Ule ujio wa straika mpya wa Simba, raia wa Msumbiji, Antonio Domingos, umempa matumaini kocha msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma ya kufanya vema kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Domingos alisaini mkataba wa miaka miwili wiki iliyopita ya kuichezea Simba pamoja na beki wa kati Mghana, Asante Kwasi akitokea Lipuli FC ya Iringa.
Mshambuliaji huyo, ametua kuichezea Simba akichukua nafasi ya Mrundi, Laudit Mavugo, aliyeachwa kwenye usajili huu wa dirisha dogo la usajili.
Djuma alisema amefurahishwa na usajili huo uliofanywa na mabosi wake, kwani ni wachezaji waliopendekezwa na benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mcameroon, Joseph Omog.
Djuma alisema katika mechi zilizopita za ligi kuu, timu yao imekuwa ikipata ushindi wa mabao machache, lakini ujio wa Domingos utaimarisha safu yao ya ushambuliaji inayoongozwa na Mganda, Emmanuel Okwi na John Bocco.
“Nimefurahishwa na usajili uliofanywa na viongozi ambao umezingatia maelekezo yetu kiufundi, kwani wamesajiliwa wachezaji wale tuliokuwa tunawahitaji katika kuimarisha kikosi chetu.
“Niseme kuwa, usajili wa Domingos utaiwezesha timu yetu kupata ushindi wa mabao mengi tofauti na michezo iliyopita ya ligi kuu ambayo tulikuwa tunashinda idadi ndogo ya mabao.
“Ninaamini uwezo mkubwa wa Domingos, hivyo kwa kushirikiana vizuri na Bocco, Okwi basi ninaamini tutapata idadi kubwa ya mabao katika mechi zijazo,” alisema Djuma.
0 COMMENTS:
Post a Comment