December 22, 2017





Na Saleh Ally
MCHEZAJI anapofikia miaka 30 katika ligi yoyote ya mchezo wa soka ambayo ni ya ushindani, thamani yake inakuwa imefikia katika kiwango kinachojulikana kama “kuporomoka”.

Kawaida kuanzia miaka 25 kupanda, ile hali ya hofu ya biashara inaanza kuingia. Timu nyingi zinazowanunua wachezaji huanza kujiuliza mara mbili au tatu, sababu kubwa ya msingi kuwanunua wachezaji hao.


Wengi hawajui, muda wa mchezaji kuwa uwanjani ni mdogo sana. Miaka kumi inaweza kuwa mingi akicheza katika kiwango cha juu na huenda kuanzia miaka 20 hadi 30, baada ya hapo huwa ni suala la kumalizia na kabla ya 20 huwa ni kutafuta nafasi.


Kwa Afrika suala la umri linaweza kuwa tatizo kubwa kwa sababu hizi mbili; moja ni wachezaji wenyewe kudanganya umri kwa kupunguza. Mwenye miaka 22 atasema ana 18 au 19 kwa lengo la kupandisha soko lake kwa kuwa wakati anaanza kucheza alichelewa, alipojitambua kwamba anaweza kufanya vizuri, tayari alikuwa na miaka 25. Anaona inakuwa vema kusema ana 20 ili aonekane kijana na soko lake kupanda.


Simba na Yanga zimecheza mechi 11 tu za Ligi Kuu Bara lakini ni timu zinazoongoza kuwa na majeruhi wengi kupita kiasi na huenda hii hali imezidi kwa msimu huu.


Ukiangalia Simba imekuwa na wachezaji zaidi ya watano waliokaa nje kwa muda mrefu zaidi. Hali kadhalika hali hiyo imewatokea watani wao Yanga.


Kuwepo kwa majeruhi wengi kwa Simba na Yanga, kuna wakati hadi ilisababisha mtafaruku na huenda suala hilo lilichukuliwa juujuu lakini ndani yake kulikuwa na ukweli.
Ukiangalia vizuri, wachezaji wengi walioumia au kuchelewa kupona ni wale ambao unaweza kusema umri wao ni wa miaka 30 au zaidi na kama ni miaka ya 20, basi lazima itakuwa ni kuanzia 27 kwenda mbele.


Wako wachezaji wa umri wa miaka ya 20 mwanzoni ambao waliumia na kurejea mara moja uwanjani kuendelea kuzisaidia timu zao au kuwa sehemu ya timu.


Katika majeruhi, unaweza kusema asilimia 25 ya wachezaji tegemeo hawakuwa na msaada mkubwa sana kwa Yanga au Simba kutokana na majeruhi ya muda mrefu kwa kuwa walioumia walikaa nje muda mrefu sana.

Yanga:
Hadi Yanga inacheza mechi 11 za ligi, tegemeo lake katika ufungaji, Amissi Tambwe hakucheza hata mechi moja kwa kuwa majeruhi na utaona ametumia muda mwingi kubaki akiendelea na matibabu kwa miezi mitatu au zaidi.
Baadaye umeona viungo tegemeo kama Thabani Kamusoko na hata Papy Tshishimbi ambaye alianza vizuri lakini akaishia kukaa benchi kwa takribani mwezi mzima.
Donald Ngoma naye amebaki nje kwa muda mrefu tena baada ya kubaki nje kwa muda mrefu mwishoni mwa msimu uliopita akijiuguza. Yanga ilikuwa kama imeachana naye lakini baada ya kusikia Simba wamezungumza naye, wakamuwahi uwanja wa ndege na kumsajili.
Obrey Chirwa, pia aliwahi kukaa nje kwa zaidi ya wiki tatu na wachezaji kadhaa vijana nao waliumia lakini walirejea mapema uwanjani kama ilivyokuwa kwa Juma Mahadhi na Matheo Anthony.

Simba:
Kwa upande wa Simba, kipa Said Mohamed ‘Nduda’, hajacheza hata mechi moja kati ya 11 kwa kuwa alipelekwa India kufanyiwa upasuaji na sasa ameanza mazoezi taratibu. Shomari Kapombe naye alikuwa majeruhi mara kadhaa tena mfululizo kabla ya kujiunga na Simba na hadi sasa yuko nje.

Method Mwanjale ameachwa Simba, lakini hakuna ubishi naye alikaa nje mara kwa mara na sasa Simba ina majeruhi wengine ambao ni Salim Mbonde na Haruna Niyonzima lakini usisahau hata Erasto Nyoni naye alilazimika kukaa nje.

