December 27, 2017



Na Saleh Ally
MWAKA 2009, nilifanikiwa kufanya mahojiano ya ana kwa ana na beki wa kulia wa Klabu ya Arsenal ya England.

Huyu ni Emmanuel Eboue, mahojiano yetu yalifanyika katika mji wa Blantyre nchini Malawi na ilikuwa ni baada ya kuunganishwa na nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Didier Drogba ambaye alinialika kwenda kufanya mahojiano naye wakati timu yake ikijiandaa kucheza na wenyeji Malawi.
Eboue ni mtu mzuri sana ingawa katika mahojiano yetu na gazeti hili la Championi, ana kasoro moja tu nayo ni suala la hasira, ukiachana na hilo, hana kingine anachoweza kujilaumu.

Nilipomuuliza kuhusiana na familia, alimsifia sana mkewe Aurellie ambaye alimuoa miezi michache kabla ya kujiunga na Arsenal akitokea Beveren ya Ubelgiji ambako anatokea mkewe. Hata hivyo, Eboue ambaye si muoga kwa maana ya kimsimamo, alisema hauwezi kujua mambo ya Mungu.

“Furaha katika maisha yangu ipo juu, hata hivyo hauwezi kujua kuhusiana na baadaye, hayo tuyaache. Lakini kwa sasa, nina familia yenye furaha,” anasema.


Nilipomuuliza kama suala la kuoa wanawake kutoka Ulaya ni jambo jema kwa wachezaji hasa waliofanikiwa kifedha badala ya kuoa Afrika, akanijibu hivi:

“Uamuzi wa mtu unatokea ndani ya moyo, hasa suala la mapenzi. Lakini mapenzi ya wanawake wa Ulaya, baba anaweza kuwa hatarini lakini watoto mara nyingi huwa salama.”

Maneno hayo ya mwisho ndiyo yaliyonivutia kukumbushia kwa ufupi mahojiano yangu na Eboue hasa baada ya kusoma Gazeti la Sunday Mirror la Uingereza na kuona picha za video akifanyiwa mahojiano na kueleza namna alivyo na maisha magumu.

Eboue amesema sasa analala chini, anaishi kwa kujificha akiwa na hofu kubwa ya kupokonywa nyumba yake huku akiwa hana hata kazi ya kufanya. Wakati mwingine analazimika kupata msaada wa kifedha kutoka kwa dada zake wanaoishi maisha ya kawaida kabisa nchini England.



Amesema atapigana hadi mwisho kuhusiana na amri ya mahakama inayomtaka kumuachia mkewe mali kwa madai yeye hawezi kuziendesha kwa kuwa “hajasoma”, hivyo hata watoto wao watatu hatakiwi kuonana nao wala kuzungumza nao kwa kuwa anaonekana hawezi kuwajali, anaweza kuwaathiri kutokana na elimu yake kuwa duni. Eboue hakwenda shule katika kiwango kizuri kwa kuwa alichagua mchezo wa soka.

Ameichezea Arsenal mechi 132, ni mmoja wa wachezaji waliocheza mechi nyingi za Ligi Kuu England pia kati ya walioitumikia Arsenal kwa muda mrefu na alikuwa akiaminika katika kikosi hicho chini ya Arsene Wenger na pia kile cha timu ya taifa ya Ivory Coast alichokotumikia kwa mechi 79 kuanzia mwaka 2004 hadi 2013.

Eboue kwa sasa anapanda basi na treni kwa kuwa hana fedha ya kununua usafiri binafsi wakati akiwa anacheza Galatasaray ya Uturuki alikuwa akiingiza kitita cha pauni milioni 1.3 (Sh bilioni 3.8) kwa mwaka.
Amesema: “Ninapoingia kwenye basi au treni, nalazimika kujificha, baadhi ya watu wamekuwa wakinijua na kushangazwa sana na kuniona pale.”
Eboue wakati mwingine analazimika kutembea umbali mrefu kwa kuwa hana fedha za kulipia usafiri wake wa basi wala treni. Ameeleza anavyolala barazani kwa rafiki yake wakati mwingine kulala bila ya kula.


