Na Saleh Ally
MMOJA wa wadau wa soka nchini Tanzania ambaye ni kivutio kwa mashabiki wengi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, maarufu kama ZHP.
Hans Poppe ambaye ni askari mstaafu na mfanyabiashara maarufu katika masuala ya usafirishaji, alikuwa kimya kwa kipindi kirefu baada ya kusafiri nje ya nchi ambako alikuwa akishughulikia masuala yake mbalimbali ya kifamilia.
Mara baada ya kurejea, SALEHJEMBE ilifanya kazi ya kumtafuta na kufanikiwa kumpata ili kujua mambo mengi ukiwemo mustakabari wa mwendo wa kikosi cha Simba ambacho yeye ndiye mhusika namba moja katika usajili.
Simba iko kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi 5, imeshinda tatu na kupata sare mbili ikiwa na mabao 14 ya kufunga na kufungwa matatu.
Hans Poppe ambaye si mtu wa kumung’unya maneno, anasema bado hajafurahishwa na mwendo wa kikosi cha Simba kwa kuwa hauaminiki.
“Hatuna mwendo mzuri kwa kweli, kesho ushindi na mechi inayofuata hamna uhakika. Kama kikosi tunacho kipana lakini namna ya kukitumia naona kama inatupiga chenga,” anasema.
Alipoulizwa kusema kinawapiga chenga ni sawa na kusema benchi la ufundi bado halijafanya kazi yake vizuri.
“Kweli, ukisema benchi la ufundi ndiyo kazi yao, wakati ule ilionekana tunakosa mabeki, alipoumia Mwanjale ikawa shida, utaona Mavugo alionekana yuko yeye tu, lakini sasa utaona tuna yeye, Mavugo na kadhalika.
“Hivyo tuna kikosi kikubwa na imara kabisa. Ndiyo maana ukiniambia nitoe mawazo, naweza kusema kwa mabao si mbali sana, lakini kwa pointi tumebaki nyuma.
“Kwangu angalau kila mechi tushinde mabao matatu hivi ndiyo itakuwa hadhi ya kikosi chetu,” anasisitiza Hans Poppe.
Pamoja na kutaka kikosi chake kifunge mabao mengi, Hans Poppe anasema bao la Mavugo lililokataliwa katika mechi dhidi ya Stand United, ni sehemu ambayo inaweza ukawa mwamko wa kuwakumbusha waamuzi.
“Kila mmoja aliona bao lile lilikuwa sahihi kabisa, vipi mwamuzi alishindwa kujua, aliamua kukataa tu na hili si jambo zuri. Waamuzi lazima wawe makini na wahakikishe kuna haki ili kuepusha kuwakatisha tamaa wachezaji hasa inapotokea kama ulivyoona bao hilo la Mavugo.”
Wakati Hans Poppe akiwa nje ya nchi, moja ya gumzo ambalo huenda linaendelea kuguswa na wadau wengi wa soka nchini hasa mashabiki wa Simba ni kuendelea kwa aliyekuwa nahodha wa Simba, Jona Mkude “kuchezea” benchi.
Hans Poppe anasema Mkude anapaswa kuendelea kujituma ili kumshawishi mwalimu. Pamoja na hivyo, ana msisitizo kuhusiana na nidhamu.
“Wakati mwingine tukubali benchi la ufundi nalo lina maamuzi yake na kocha kama anaona mchezaji anafanya anachomuagiza na anamsaidia, vipi atamuweka benchi?
“Mkude aongeze kujituma, lakini pia adumishe nidhamu. Unakumbuka alishindwa kwenda Songea sijui alipitiwa usingizi au ilikuwaje. Kwa kocha naye ni binadamu, huenda hakufurahia na kadhalika.
“Kama hiyo haitoshi, utaona kuwa tulichofanya Simba safari hii ni kuweka wachezaji ambao watakuwa na ushindani katika kila namba. Si mchezaji mmoja tu katika namba, siku hayupo mnachanganyikiwa, kumbuka msimu uliopita tulikuwa tunawachezesha hadi akina Bokungu namna tano. Huo ndiyo ushindani na Mkude apambane atacheza tu,” anasema Hans Poppe.
Kimataifa:
Kumbuka Simba safari hii imerejea katika michuano ya kimataifa baada ya kubeba Kombe la Shirikisho na itashiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Hans Poppe anasema, kikosi chao kinaendelea na maandalizi kupitia mechi hizo za Ligi Kuu Bara.
“Wakati tunapocheza ligi, kocha anaendelea kukipanga kikosi na wachezaji wanaendelea kujiimarisha.
“Kikubwa kwetu kitakuwa ni ratiba, pale itakapotoka na kujua tutaanza na timu ipi basi inakuwa rahisi kujua maandalizi yetu yawe na uzito upi kulingana na timu tunayokutana nayo,” anasema Hans Poppe.
Pamoja na hivyo kumekuwa na taarifa kwamba Simba inataka kusaka kocha mpya kutokana na mwenendo kuonekana si mzuri na huenda Kocha Joseph Omog akapoteza nafasi yake.
“Kwanza nimekuwa nje ya nchi muda mrefu kidogo kwa hiyo kuna mambo kadhaa sijashiriki, lakini sioni kama kuna ubaya kama Simba itaamua kutafuta kocha.
“Kocha anaajiriwa kwa ajili ya kuleta matokeo, kama imeshindikana ni lazima kutafuta njia nyingi au kocha mwingine. Hivyo Simba kutafuta kocha wala halitakuwa jambo baya kama wanafanya hivyo.
“Jiulize kama matokeo si mazuri kuna ubaya gani kama utabadilisha. Uendelee kuumia kwa kuwa unahofia watu watalaumu! Unajua ndiyo inakuwa hivyo, viongozi wakiona tatizo wakalifanyia kazi watalaumiwa, wakisema wakae kimya watalaumiwa. Sasa kizuri hapo kuangalia kilicho sahihi.
“Hapa kikubwa ni kuangalia, kocha amefikia malengo. Kama ndiyo, basi aendelee kubaki kama hapana basi si vibaya kutatua tatizo.
“Kawaida Simba huwa hatupishani na makocha kwa ajili ya viwango vyao. Mara nyingi ni kwa ajili ya kipato, (Goran) Kopunovic alitaka tumlipe zaidi, angalia yule babu (Patrick) Liewig pia alitaka kulipwa zaidi ikawa vigumu. Hivyo ikitokea kocha tumeshindwana sababu ya kiwango, halitakuwa jambo la kushangaza,” anasema.
Ukiachana na suala la Omog, Hans Poppe pia amezungumzia suala la kiungo mpya wa Simba, Haruna Niyonzima ambaye amekuwa akilaumiwa kuwa hayuko katika kiwango chake.
“Kama utazungumzia ujuzi, Niyonzima yuko vilevile na hawezi kwisha. Ni kiungo mwenye uwezo sana na itafikia siku atafanya vizuri tu.
“Lakini sasa kuna tatizo la kujenga mjumuiko wa timu na kuzoeana. Utaona akiwa Yanga walikuwa wanajua atakwenda wapi, atapiga wapi au atafanya nini. Anakwenda anazoeana na wenzake na timu ni mpya, hivyo ni suala la subira tu,” anasema Hans Poppe au ZHP.
0 COMMENTS:
Post a Comment