Ninacholenga hapa, kwanza kuwakumbusha kuwa mchezo wowote, kuumia ni asilimia 100, hili ni la kitaalamu zaidi na inakuwa hivyo kwa sababu unahusisha watu kugusana na wakati wowote yanaweza kutokea majeraha.

Kwa mwanadamu kisayansi, kila umri unavyozidi, uwezekano wa kuumia unaweza kuongezeka kwa asilimia 15 lakini kwa mchezaji mwenye umri mkubwa anapoumia, uharaka wake wa uponaji una uharaka wa asilimia 25 tu tofauti na mchezaji kijana ambaye  hali ya kupona haraka inakuwa kwa asilimia 70 hadi 90.
Sisemi Yanga na Simba zisisajili wakongwe, lakini ninakumbushia mambo kadhaa na hasa suala la mchanganyiko wa wachezaji lakini wachezaji wenyewe pia kujitambua kulingana na umri wao.
Kila umri unavyopanda, basi mchezaji anatakiwa kujilinda au kufanya mambo yake pia akitambua umri wake. Inawezekana amepunguza umri au la, lakini ukweli atakuwa anaujua yeye na vizuri kujitambua.
Kawaida mwanadamu ana tabia ya kubishana na hali halisi. Hata mwenye miaka 35 hujiona kama bado ana 25 kwa kuwa haamini alipofikia na angependa kubaki alipokuwa jambo ambalo linaweza kumsababishia mazingira.
Bado klabu kubwa kama Yanga na Simba zinapaswa kuwa na kitengo cha uchunguzi au skauti watakaofanya kazi za kutafuta wachezaji kitaalamu zaidi na ikiwezekana wakati wa kusajili katika kujadili bei pia waangalie masuala ya umri na rekodi za wachezaji.
Mfano wachezaji wanaosajiliwa wakiwa na rekodi kubwa ya majeruhi na unakuta baada ya kuingia katika klabu badala ya kuanza kuisaidia lakini klabu inalazimika kumwaga fedha kuanza kumtibu.

Mchezaji kumsajili halafu nusu msimu akakaa nje wakati alikuwa akijulikana ana rekodi ya majeruhi si sahihi. Kusaini kitaalamu ni kujali vipimo vya afya.

Sijui kama mnajua, klabu za Ulaya au kwingine soka lilipopiga hatua huwapima wachezaji hata wachezaji wake inaotaka kuwaongezea mkataba ili kupata uhakika.

Umri unashusha bei, majeruhi yanashusha bei. Lakini hapa nchini klabu haiangalii na inawezekana kabisa, baadhi ya wahusika kupata kitu fulani inachangia haya yote kutofuatwa na mwisho klabu inaingia hasara kubwa.

Kuumia hakujali mkubwa wala mdogo ingawa kuna uwezekano wa kuepuka kwa upande mwingine. Lakini uponaji wa mkongwe na kinda ni mambo mawili tofauti kabisa.


Iko haja, Yanga na Simba zikajifunza jambo kupitia msimu huu kuwa haukuwa mzuri na zikipiga hesabu zitagundua zimepata hasara kwa kuwa zimelipa mishahara bila kupata huduma na zikalipa matibabu bila ya kupokea huduma pia na hata kama kuumia ni bahati mbaya lakini kuna sehemu umakini ungekuwa mkubwa, ingeepukika.

1 COMMENTS:

  1. SUALA LA UMRI NI INSHUU!!!
    Kwa kiwango kikubwa wachezaji tunaowachukua ni wale wanaokuja kupiga hela na kumalizia kipaji chao kwa kuwa umri unakuwa umesonga.Katika vilabu hivi vyetu viwili suala la kumchukua mchezaji ambae anahitajika kuvumiliwa kwa kuwa na umri mdogo ni ndoto. Simba na Nduguze Yanga wanahitaji mafanikio ya haraka.

    Umeona kilichomtokea yule kipa Mghana wa Simba???si majeruhi wala hakufungwa goli za hivyo ila hatuhitaji muda wa kupoteza. Uliona kwa Yossouf Aboubakar....tulishindwa kukaa nae kwa kuwa alikuwa kijana ila hatuna muda wa kupoteza. Sisi zetu ni magari ya mkaa braza and sistaz. Tunahitaji magari yaliyopigwa sana spana kwa kuwa tunaamini wanauzoefu wa barabara (Mashindano ya Kimataifa).

    Tunaweza kuwa na hela lakini tunashindwa kupata wachezaji bora kwa kuwa wachezaji wengi hawafikilii ligi yetu. Ukiona mchezaji umemshawishi kaja Tanzania basi ujue kaangalia maslahi na si kipaji chake. Mchezaji anaetakiwa na Keizer Chied, Mamelody nk..sis hatuwezi kumchukua.

    Yetu sisi ni gari za mkaa

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic