NA SALEH ALLY
KATIKA moja ya mikakati mikubwa ya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) ni kuhakikisha kuna kozi nyingi na za kutosha za makocha wa makipa.
Mafunzo hayo yameanza kutolewa na makocha mbalimbali ambao wamepitia mafunzo ya kisasa zaidi kuhusiana masuala ya walinda milango.
Waliopewa kozi hizo zilizopewa jina la mbinu mpya za ulinzi, wao wanakwenda wanasambaa nchi moja baada ya nyingine wakitoa mafunzo kwa makocha wa makipa.
Msimu uliopita, klabu kubwa barani Ulaya zilitakiwa kutoa nafasi kwa makocha wao wa makipa kwenda katika kozi hizo za mbinu za kisasa za ulinzi.
Kozi hizo zilihusisha na wataalamu wa masuala ya mwili kisayansi au kibaiolojia ili kujua kipa anaweza kufanya nini kuulazimisha mwili wake kuwa bora zaidi au kufanya kitendo kulingana na hali halisi.
Matukio mengi wanayokutana nayo walinda milango uwanjani huwa ni ya kushitukiza. Takwimu zinaonyesha matukio ya kawaida ni asilimia 25 tu pale kipa anapokutana na timu yenye washambulizi wakali katika ushambulizi.
Kwa nyumbani, makipa hawana mafunzo ya kisasa zaidi kwani walimu wao hawajahudhuria kozi ambazo zingewasaidia kujiongeza zaidi.
Uefa imeungana na Caf katika kozi za makipa. Lakini bado kuna nafasi kwa Tanzania kupata wakufunzi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ili kuwaimarisha zaidi wakufunzi au makocha wa makipa hao.
Fifa imekuwa ikitoa nafasi ya wakufunzi kujifunza zaidi ili kusambaza ujuzi zaidi katika sehemu mbalimbali ambako mpira unachezwa.
Washambulizi wanafundishwa mbinu mpya kila kukicha kwa lengo la kuwazidi ujanja makipa. Lakini makipa wa Tanzania wanafundishwa mbinu zilezile na makocha wao wanakuwa hawajajifunza kuwafundisha.
Mfano, kocha mzuri wa makipa kama Juma Pondamali, mara ya mwisho lini alipata mbinu mpya za kuwanoa makocha wake au kocha wa makipa wa Simba, Muharami Mohammed, hali kadhalika na wengine wa Ligi Kuu Bara.
Nimekuwa nikisisitiza hili na huenda makocha wakafikiri kama ninawaandama, lakini kama watapata nafasi ya kujifunza tena watagundua wamechelewa mambo mengi sana kuliko wanavyojua.
Huenda wao pia wasiwe na kosa kwa kuwa wanahitaji kupata nafasi hiyo kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au klabu zao ili wajifunze zaidi ili baadaye wausambaze utaalamu mpya.
Makocha hasa wa kigeni, utaona wengi ni makocha wanaofundisha timu nzima na si makipa. Wanafanya hivyo kwa kuwa wanajua kuna makocha wa makipa.
Sasa wanaoachiwa kazi hiyo nao wanakuwa hawana kipya zaidi ya kuendeleza kilekile ambacho walijifunza mwaka 47 na mwisho kusababisha mambo kwenda kwa mazoea zaidi.
Iko haja ya kuangalia hili na kulifanyia kazi. Makocha wanaweza nao kuliangalia na kuliombea ili tupunguze kuwaona makipa wetu hawana kitu wakati wamekuwa hawapewi nafasi ya kujifunza zaidi.
Lakini wakati wanasubiri kupata nafasi hiyo ya kujifunza au kupewa mafunzo, bado makipa na makocha wao wanaweza kujisomea na kupata mambo mapya kuhusiana na mafunzo yao kupitia mitandao mbalimbali ya mafunzo.
Kujiimarisha kwa kujifunza kila kunapokucha ni jambo muhimu sana na si sawa kulichukulia kama la kawaida sana au kujiamini kupitia kipaji pekee.
Hamjachelewa kwa kuwa bado kuna nafasi na litakuwa ni jambo zuri zaidi kama mkiamini dunia inakwenda kwa kasi sana na kujifunza zaidi ni jambo zuri na inawezekana. Kila la kheri.
0 COMMENTS:
Post a Comment