October 9, 2017



NA SALEH ALLY
KIKOSI cha Taifa Stars kimemaliza mechi yake dhidi ya Malawi kwa sare ya bao 1-1 huku timu yetu ya taifa ikilazimisha kusawazisha.

Kwa waliopata bahati ya kuona mechi hiyo, Taifa Stars ilikuwa na nafasi ya kuongeza bao moja zaidi katika dakika za mwisho hasa ile krosi ya nahodha Mbwana Samatta ambayo kinda Mbaraka Yusuf alishindwa kuimalizia akiwa amebaki na goli pekee.

Mashabiki wa Tanzania kama ilivyo kwa wengine, wangependa kuona kikosi chao cha timu ya taifa kinafanya vizuri bila ya kujali ni mchezo wa kirafiki au wa mashindano. Raha ya ushabiki ni kuona unachokiunga mkono kinakuwa juu, imara au maarufu.

Hii ni kawaida duniani kote na tunapaswa kukubali kwamba mashabiki hawawezi kuwa wavumilivu kwa kiwango kikubwa kama tunavyotaka, badala yake wachache wenye subira wanaweza kusubiri na kusubiri, lakini wengi huchoka mapema.

Tena mimi ninaona, Watanzania pia wanapaswa kupewa pongezi. Hakika wamevumilia sana na mambo yamekuwa ni “Tia maji, tia maji” kwa muda mrefu. Hivyo tunapaswa kuwapa nafasi nao waseme maoni yao na kupunguza hasira ya kile wanachoona wanakosa.

Ukiachana na hicho, kikubwa kilichonivutia kuandika Metodo ya leo ni wachezaji wawili wa Taifa Stars kulambwa kadi nyekundu katika mechi hiyo, moja ikiwa ni ya moja kwa moja na nyingine ikitengenezwa na kadi mbili za njano.
Mwamuzi aliyetoa kadi hizo mbili nyekundu katika mechi ya kirafiki ni Mtanzania Israel Nkongo ambaye alianza kwa Erasto Nyoni na baadaye Mzamiru Yassin.

Nyoni alipewa kadi nyekundu moja kwa moja baada ya kuonekana amempiga kiwiko mchezaji wa Malawi waliporuka kupiga kichwa. Mzamiru akapewa kadi mbili za njano kutokana na kufanya madhambi.

Tukubali sote, kwamba wachezaji wote wawili wanatoka katika kikosi cha Simba na ungeona mjadala wa mtandaoni ulilalia kuwa wao wanatokea Simba na hawana nidhamu.
Lakini kwangu naona ni ishu ya wao kuishughulikia kama wachezaji na kwa kuwa walipata kadi wakiwa Taifa Stars ningependa kuangalia kipi naona ni sahihi na kipi la!

Kama ingekuwa ni mapenzi kwa taifa langu, hata mimi ningeshangazwa sana na Nkongo, kwamba vipi anafanya hivyo na wachezaji hawa tunawategemea baadaye. Ingewezekana ile kadi ya Nyoni, angekausha tu au kumpa njano na kumuonya na ile ya Mzamiru ya pili pia, angepotezea tu.

Lakini najiuliza, tunahitaji kuwa na waamuzi duni katika kiwango cha kimataifa kwa ajili ya kulisaidia taifa letu. Au tunakubali waamuzi wanapaswa kufanya kazi yao kwa ufasaha ili kufanikisha kile ambacho tunaona tunapungukiwa.

Kadi alizotoa Nkongo kwa wachezaji hao zilikuwa sahihi au la! Kama tunaona ni sahihi, kwa nini tunataka kuvunja uhalali ili kutengeneza uzalendo uliofanywa na wengine ambao hawakuwa makini na kuufikiria huo uzalendo. Tunamuona kama shetani lakini kama yuko sahihi, basi tujue ni shetani aliyelenga kutusaidia baadaye katika usahihi wa soka letu.

Kama tutakuwa tunakubaliana zile kadi zilikuwa sahihi, basi badala ya kumlaumu Nkongo tunatakiwa kumpongeza kwa kazi nzuri na baada ya hapo tutumie fursa hiyo kuwakumbusha Nyoni na Mzamiru kujifunza tena.

Hiyo ilikuwa ni mechi ya kirafiki, jiulize ingekuwa mechi ya kufuzu? Unaona Malawi walikuwa wamepaniki sana, ubabe ulitawala na ingewezekana Nyoni kwa uzoefu wake angeweza kuwa makini na kuepuka mengi. Wachezaji wa Malawi waliona mwisho wamezidiwa wakatumia muda mwingi kuanzisha mizozo na Nyoni ni kati ya walioingia katika mtego huo.

Ishu ya Mzamiru inaweza kuwa ni ishu ya kutojenga kumbukumbu, kwamba sasa ana kadi moja ya njano na uchezaji wake unatakiwa kubadilika kwa aina ipi na umakini uongezeke kwa kiwango kipi pia.

Simba itacheza michuano ya kimataifa, Nyoni na Mzamiru watarudi siku nyingine Taifa Stars. Badala ya kumlaumu Nkongo, bora kuangalia walipojikwaa na kupafanyia kazi. 


1 COMMENTS:

  1. Kwa hili,sikuungi mkono saleh!hakuna anaependa kumdekeza mwanae ikiwa anajua baadae ataharibikiwa.nkongo alishindwa kuumudu mchezo.kwa kosa la mzamiru ni sahihi alipaswa kutunza kumbukumbu na kuwa mwangalifu.ila kwa erasto hapana,kwanza ukiangalia urukaji wa erasto na yule forward ulikuwa 50;50 kwa utanuzi wa mikono.ila erasto alimzidi katika kuruka.na hakustahili strait red card.ukisema ike ni strait red card nikumbushe wapi erasto alionywa au niambie udhahiri wa faulo yake na kadi nyekundu.vipi mchezaji wa malawi kurudishia kwa erasto wakati filimbi alishapuliza?sheria inasema nini?vipi gadiel michal aliekaliwa makusudi na baadae akarudisha kwa kipepsi?Israel alichukua hatua gani?na kuna tofauti gani kati ya hayo matendo mawili?kwenye mambo yamsingi sioni tija ya kusema huyu ni wa simba ana huyu ni wa yanga.ni vema kuzungumza kama watanzania,sio kwakupendelea popote ila kuweka ukweli.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic