January 10, 2018




Na Mwandishi Wetu
 MKURUGENZI wa Ufundi wa zamani wa Klabu ya Coastal Union, Nassor Bin Slum ameamua kuvunja ukimya na kusema klabu hiyo inakosa haki yake kwa kuwa tu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia ni mwanachama wake.

Bin Slum ambaye alikuwa ni mkurugenzi wa ufundi wa Coastal Union ikiwa Ligi Kuu Bara amesema, kumekuwa na njama za chinichini zinazofanywa kulitumia vibaya jina la Karia kwa lengo la kuiangusha Coastal Union ili isirejee ligi kuu.

Akizungumza na Championi Jumatano katika mahojiano maalum, Bin Slum amesema njama hizo zinafanyika kwa juhudi kubwa na baadhi ya viongozi wa timu nyingine za Ligi Daraja la Kwanza kwa kuwa wameingia woga kutokana na ubora wa Coastal Union.

“Mimi ni mwanachama na mdau mkubwa wa Coastal Union, nimekaa kimya sana kwa muda mrefu lakini naona kama mwisho nimechoka na itakuwa ni vizuri sana kama nitavunja ukimya katika hili suala.

“Coastal Union ina kikosi bora kabisa, tumechanganya wachezaji wakongwe kama akina Athumani Iddi Chuji, kipa (Hussein Sharrif) Casillas na wengine pamoja na wachezaji bora ambao ni damu changa.

“Lengo lilikuwa ni kujenga kikosi sahihi ambacho kitarejea ligi kuu na kimekuwa kikipambana kweli kwa kuonyesha soka safi kabisa. Lakini ajabu hakuna anayeona ubora wa kikosi hicho zaidi ya kusema maneno ambayo si sahihi,” anasema Bin Slum na kuongeza.

“Kila timu inayokaribia kucheza na Coastal Union utasikia Coastal lazima watashinda kwa kuwa ni timu ya Rais wa TFF yaani Karia. Kila mechi utasikia hivyo lakini ukweli hakuna hata mmoja amewahi kuonyesha ameonewa wapi.

“Hili jambo limezidi kuota mizizi na linasambazwa kwa makusudi, mimi ninajua lengo ni kuidhoofisha Coastal Union, kitu ambacho si sahihi hata kidogo kwa kuwa nawashauri vizuri kuachana na propaganda ili tucheze mpira.

“Kweli Karia ni mwanachama wa Coastal Union, kweli anashabikia lakini lini Coastal imependelewa? Upendeleo katika kitu gani? Mara ngapi tunapata matokeo mazuri hadi ugenini tena tukiwa tumeonyesha soka safi sana!”

Bin Slum anasema kuna baadhi ya viongozi wa timu wanazoshindana nazo wanafanya makusudi kwa kufanya propaganda kwa lengo la kutaka kuonyesha Coastal Union inapendelewa.

“Kinachonisikitisha zaidi kuna vyombo vya habari navyo vinakubali kutumika kwenye propaganda hii. Mfano leo Coastal inacheza na Mufindi Jumamosi, ajabu tayari wameanza kusema wataonewa.

“Kama kuna timu nyingine zinafanya uonevu, basi TFF inapaswa kukemea ili hili suala liishe na haki itendeke. Lakini Coastal Union inashinda kwa uhalali na vizuri kukawa na juhudi na heshima ya namna watu wanavyojituma.

“Binafsi naona kama kuna suala la haki, huenda waamuzi wanaweza wakawa wanaingia hofu ya kuiminya Coastal kwa sababu hiyo lakini hakuna upendeleo,” anasisitiza.

Bin Slum amesema Watanzania wapenda mpira wanajua Karia kuwa ni mtu mwadilifu na hakuna anayeweza kuhoji utendaji wake bora na mtu asiyependa longolongo.

“Nakuhakikishia, hata kama Karia ni shabiki wa Coastal Union na wachezaji wasifanye juhudi ya kucheza na kushinda, hawatapanda na ikiwezekana wanaweza kuteremka.

“Karia ni mtu asiyetaka mchezo linapofikia suala la uadilifu, hapendi kupindisha mambo na si mtu wa kutumia njia za mkato. Hivyo ukweli ni kwamba Coastal Union inafanya kila linalowezekana kwa juhudi kubwa kabisa kuhakikisha inapanda na si kwa ajili tu eti Karia ni kiongozi wake,” anasema.

 Bin Slum amesisitiza na kuwataka wanaoiunga mkono kutokatishwa tamaa na maneno ambayo wanayaona hayana msingi wala ukweli wowote badala yake waendelee kuiunga mkono klabu yao kwa niaba ya Mkoa wa Tanga.

“Mashabiki waendelee kuiunga timu mkono na hata ikipanda hakutakuwa na jipya kwa kuwa hii si mara ya kwanza kupanda ligi kuu na sote tunajua Karia hakuwa kiongozi wa TFF. Ilipoteremka daraja alikuwa makamu wa Rais TFF na bado ikateremka.

“Msisitizo wangu kwamba ni wanachama na mashabiki waachane na maneno hayo yasiyo na tija badala yake waisaidie Coastal Union kuiunga mkono hadi ifikie malengo yake,” anasema.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic