Na Saleh Ally
NILIZUNGUMZA na ndugu wa Haruna Niyonzima, yalikuwa ni mazungumzo ya kawaida kabisa lakini kwa kuwa tumezoeana siku nyingi tokea nilipokutana naye jijini Kigali, Rwanda mwaka 2007, alikuwa ni muwazi na tayari kunieleza karibu kila ninalotaka kujua.
Wakati wa mazungumzo yetu ya kawaida, liliingia suala la Niyonzima kutofanya vizuri. Gumzo lilianzia makocha kumkosea Niyonzima, yeye akiamini kumchezesha namba 11, bado ni tatizo kwa kuwa hata akiwa Yanga alishindwa kuonyesha soka kwa kiwango chake bora.
Akasisitiza, alidhani Simba wangemtumia kama namba nane na wangeshangazwa na mengi kwa kuwa hapo ni kama “nyumbani” kwake.
Mwisho mazungumzo yetu yalikwenda hadi aliponieleza namna Niyonzima alivyokata tamaa baada ya kutua Simba kwa kuwa inaonekana hawamuamini na hawajataka kumpa muda na anakatishwa tamaa kwa kuwa kila anachofanya anaonekana amekosea!
Ilikuwa rahisi sana kumuamini kuhusiana na maneno anayoyasema kwa kuwa najua ni mtu aliye karibu na Niyonzima na anaweza kuwa huru kwake zaidi yangu au watu wengine.
Siku chache baada ya kukutana na ndugu wa Niyonzima, nilikutana na kiongozi wa Simba ambaye aliponiona katika sehemu niliyokuwa nimekaa alinifuata, nami nikasimama kumsalimia. Kidogo tukaanza kujadili masuala ya soka na kitu cha kwanza aliniuliza namuonaje Niyonzima kama kweli anaweza kuwasaidia?
Nilishangazwa na swali hili na kwa kuwa dirisha dogo la usajili lilikuwa limekaribia kufunguliwa nilimuuliza kama walitaka kumuacha akacheka na mwisho akanieleza walikuwa hawaelewi walikuwa sahihi au walikosea maana mambo yako ambavyo hawakutegemea.
Hiyo nayo sikutegemea kauli hiyo, hata kiongozi huyo niliona kama ameshituka namna nilivyoshangaa na mwisho nilimpa maoni yangu.
Kwanza sina hofu na Niyonzima hata kidogo, kusema hajui mpira au hawezi kuwa na msaada kwa Simba ni kuonyesha haujui lolote kuhusiana na mchezaji huyo.
Lakini kuna kila sababu ya kukubali mambo kadhaa, kwamba mchezaji naye ni mwanadamu na lazima ujue unapomchanganya na jambo fulani hata kama ana uwezo, basi anashindwa kufikia kiwango chake sahihi.
Niyonzima ni kati ya viungo bora waliowahi kutokea katika ukanda wa Afrika Mashariki na kama atatulia nakujua yuko katika wakati upi, ana nafasi ya kurejea na kuwashangaza wengi sana wakiwemo wale wanaoona kama amepotea.
Atakuwa na uwezo wa kuwashangaza pale atakapokuwa ametulia na tayari kufanya kazi. Anatakiwa kutulia kisaikolojia na kuepuka kutekwa na maneno ya kukatisha tamaa badala yake, ayachukulie maneno hayo positive wale wanaomvunja moyo iwe kama wanampa moyo ili afanye vizuri.
Niyonzima ni kiungo mzoefu, kuwa nahodha wa timu ya taifa si jambo dogo. Hivyo anatakiwa kutambua mashabiki wana haki ya kusema wanachosema kwa kuwa wakati mwingine wanaweza kulizungumzia wasilolijua lakini kwa kuwa wanataka kuona timu inashinda, basi wanaweza kusema lolote ilimradi.
Lakini yeye hawezi kufanikiwa kurejea katika kiwango chake na kuwa yule Niyonzima anayejulikana kama atatekwa na maneno ya mashabiki halafu asumbuke kutaka kuwajibu.
Wako wanaosema wanamuona klabu karibu kila siku, lakini inawezekana waliwahi kumuona siku moja tu. Pia kama mwanadamu ana haki ya kwenda kustarehe lakini hapaswi kuonekana kila mara huku akiona utendaji wake haujaimarika.
Wakati wa maandalizi ya msimu mpya, Niyonzima hakupata muda huo. Tayari hata yeye amewahi kulielezea suala hilo. Lakini bado haliwezi kuwa jibu sahihi kwa mashabiki au hata viongozi wa klabu kwa kuwa wanatamani kuiona faida yake.
Inawezekana kabisa viongozi wakawa wanamsema vibaya au mashabiki wanamuudhi kwa maneno ya shombo, lakini hatakiwi kuwajibu kwa maneno mengi. Badala yake kinachotakiwa ni kuwajibu kwa kazi bora uwanjani na kuisaidia timu yake jambo ambalo analiweza.
Kumekuwa na maneno mengi, mfano amecheza mechi 10 kati ya 11 na hajafunga hata bao moja. Kazi ya Niyonzima si kufunga pekee na huenda Kocha Joseph Omog ndiye anajua zaidi. Na itakuwa vizuri viongozi waonyeshe wanajua hali ulivyo, wamuunge mkono na waepuke kuwa kama mashabiki.
Niyonzima anaujua mpira kweli lakini ili afanye kama anavyojulikana mambo mawili ni muhimu sana. Jambo la kwanza ni kujiimarisha kimazoezi ili kuwa fiti kwa kuwa hakupata muda lakini kingine ni kujiimarisha kichwani ili kukwepa maneno mengi ya mashabiki na hata viongozi, halafu aache miguu yake itoe majibu.
0 COMMENTS:
Post a Comment