Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya anaamini bado ana nafasi ya kufanya vizuri na kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa barani Afrika.
Kichuya anaamini akiendelea kukomaa, itafikia siku atacheza soka la kulipwa kama ilivyo kwa nahodha wake katika kikosi cha Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta anayekipiga katikatimu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Kichuya ambaye msimu uliopita alifanikiwa kuifungia timu yake hiyo mabao 12 katika Ligi Kuu Bara, ameonyesha kiwango kizuri cha kuitumikia Simba na kuwa msaada mkubwa katika timu yake hiyo.
Kichuya amezungumza na gazeti hili na kusema kuwa moja ya mikakati yake ni kuona anafanikiwa kuvuka mipaka ya Tanzania na kwenda kucheza nje kama ilivyo kwa wachezaji wenzao waliowatangulia.
“Hicho alichokizungumza Samatta ni kama ametukumbusha, kwa kuwa kila mchezaji lengo lake ni kuona anafanikiwa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na hakuna asiyependa jambo hilo lisimtokee.
“Kwa upande wangu najipanga kuona nafanikiwa kufanya vyema kwenye ligi ili mwisho wa siku niweze kupata nafasi ya kwenda nje.
“Moja ya malengo yangu ni kuona siku moja natoka nje ya mipaka ya Tanzania na ninaamini hilo litawezekana kwa uwezo wa Mungu,” alisema Kichuya.
0 COMMENTS:
Post a Comment