 Muda wa yeye kukabidhi nyumba kwa mkewe umefika, kama atachelewa, kama jaji atapitisha, maana yake atatolewa msobemsobe nje kama mwizi ili nyumba apewe mkewe kwa kuwa ni msomi.
 Maumivu zaidi kwamba hata watoto wake Clara (14), Maeva (12) na Mathis (9) nao hatakiwi kuwa na mawasiliano nao kwa kigezo cha elimu duni alichotumia mkewe kummaliza kwa makusudi kabisa.


Eboue sasa ni masikini baada ya juhudi kubwa za kupambana uwanjani kutengeneza fedha kwa ajili ya maisha yake ya baadaye. Jambo baya kabisa ambalo linathibitisha wanawake wa Ulaya wamelenga kuchuma kupitia wanasoka wa Kiafrika wanaopata mafanikio barani humo na vyombo vya sheria vimejipanga kuwasaidia.
 Fedha zinazoonekana kugombewa au mali, zimepatikana uwanjani kwa juhudi na wala si elimu. Aurellie alijua anaolewa na mwanasoka ambaye hana elimu ya daktari au mwanasayansi anayetengeneza ndege na hili limewatokea wanamichezo kadhaa wa Kiafrika kupitia wanawake wa kizungu.

Kuna jambo la kujifunza hapa kwa haya yanayomtokea Eboue hata sisi tuna wanasoka wetu wanaocheza nje ya Tanzania, kwamba wanapaswa kuwa makini na wakumbuke, wanawake wa kizungu, mara zote wana malengo ambayo yanaweza kuwa tofauti na ya wanaume wa Kiafrika wanaokuwa nao.

Sijui kama wanasoka wa Tanzania wanaocheza nje ya Afrika nao wana mpango wa kuoa wazungu, lakini najua wengi wanaweza kulitumia sakata la Eboue kama funzo kuu la maisha kwamba unapopambana kusaka maisha, unakumbuka kuna maisha baada ya soka.

Tayari kuna taarifa klabu ya Galatasaray imejitokeza kumsaidia kazi Eboue awe sehemu ya makocha wake, lakini utaona shida aliyonayo wakati alikuwa akikusanya mamilioni ya fedha.

Wewe unayekusanya mamilioni ya Kitanzania sasa ukiwa maarufu unahifadhi fedha? Umejiandaa kwa ajili ya kesho na una mpangilio sahihi wa mali zako kisheria au katika mfumo bora unaokulinda wewe?

Wakati mwingine vizuri kuwaamini watu wa karibu yako, lakini wakati mwingine si sahihi, hivyo lazima kuinua macho badala ya kuacha maisha yaende kwa juhudi na maarifa kutafuta kilicho sahihi lakini mwisho uwe wa majonzi makubwa kama ilivyo kwa Eboue ambaye nilipokutana naye Malawi, inaonyesha wazi alikuwa na hofu lakini inaonekana hakuifanyia kazi kuwa katika njia sahihi, ndiyo maana anateseka namna hii, leo


1 COMMENTS:

  1. NIMEKUELEWA EBOUE.....:
    “Uamuzi wa mtu unatokea ndani ya moyo, hasa suala la mapenzi. Lakini mapenzi ya wanawake wa Ulaya, baba anaweza kuwa hatarini lakini watoto mara nyingi huwa salama.”

    Sentensi ya kishujaa aliyokuwa nayo kaka mkubwa. Aliamin kutoka moyoni wanawake wa Ulaya si watu sahihi ila alijitolea muhanga kwa mustakabari wa maisha ya watoto wake. Aliamini watoto wake wataishi poa kwa kuwa mama yao atakuwa ni wa Ulaya.

    Hata yeye akipata shida si kibaya ila watoto tu waishi poa. Hii ni sawa na mtu anaeamua kujitolea muhanga kwa ajuli ya kizazi chake. Emmanuel Eboue mwanasoka wa Afrika mwenye upeo wa Kiafrika. Alikuwa na mawazo ya Kiafrika ili kuifanya Afrika iwepo Ulaya. Nimekubali mawazo yako kaka...maana sentensi kama zako zipo huku mtaani

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic