosha mkono na kusema nafasi ya Tanzania kwenda Kombe la Dunia ipo? Atakayesema hivyo labda atakuwa ni mwanasiasa na hajui nini kinaendelea katika mchezo wa soka hasa roho mbaya za viongozi waliopewa nafasi ya kuuongoza mchezo huo.

Viongozi wamekuwa tatizo kubwa, wameuua mchezo kwa roho mbaya zao za kukubali ufe lakini wao waishi maisha mazuri na matamu bila ya woga au huruma hata kidogo. Wamekuwa waongo, walaghai, wabinafsi walio tayari kuwaweka ndugu na rafiki zao katika nafasi nyeti za maendeleo huku wakijua hawana uwezo.

Hawajali kwa kuwa wanajua wanachotafuta ni mafanikio yao binafsi badala ya maendeleo ya soka. Hawajali kwa kuwa wanajua hakuna wa kuwafanya lolote na hawaogopi kwa kuwa wanaamini wakifanya madudu, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) litajitokeza kuwakomboa kwa kisingizio kuwa “wanaingiliwa”.

Iceland hawajafanya mambo mengi sana kufuzu. Badala yake wamekuwa wakweli, wenye nia, wenye kutaka kubadili mambo na kuipa heshima nchi yao.

Hauwezi kutamani kuipa nchi yako heshima huku ukiwa unafanya mambo yanayoondoa upendo wako kwa nchi au taifa unalolitumikia.

Angalia thamani ya wakazi 350,000 wa Iceland wanaofaulu mtihani mgumu uliowashinda asilimia 50 ya milioni 52.


Inawezekana Iceland imewashitua na kuwashangaza wengi sana. Kila mmoja anaweza kuwa na fikra zake binafsi lakini ukweli kwa mawazo ya sisi Watanzania, tunapaswa kujitafakari na hasa waliopewa dhamana ya kuongoza mchezo wa soka, nao waone aibu na ikiwezekana mabadiliko yaanze sasa maana tusitegemee miujiza kufikia mafanikio huku tukiendelea kufanya madudu kama wadudu.

2 COMMENTS:

  1. Brother huwezi kujua udhaifu wetu watanzania kama hujaishi au kutembelea nchi za wenzetu . Sisi watanzania ni watu wa hovyo sana tena sana. Na si katika michezo tu bali katika mfumo mzima wa maisha yetu. Utasikia vijana wanalia na ajira jamani? Katika familia ya kitanzania mtu hapungui kuwa na watoto angalau sita. Acha familia chukulia ukoo mzima una wanafamilia wangapi? Achana na ukoo chukulia mtaa au kijiji ina vijana wangapi? Wakikusanya nguvu zao kama community moja wazalishe mchezaji mmoja caliber au kiwango cha samata na kucheza nje ya nchi basi tayari wamezalisha ajira katika familia au umma achana na cristian ronaldo. Vijana wanaachwa wanadhurura hovyo mpira pesa tena si mchezo na vijana ndio makinikia yenyewe hadimu yanayozalisha mpira. Drogba mmoja alijenga hospital licha ya kuzalisha ajira anaokoa maisha ya watu. Amini hakuna kipya wanachokifanya wenzetu sisi tushindwe isipokuwa sisi watanzania ni wazembe. Vipi wakenya miaka nenda miaka rudi watuzidi kwenye riadha wakituacha tumelala kama tumekufa wanakipi kipya? Riadha ni pesa na si pesa tu bali ni dili heavy ya kuipa kiki nchi duniani. Wkati mwengine unataka kulia. Utasikia watu wanampiga vita Maghuful? Maghuful anawaamsha watanzania yaani kila ukimsikiliza na kumtizama Magufuli huwezi amini kuwa ni mtanzania au kapandikizwa kutoka nje ua nchi yetu. Anaupeo na maono tofauti kabisa na watanzania wa kwaida. Mabadiliko ya mara kwa mara anayoyafanya katika serikali yake inadhihirisha kuwa hajalala na yupo katika mapambano ya kutafuta watu sahihi wakuleta mabadiliko ya kweli nchini. Mpira wetu unahitaji mabadiliko makubwa kwanza hatuhitaji kocha bali tunahitaji manager who can manage and overhaul the whole of our football program kuwa na mtu kama Mayanga kuwa ndio kocha mkuu wa timu za taifa ni aibu hata yeye mwenyewe Mayanga kama angelikuwa mzalendo wa kweli asingekubali kuchukua zamana ile basi bora kumuachisha kucheza mpira wa kulipwa Samata na kumpa anachotaka ili aje kuwa kocha kuliko kuwa na kocha kiwanago cha Mayanga ni upuuzi mtupu. Wazungu wanasema if you don't spend enough today don't come and complain tomorrow cause you wont be satisfied. Tunahitaji watu madhubuti wa kuwaaminisha vijana kuwa 100% wanaweza kuwa kama mchezaji yeyote duniani kujiamini ndiko kunakomfanya simba kumuangusha nyati sio nguvu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic